• HABARI MPYA

  Alhamisi, Agosti 30, 2012

  SIMBA SC WAENDELEA KUIPANGIA MAKOMBORA AZAM FC

  Kikosi cha Simba

  Na Princess Asia
  SIMBA inaendelea kujipanga kwa ajili ya mechi ya Ngao ya Jamii, dhidi ya Azam FC itakayopigwa Septemba 8, mwaka huu Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam na katika kukusanya makali, itakuwa na mechi nyingine ya kimataifa Jumapili ya kujipima nguvu, dhidi ya City Stars ya Nairobi.
  Hiyo ni timu ambayo ilicheza na Simba Agosti 8, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika Simba Day na wenyeji wakachapwa mabao 3-0 na Jumapili watarudiana Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.
  Awali, Simba ilikuwa icheze na Coastal Union Jumapili Uwanja wa Taifa, lakini imeachana na mechi hiyo, kwa kuwa Wagosi hao wa Kaya wataanza kucheza na Yanga Jumamosi.
  Katika hali inayoashiria Kocha Mserbia, Milovan Cirkovick bado hajapata kikosi rasmi cha kwanza, jana alifanya mabadiliko mengine makubwa katika mchezo wa kirafiki dhidi ya JKT Oljoro, kutoka kile kilichocheza na Mathare United ya Kenya Jumapili.
  Katika mchezo huo, ambao Simba ilishinda mabao 2-1, kikosi kilikuwa; Wilbert Mweta, Haruna Shamte/Nassor Maspoud ‘Chollo’, Paul Ngalema/Amir Maftah, Paschal Ochieng, Juma Nyosso, Amri Kiemba/Salim Kinje, Mwinyi Kazimoto, Ramadhani Chombo ‘Redondo’, Mrisho Ngassa, Daniel Akuffo/Abdallah Juma na Kiggi Makassy/Uhuru Suleiman.
  Kikosi hicho kimeibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya wenyeji JKT Oljoro, mshambuliaji kutoka Stella Abidjan ya Ivory Coast, Mghana Daniel Akuffo akiendelea kutunisha akaunti yake ya mabao Msimbazi, akifikisha mawili wakati Mrisho Khalfan Ngassa alifungua rasmi akaunti yake ya mabao jana katika mchezo huo.
  Akuffo aliifungia bao la kwanza Simba SC dakika ya 25, akiunganisha pasi ya Ngassa- hilo likiwa bao lake la pili tangu aanze kuichezea timu hiyo mwezi huu, baada ya awali kufunga kwenye Uwanja huo huo Jumapili dhidi ya Mathare United ya Kenya katika ushindi kama wa leo, 2-1.
  Ngassa alifungua akaunti yake ya mabao Simba SC dakika ya 76 akiunganisha pasi ya Abdallah Juma ‘Dullah Mabao’ na Oljoro ilipata bao la kufutia machozi dakika ya 89 kwa penalti iliyotiwa nyavuni na Markus Mpangala baada ya Paschal Ochieng kumuangusha mchezaji huyo wa timu ya Maafande wa Jeshi la Kujenga Taifa kwenye eneo la hatari.    
  Simba inajiandaa na mechi ya Ngao ya Jamii Septemba 8, mwaka huu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ambayo kihistoria hiyo itakuwa mechi ya tano ya Ngao ya Jamii kuchezwa nchini na ya pili kuishirikisha timu nje ya wapinzani wa jadi wa soka ya Tanzania, Simba na Yanga.
  Mtibwa ilicheza na Yanga mwaka 2009, baada ya Simba kugoma na ikashinda mabao 2-1 na kutwaa Ngao, wakati kabla ya hapo, mwaka 2001, Ligi Kuu ya Tanzania ikiwa bado inadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia ya Safari Lager, ilichezwa mechi ya kwanza ya Ngao kihistoria.
  Katika mechi hiyo, Yanga ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Simba na mwaka juzi Yanga iliifunga tena Simba kwa penali 3-1 kufuatia sare ya 0-0 na mwaka jana, Simba ilitwaa Ngao ya kwanza katika historia yake, kwa kuifunga Yanga mabao 2-0. 

  MABINGWA WA MECHI ZA NGAO YA JAMII:
  Mwaka          Mshindi        Matokeo 
  2001             Yanga           2-1 Simba
  2010             Yanga           0-0 Simba (3-1penalti)
  2011             Simba           2-0 Yanga
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA SC WAENDELEA KUIPANGIA MAKOMBORA AZAM FC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top