Mbuyu Twite |
Na Mahmoud Zubeiry
MAMBO matatu yamemfanya beki Mbuyu Twite wa APR ya Rwanda, aachane
na Simba SC na kuamua kujiunga na Yanga SC, BIN ZUBEIRY imebaini
baada ya uchunguzi wa kina uliohusisha vyanzo kutoka Tanzania, Rwanda na Jamhuri
ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Mambo hayo ambayo kwa mjumuisho unaweza kuyaita ‘Ujanja
ujanja wa mjini’ wa viongozi wa klabu hiyo ndio leo, yanaiponza klabu hiyo
kumpoteza aina ya mchezaji ambaye walimuhitaji sana kwenye kikosi chao ili
kujiimarisha.
Mosi; Namna ambavyo ‘walimuenzi’ kiungo Patrick Mutesa
Mafisango (sasa marehemu), pili; desturi ya kuwaacha wachezaji wa kigeni baada
ya kuwasajili, hata kabla hawajaitumikia timu mfano Lino Masombo, Derrick
Walullya na wengineo na tatu hadhi ya klabu yao kwa sasa ukilinganisha Yanga na
Azam FC.
Habari za kiuchunguzi, ambazo BIN ZUBEIRY imezipata zinasema
kwamba Mbuyu alilishwa ‘sumu’ za kutosha ili aichukie Simba, kwanza klabu hiyo
ilivyoutelekeza mwili wa marehemu Mafisango baada ya kifo chake, ambao hakuna
kiongozi mkuu wa klabu hjiyo hata mmoja aliyekwenda kumzika DRC, zaidi ya Mjumbe
mmoja wa Kamati ya Utendaji na mchezaji mmoja.
Pamoja na namna ambavyo Simba hawakujali kabisa mambo
mengine muhimu kuhusu marehemu Mafisango, kama arobaini yake na kadhalika, Wakongo
wameichukulia hiyo kama ni dharaua na ulipotokea mjadala Mbuyu aende wapi, watu
wa Kongo wakamnyooshea kidole kinachoelekeza Jangwani.
Ikumbukwe, Mafisango aliyejiunga na Simba akitokea Azam FC,
iliyomsajili kutoka APR ya Rwanda, alifariki akiwa mchezaji muhimu ndani ya
Simba akiongoza kwa kufunga mabao na mwenye mchango mkubwa kwenye timu.
Simba, hivi karibuni ilimsajili mchezaji Lino Masombo kutoka
DRC, lakini baada ya mwezi mmoja na ushei ikamtema kama ilivyofanya kwa Mganda,
Derrick Walullya msimu uliopita, hilo limetajwa kumsitisha Mbuyu kuangukia Msimbazi
na kuamua kurudisha fedha zote alizochukua kwa Mwenyekiti, Ismail Aden Rage (dola
za kimarekani 30,000 kwa mujibu wa Simba).
Lakini pia, wakati Mbuyu anasaini Simba kuchukua fedha,
alikuwa hajui kwamba katika soka ya Tanzania hivi sasa, klabu ambazo zinachuana
kwa ‘utajiri’ ni Yanga, ambao Mwenyekiti wao Yussuf Manji ni mfanyaiashara
mkubwa na Azam FC ambayo inamilikiwa na mfanyabiashara mwingine, Said Salim
Bakhresa.
Yanga imemsajili Twite, wakati tayari akiwa amekwishaini
Simba SC, baada ya kumrudisha kwenye uraia wake wa asili, Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo (DRC), badala ya Rwanda aliopewa wakati akicheza nchini
humo na kumbadili jina pia.
Kwa kumbadili uraia, Yanga walipata na Hati ya Uhamisho wa
Kimataifa (ITC) ya mchezaji huyo, kutoka Shirikisho la Soka (DRC), na kuwaacha Simba
wakihangaika bila mafanikio kupata ITC ya mchezaji huyo kutoka FERWAFA,
Shirikisho la Soka la Rwanda.
Yanga inamsajili Twite kama mchezaji kutoka St Eloi Lupopo,
klabu ambayo aliichezea kabla ya kutua APR mwaka 2006 kwa pamoja na ndugu yake,
Kabange. Lakini mchezo uliochezwa hapa ni kwamba Twite alikuwa anacheza kwa
mkopoAPR.
Habari zaidi zinasema, Yanga inamsajili pia na pacha wake
Mbutu (pacha wa kuzaliwa kabisa), Kabange, kwa sababu wachezaji hao kawaida yao
kucheza timu moja daima.
Huko nyuma, Yanga iliwahi kuifanyia tena Simba ‘umafia’ kama
huu katika usajili wa wachezaji, Charles Boniface Mkwasa na Yussuf Ismail Bana,
miaka ya 1980.
Simba ilimsaiji beki wa Pamba kama Yussuf Bana, lakini Yanga
wakaingilia kati na kumsajili kwa jina la Yussuf Ismail Bana, Mwenyekiti wa
Chama cha Soka Tanzania (FAT, sasa Shirikisho, TFF), wakati huo Said Hamad El
Maamry akamuidhinisha beki huyo kucheza Yanga.
Simba walijaribu kumuiba kiungo Charles Boniface,
aliyesajiliwa Yanga kutoka Tumbaku ya Morogoro na kumsajili, lakini baadaye
Yanga wakamsajili pia na kumbadili jina, wakimpa Charles Boniface Mkwasa.
Mkwasa alifungiwa na FAT ya El Maamry kabla ya kufunguliwa
baadaye na kuendelea kukipiga Yanga.
Japokuwa kinachozungumzwa kwa sasa ni kwamba, mtoto wa rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ridhiwani Kikwete amewasaidia Yanga
kumbadili njia Mbuyu, lakini uchunguzi wa kina uliofanywa na BIN
ZUBEIRY umegundua mtoto huyo wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete hajahusika
kabisa na usajili wa beki huyo, bali ni Bin Kleb.
Kulingana na uzoefu wa ‘fitina za soka ya bongo’,
inawezekana Simba wanamtaja Ridhiwani, ili ionekanane wamemkosa mchezaji huyo
kwa nguvu za vigogo wa serikali, wakati ‘ubabaishaji’ wao wenyewe.
Swali gumu ambalo bado litaendelea kuwaumiza wana Simba ni
kwamba, akijua kwamba mchezaji huyo wakati anamsajili na Yanga pia walikuwa
wanamfukuzia, kwa nini Rage alimuacha Rwanda, ambako Bin Kleb alibaki pia.
Na hiyo inaumiza zaidi inapokumbukwa kwamba beki wao Kevin
Yondan, alisaini na kujiunga na Yanga, wakati tayari akiwa amekwishasaini
kuendelea kuichezea kla bu hiyo- maana yake vipongozi wa Simba hawajifunzi
kutoka na makosa.
0 comments:
Post a Comment