• HABARI MPYA

    Friday, August 24, 2012

    BOCCO ADEBAYOR AFUZU SUPER SPORT, AZAM WATAKA MILIONI 300

    John Bocco 'Adebayor'

    Na Mahmoud Zubeiry
    MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, John Raphael Bocco ‘Adebayor’ amefuzu majaribio katika klabu ya Super Sport United ya Afrika Kusini na Azam FC inataka dola za Kimarekani 200, 000, zaidi ya Sh Milioni 300 kumuuza.
    Habari za ndani kutoka Azam FC, ambazo BIN ZUBEIRY imezipata zimesema kwamba pamoja na kutaka Milioni 300, Azam wametoa sharti la kupatiwa aslimia 15 Bocco atakapouzwa na klabu hiyo kwenda klabu nyingine.
    Bocco, ambaye amerejea nchini jana baada ya wiki mbili za majaribio na Super Sport, inaelezwa yeye mwenyewe ni kama hajaridhishwa sana na soka ya Afrika Kusini, kwani anaona kama haina ushindani na msisimko kama soka ya Tanzania kwa sasa.
    Pamoja na hayo, uongozi wa Super Sport unatarajiwa kuja Dar es Salaam wiki ijayo kufanya mazungumzo na uongozi wa Azam, ili wapunguziwe bei.
    Hata hivyo, Azam inaonyesha haiko tayari kumuuza mchezaji huyo chini ya dola 150,000 kwa sababu inaamini ni mchezaji bora ambaye anaweza kununuliwa kwa bei nzuri zaidi na timu nyingine baadaye.
    Inaoenakana Azam haina papara ya kumuuza Bocco kwa sababu mbali na thamani yake halisi kama mfungajin bora wa Ligi Kuu, mchezaji tegemeo wa timu ya taifa na klabu yake, lakini inaaminika kwa sasa mshambuliaji mwingine aina ya Bocco Azam hawawezi kumpata kwa urahisi kwa namna yoyote.
    “Mchezaji ambaye anaweza kufunga mara tatu katika mechi moja dhidi ya timu ngumu hapa kwetu kama Simba au Yanga si mchezaji rahisi. Hatukatai kumuuza, na hiyo ndio sera yetu, lakini lazima tumuuze kwa bei ambayo itakuwa na maslahi kwetu,”alisema kiongozi mmoja wa Azam.
    “Umefika wakati Watanzania lazima tuamke, Super Sport haichezi mara kwa mara michuano ya Afrika na kwa ujumla, hakuna timu ya Afrika Kusini inayofika mbali kwenye michuano ya Afrika. Na pia tujiulize katika miaka mitatu iliyopita, Super Sport imeuza wachezaji wangapi Ulaya.
    Tazama mtu kama Samatta (Mbwana) amenunuliwa na TP Mazembe (ya DRC) kwa zaidi ya dola 150,000. Hiyo ni timu ambayo inacheza hadi Klabu Bingwa ya Dunia, sasa wao Super Sport wana lipi la kutushawishi sisi na mchezaji mwenyewe zaidi ya fedha? Wao walete fedha tuwauzie mchezaji, ili tutafute mchezaji mwingine kama Bocco, Bocco ni lulu bwana,”alisema kiongolzi huyo.
    Super Sport ilivutiwa na soka ya Bocco, katika michuano ya Klabu Bingwa ya soka Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, mwezi uliopita, hivyo kumuita kwa majaribio na kama Azam itamuuza, ataweka historia ya kuwa mchezaji wa pili wa Tanzania kuchezea klabu hiyo, baada ya Suleiman Matola 2005 hadi 2007, akitokea Simba SC.
    Katika Kombe la Kagame, Bocco alifunga mabao matano na kushika nafasi ya tatu katika wafungaji bora, nyuma ya Hamisi Kiiza na Said Bahanuzi wa Yanga, aliyeibuka mfungaji bora.
    Lakini Bocco pia alikuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu uliopita, kwa mabao yake 18 akiwapiku hadi washambuliaji wa kigeni waliocheza ligi hiyo msimu huo, Felix Sunzu, Emmanuel Okwi, Kenneth Asamoah, Davies Mwape na Dalington Enyiana.
    Tangu aipandishe Ligi Kuu Azam FC msimu wa 2008/2009 kwa mabao yake, akiibuka mfungaji bora wa Ligi Daraja la Kwanza, Bocco amekuwa akiingia kwenye mbio za kuwania kiatu cha dhahabu cha Ligi Kuu, msimu wa kwanza akizidiwa na Boniphace Ambani aliyekuwa Yanga, msimu wa pili Mussa Mgosi aliyekuwa Simba na msimu wa tatu na Mrisho Ngassa, kabla ya msimu uliopita kutimiza ndoto zake za kuwa mfungaji bora wa ligi hiyo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BOCCO ADEBAYOR AFUZU SUPER SPORT, AZAM WATAKA MILIONI 300 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top