• HABARI MPYA

  Jumatatu, Agosti 27, 2012

  YANGA WAREJEA LEO BAADA YA KUZOA 'POINTI SITA' RWANDA

  Said Bahanuzi kushoto katika mechi ya jana dhidi ya Polisi. Yanga ilishinda 2-1.


  Kiiza katika mechi ya jana

  Benchi la Yanga jana

  Kocha Mkuu, Tom Saintfiet akijadiliana na Msaidizi wake, Freddy Felix Minziro, nyuma yao wachezaji wakipsha jana. Picha zote na Saleh Ally, Mhariri kiongozi gazeti la Championi 
  Na Princess Asia
  MABINGWA wa soka Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, Yanga SC ya Dar es Salaam wanatarajiwa kurejea leo Dar es Salaam, baada ya kukamilisha ziara yao nchini Rwanda jana kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Polisi kwenye Uwanja wa Amahoro.
  Katika mchezo huo, Stefano Mwasyika aliisawazishia Yanga, baada ya Fabrice kutangulia kuifungia Polisi na Nahodha Msaidizi, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ akafunga la pili.
  Katika mchezo wa awali Ijumaa, Yanga waliwachapa mabingwa wa zamani wa Afrika Mashariki na Kati, Rayon Sport mabao 2-0 kwenye Uwanja huo huo wa Amahoro mjini Kigali.
  Yanga ambao siku moja kabla ya mechi hiyo ya kwanza, walitembelea Ikulu ya Rwanda, walipoalikwa na rais Paul Kagame kupeleka Kombe la Afrika Mashariki na Kati, ambalo tangu mwaka 2002 mfadhili wake mkuu na mlezi wake ni Rais Kagame, siku hiyo mabao yake yalitiwa kimiani na Hamisi Kiiza dakika ya pili na Simon Msuva dakika 12.
  Awali, Yanga ilikuwa icheze pia na mabingwa wengine wa zamani wa Kombe la Kagame, APR, lakini kutokana na timu hiyo kukabiliwa na mgogoro hivi sasa uliosababisha kufukuzwa kwa kocha Mholanzi, Ernest Brandy na nafasi yake kupewa kocha mzalendo kwa muda, imeshindwa kucheza na Yanga wanaondoka leo kurejea Dar es Salaam.
  Ikifika Dar es Salaam, Yanga itaendelea na mazoezi kwenye Uwanja wa sekondari ya Loyola kujiandaa na Ligi Kuu ya Bara, inayotarajiwa kuanza Septemba 15.
  Yanga ilikwenda Rwanda na msafara wa watu 42, wakiwemo wachezaji 28, Maofisa watano wa benchi la Ufundi na viongozi wanane.
  Viongozi walio na timu Kigali ni Mwenyekiti, Yussuf Manji, Makamu Mwenyekiti, Clement Sanga na Wajumbe wa Bodi ya Wadhamini Mama Fatma Karume, Francis Kifukwe na Seif Ahmed ‘Magari’ sambamba na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji, Abdallah Bin-Kleb na Salum Rupia.
  Benchi la ufundi ni kocha mkuu; Tom Saintfiet, Kocha Msaidizi Fred Felix Minziro, Kocha wa makipa, Mfaume Athumani, Meneja Hafidh Saleh, Daktari, Sufiani Juma na Mtunza vifaa Mahmoud Omary ‘Mpogolo’, wakati wachezaji ni makipa: Yaw Berko, Ally Mustafa ‘Barthez’ na Said Mohamed. Mabeki Shadrack Nsajigwa, Godfrey Taita, Juma Abdul, Oscar Joshua, Stefano Mwasyika, David Luhende, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondan, Ibrahim Job, Ladisalus Mbogo; viungo Athumani Iddi ‘Chuji’, Juma Seif ‘Kijiko’, Salum Telela, Simon Msuva, Shamte Ally, Omega Seme, Idrisa Rashid, Nizar Khalfan, Haruna Niyonzima, Frank Domayo, Rashid Gumbo, Nurdin Bakari na washambuliaji; Hamis Kiiza ‘Diego’, Jerry Tegete na Didier Kavumbangu.
  Yanga ilitwaa Kombe la Kagame kwa mara ya pili mfululizo wiki mbili zilizopita, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa kuifunga Azam FC mabao 2-0, ambayo yalitiwa kimiani na Hamisi Kiiza ‘Diego Milito’ na Said Bahanuzi ‘Spider Man’.
  Hiyo kwa ujumla ilikuwa mara ya tano mfululizo, Yanga inatwaa Kombe hilo, baada ya awali kuchukua mwaka jana, wakiifunga Simba katika fainali bao 1-0, Uwanja wa Taifa mfungaji Kenneth Asamoah ambaye ametemwa, ingawa siku hiyo Kiiza pia alifunga bao safi, ambalo refa alilikataa.
  Yanga ilichukua kwa mara ya kwanza Kombe hilo, mwaka 1975 ikiifunga tena Simba katika fainali, mabao 2-0 wafungaji Sunday Manara ‘Computer’ na Gibson Sembuli (sasa marehemu) Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
  Ikachukua tena mwaka 1993, Uwanja wa Nakivubo, Kampala, Uganda kwa kuifunga SC Villa mabao 2-1, yaliyotiwa kimiani na Said Nassor Mwamba ‘Kizota’ (sasa marehemu) na Edibily Jonas Lunyamila.
  Ilichukua tena mwaka 1999, ikiifunga tena SC Villa, Uwanja wa Nakivubo, kwa penalti 5-3, kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 120, Yanga ikisawazisha bao kupitia kwa Lunyamila, baada ya Hassan Mubiru kutangulia kuifungia Villa, siku hiyo Manyika Peter akicheza penalti mbili za Waganda.   
  Aidha, kwa kutwaa Kombe hilo chini ya Mbelgiji huyo, Yanga imeendeleza rekodi yake ya kutwaa mataji ya michuano hiyo, chini ya makocha wa kigeni baada ya mwaka 1975 kuchukua chini ya Tambwe Leya aliyekuwa raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kabla ya kuchukua uraia wa Tanzania, (sasa marehemu), 1993 chini ya Nzoyisaba Tauzany aliyekuwa raia wa Burundi kabla ya kuchukua uraia wa Tanzania, mwaka 1999 chini ya Raoul Shungu wa DRC na mwaka jana chini ya Mganda, Sam Timbe.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA WAREJEA LEO BAADA YA KUZOA 'POINTI SITA' RWANDA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top