• HABARI MPYA

    Wednesday, August 22, 2012

    SIMBA NA AZAM SEPTEMBA 8 TAIFA NGAO YA JAMII

    Simba na Azam walivyokutana mara ya mwisho Kombe la Kagame

    Na Mahmoud Zubeiry
    MECHI ya Ngao ya Jamii ya kuashiria kufunguliwa kwa pazia la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, inatarajiwa kuchezwa Septemba 8, mwaka huu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ikizikutanisha bingwa wa ligi hiyo, Simba SC na washindi wa pili, Azam FC.
    Habari za ndani kutoka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), zimesema kwamba, kuchelewa kwa mechi hiyo ambako kumeenda sambamba na kuchelewa kuanza kwa ligi hiyo, kumetokana na kuchelewa kufikiwa mwafaka mapema wa mkataba mpya wa udhamini wa Ligi Kuu.
    Mkataba wa awali wa Vodacom na TFF unafikia tamati mwishoni mwa mwezi huu na kusainiwa mkataba mwingine, baada ya majadiliano yanayoendelea.
    Lakini kwa kuwa Mkutano Mkuu wa TFF uliopita uliridhia kuanzia msimu ujao Ligi Kuu iendeshwe na kampuni itakayoundwa na klabu za Ligi Kuu mjadala kuhusu udhamini mpya wa ligi umekuwa mrefu kutokana na kuhusisha pande tatu, klabu, wadhamini na shirikisho.
    Lakini sasa, kwa vyovyote, hata maridhiano ya mkataba mpya wa udhamini na Vodacom yachelewe tena, mechi hiyo itachezwa Septemba 8, ikiwa ni wiki moja kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu.
    Kihistoria hiyo itakuwa mechi ya tano ya Ngao ya Jamii kuchezwa nchini na ya pili kuishirikisha timu nje ya wapinzani wa jadi wa soka ya Tanzania, Simba na Yanga.
    Mtibwa ilicheza na Yanga mwaka 2009, baada ya Simba kugoma na ikashinda mabao 2-1 na kutwaa Ngao, wakati kabla ya hapo, mwaka 2001, Ligi Kuu ya Tanzania ikiwa bado inadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia ya Safari Lager, ilichezwa mechi ya kwanza ya Ngao kihistoria.
    Katika mechi hiyo, Yanga ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Simba na mwaka juzi Yanga iliifunga tena Simba kwa penali 3-1 kufuatia sare ya 0-0 na mwaka jana, Simba ilitwaa Ngao ya kwanza katika historia yake, kwa kuifunga Yanga mabao 2-0. 

    MABINGWA WA MECHI ZA NGAO YA JAMII:
    Mwaka               Mshindi       Matokeo     
    2001                   Yanga          2-1 Simba
    2010                   Yanga          0-0 Simba (3-1penalti)
    2011                   Simba           2-0 Yanga
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA NA AZAM SEPTEMBA 8 TAIFA NGAO YA JAMII Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top