![]() |
| John Bocco 'Adebayor' wa Chamazi |
Na Mahmoud Zubeiry
MSHAMBULIAJI wa
kimataifa wa Tanzania, John Raphael Bocco ‘Adebayor’ leo anakamilisha muda wake
wa nyongeza wa kufanya majaribio katika klabu ya Super Sport United ya Afrika
Kusini.
Katibu wa Azam FC,
Nassor Idrisa ameiambia BIN ZUBEIRY kwamba, muda wa wiki
moja ya ziada ulioombwa na Super Sport kuendelea kumtazama Bocco unamalizika
leo na kuanzia jioni wanatarajia kupata taarifa mpya kuhusu mustakabali wa
mpachika mabao huyo.
Super Sport ilivutiwa
na soka ya Bocco, katika michuano ya Klabu Bingwa ya soka Afrika Mashariki na
Kati, Kombe la Kagame, mwezi uliopita, hivyo kumuita kwa majaribio, ambayo
akifuzu ataweka historia ya kuwa mchezaji wa pili wa Tanzania kuchezea klabu
hiyo, baada ya Suleiman Matola 2005 hadi 2007, akitokea Simba SC.
Katika Kombe la Kagame,
Bocco alifunga mabao matano na kushika nafasi ya tatu katika wafungaji bora,
nyuma ya Hamisi Kiiza na Said Bahanuzi wa Yanga, aliyeibuka mfungaji bora.
Lakini Bocco pia
alikuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu uliopita, kwa
mabao yake 18 akiwapiku hadi washambuliaji wa kigeni waliocheza ligi hiyo msimu
huo, Felix Sunzu, Emmanuel Okwi, Kenneth Asamoah, Davies Mwape na Dalington
Enyiana.
Tangu aipandishe Ligi
Kuu Azam FC msimu wa 2008/2009 kwa mabao yake, akiibuka mfungaji bora wa Ligi
Daraja la Kwanza, Bocco amekuwa akiingia kwenye mbio za kuwania kiatu cha
dhahabu cha Ligi Kuu, msimu wa kwanza akizidiwa na Boniphace Ambani aliyekuwa
Yanga, msimu wa pili Mussa Mgosi aliyekuwa Simba na msimu wa tatu na Mrisho Ngassa,
kabla ya msimu uliopita kutimiza ndoto zake za kuwa mfungaji bora wa ligi hiyo.



.png)
0 comments:
Post a Comment