HATIMAYE mambo yameanza
kumnyookea mshambuliaji chipukizi wa kimataifa wa Tanzania, Thomas Emmanuel
Ulimwengu baada ya kupandishwa rasmi kwenye kikosi cha kwanza cha klabu ya Tout
Puissant Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
![]() |
| Na Mahmoud Zubeiry |
Ulimwengu alisafiri na
Mazembe nchini Misiri kwa ajili ya mechi ya Kundi B ya Ligi ya Mabingwa Afrika
dhidi ya wenyeji, Zamalek ya Misri na alikuwa kwenye benchi kwa dakika zote 90 Jumapili
wakati wababe hao wa DRC wakiifunga Zamalek mabao 2-1 kwenye Uwanja wa chuo cha
Jeshi, Al-Qahirah mjini Cairo.
Katika mchezo huo ambao,
mshambuliaji mwingine chipukizi wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta ‘Sama Goal’
aliifunga Mazembe bao la ushindi dakika ya 44, akiunganisha pasi ya Tressor
Mputu Mabi.
Uli alisajiliwa msimu
uliopita Mazembe, lakini kwa muda wote amekuwa kwenye kikosi cha wachezaji wa
akiba hadi mwishoni mwa wiki, alipokaa kwenye benchi kwa mara ya kwanza pamoja
na kocha Msenegali, Lamine N’Diaye.
Katika mchezo huo wa
Kundi B, Himoonde alitangulia kuifungia Mazembe dakika ya 34 akimalizia pasi ya
Mputu, lakini Omotoyossi akaisawazishia Zamalek inayofundishwa na kocha Jorvan
Vieira dakika ya 36, pasi ya Mohamed Ibrahim.
Ushindi huo wa kwanza
ugenini kwa Mazembe katika hatua ya makundi, unaifanya TPM ifikishe pointi
saba, baada ya kucheza mechi nne, kushinda mbili, sare moja na Berekum Chelsea
na kufungwa moja na Al Ahly ugenini.
Al Ahly iliyotoa sare
ya 1-1 na Berekum Chelsea nchini Ghana Jumapili, bado inaongoza kundi hilo kwa
pointi zake 10, wakati wababe wapya wa Ghana wanashika nafasi ya tatu kwa
pointi zao tano na Zamalek wanashika mkia wakiwa hawana pointi hata moja.
Miezi miwili iliyopita,
nilifanya mahojiano na Makamu wa Rais wa Mazembe, Mohamed Kamwanya kuhusu
kuchelewa kwa Ulimwengu kuingizwa kwenye kikosi cha kwanza, ambaye alisema
kwamba mshambuliaji huyo anachelewa kwa sababu kiwango chake bado kidogo.
Alisema kwamba,
Ulimwengu kila anapopewa ruhusa ya kurejea Tanzania kujiunga na timu za taifa,
kwanza huchelewa kurudi Lubumbashi na pia hurudi akiwa hayuko fiti.
“Hicho ndio
kinamchelewesha, lakini kama siyo hivyo angekuwa anacheza tu kama mwenzake. Na
nyinyi watu wa vyombo vya habari mtusaidie, kwa sababu wachezaji wakija huko
wanafanya anasa, wanarudi huku hawako fiti, sasa inakuwa mbaya,”alisema
Kamwanya.
Mazembe ilifikia hatua
ya kuwazuia wachezaji wote hao, kurejea Tanzania kujiunga na timu za taifa, kwa
sababu hata Samatta inaelezwa anaporejea nyumbani, akirudi Lubumbashi anakuwa
ameshuka kiwango.
Hali hiyo imetafsiriwa
inatokana na wachezaji hao kufanya anasa wanapokuwa Dar es Salaam na chanzo ni
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuchelewa kuwapa tiketi wachezaji hao,
wanapomaliza majukumu yao ya kitaifa, hivyo wakati wasubiri tiketi wanaishia
kujirusha, kula bata kwa kwenda mbele.
Kwa kuwa kipindi chote
hicho wanakuwa hawafanyi mazoezi na wanaichosha miili yao kwa anasa,
wanaporekea Lubumbashi wanampa kazi kocha Lamine N’Diaye kuanza kuwatengeneza
upya.
Amechoka N’Diaye, aliweka
ngumu Uli hakurudi nyumbani kuichezea timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa
miaka 20, Ngorongoro Heroes na kwa kumkosa mpachika mabao wake huyo tegemeo,
sisiti kusema ilichangia kwa kiasi kikubwa kutolewa na Nigeria katika mbio za
kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika.
Hilo liliwafanya TFF,
walalamike sana hasa baada ya kumpiga stop na Samatta pia kujiunga na kambi ya
timu ya taifa ya wakubwa, Taifa Stars kwa ajili ya mchezo wa kirafiki dhidi ya
Botswana Jumatano iliyopita, ambao uliisha kwa sare ya 3-3 mjini Gabarone hadi
kutishia kulifikisha suala hilo Shirikisho la Soka Afrika (CAF), kwani
wamekiuka agizo la Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
Lakini leo TFF, wanasahau
kwamba, Mazembe ilikuwa ina hoja na lalamiko la msingi, ambalo naamini kesi
hiyo ikienda popote, klabu hiyo bingwa Afrika mara nne, itashinda.
Mchezaji ni mali ya
klabu na kanuni zinatoa mwongozo mzuri juu ya ushiriki wao kwenye timu za
taifa, hivyo hata vyama vya soka vina wajibu wa kuzitekeleza kanuni hizo.
TFF wamezoea kufanya
mambo kienyeji na ni jana tu kocha wa Yanga, Mbelgiji Tom Saintefiet
aliwalalamikia kwa kumchukua mchezaji wake, Said Bahanuzi akiwa mzima na
kumrejesha majeruhi, bila hata ya kutoa taarifa kwa klabu hiyo.
Tumekwishasau sakata la
beki wa Yanga, Stefano Mwasyika kuamua kujitoa timu ya taifa, baada ya
kutelekezwa alipoumia hadi klabu yake ikamtibu?
Bado wamekuwa hawajali
hata umuhimu wa kuwarejesha mapema wachezaji wa nje baada ya kumaliza majukumu
yao ya kitaifa.
Ndiyo maana ninasema, kabla
ya kuwahukumu Mazembe, tunapaswa kutafuta kiini cha ghafla mabingwa hao wa
zamani Afrika kupuuza wito wa TFF kutuma wachezaji Dar es Salaam.
Mara kadhaa nimekuwa
nikiwaona makocha wa nchi jirani, ambazo wachezaji wake wanacheza hapa Tanzania
wakija nchini kuwafuatilia wachezaji wao, mfano Mserbia Milutin Sredojevic
‘Micho’ wa Rwanda au Msoctland, Bobby Williamson wa Uganda.
Wanapokuwa hapa
hujionea wachezaji wao namna wanavyocheza na kufanya uteuzi kwa ajili ya timu
taifa, juu ya wachezaji ambao wanawajua fika. Micho anakwenda hatua kadhaa
zaidi, anawahangaikia wachezaji wa Rwanda kupata timu Ulaya, au nchi nyingine
Afrika, ambako watakusanya uzoefu zaidi na baadaye kuisaidia Amavubi.
Lakini sijawahi kusikia
hata siku moja kocha wa timu ya taifa, si Kim Poulsen tu, tangu Mdenmark
mwingine, Jan Poulsen aliyemrithi Marcio Maximo kutoka Brazil akisafiri kwenda
DRC kuwafuatilia Samatta na Ulimwengu, ama Kenya ambako katika Ligi Kuu tuna
mtu anaitwa Idrisa Rajab au Angola ambako tuna mtu anaitwa Said Maulid.
Huwezi kuniambia eti
leo SMG ana uzee wa kutelekezwa moja kwa moja timu ya taifa bila kuzingatia
uwezo wake unaomuweka katika moja ya ligi kubwa Afrika, Girabola, wakati mwaka
2000 mchezaji huyo akisajiliwa Simba SC kutoka Kigoma, Shaaban Nditi alikuwa
anacheza Singida United Ligi Kuu tangu 1999 na akina Kipanya Malapa na Edward
Rodgers Kayoza.
Wakati fulani, Jan
Poulsen alikwenda Sweden kumfuatilia Athumani Machuppa, kwa kuwa ni pua na
mdomo na kwao Denmark- lakini zaidi makocha wa Taifa Stars wamekuwa na desturi
ya kusubiri sifa za wachezaji kupitia vyombo vya habari ndipo wawaite, ndio
maana historia inamtaja Amy Ninje kama mmoja wa wachezaji wa zamani wa Taifa
Stars.
Baada ya mechi ya
kwanza dhidi ya Nigeria, Flying Eagles, kocha wa Ngorongoro Heroes, Mdenmark
Jakob Michelsen alisema kwamba ataongeza nguvu katika kikosi chake kwa kumuita
kiungo Adam Nditi wa Chelsea ya vijana ya England, ambaye tayari ameingia
kwenye programu za kukomazwa kwenye kikosi cha wakubwa cha mabingwa hao wa
Ulaya.
Sijui jitihada gani za
dhati zilifanyika- lakini nachokiona hapa kocha anatakiwa kusafiri hadi London
na kufika Stamford Bridge kukutana na makocha wa Nditi kuzungumza nao kuhusu
huyo mchezaji na kuzungumza naye mchezaji mwenyewe pia, kuliko kuzungumza
kwenye vyombo vya habari.
TFF inapaswa kumpa
fungu hata Kim akafuatilie na kujua kuhusu Nditi kama yupo kwenye nafasi ya
kuchezea Tanzania, kulikoni kuamua kwa kudhani tukiwa hapa nyumbani.
Sasa baada ya kumzuia
Uli kurudi Tanzania, ndani ya wiki mbili amepandishwa kikosi cha kwanza cha
Mazembe na kukaa benchi katika mechi ya Ligi ya Mabingwa- ina maana mwezi ujao
sasa tutakuwa tunazungumza habari nyingine kuhusu mchezaji huyu.
Kufanya vizuri kwa
wachezaji hawa ni faida kwa Tanzania pia- na kuwakwamisha kufanya vizuri ni
hasara zaidi kwa Mazembe, iliyowekeza fedha nyingi kwa nyota hawa, ingawa na
taifa letu pia litapoteza.
TFF kwao kupoteza si
hasara ndio maana hawakujutia Mwasyika alipovunjika goti na hawakujali Athumani
Iddi ‘Chuji’ alipopoteza mwelekeo, ndiyo maana hawakumsaidia, ingawa leo akiwa
amerudi mstarini, ndio wanaona umuhimu wake.
Sasa wakati TFF
wakilialia Dar es Salaam na kupigia mikwara ya kwenda CAF na FIFA kushitaki,
Ulimwengu ametupa jibu Mazembe walikuwa sahihi.



.png)
0 comments:
Post a Comment