• HABARI MPYA

    Sunday, April 01, 2012

    JOHN BOCCO AFANYIE KAZI MAPUNGUFU YAKE, ASISUSE TIMU YA TAIFA

    Hapa Bocco alibaki yeye na kipa, baada ya kupewa pasi nzuri akiwa kwenye nafasi nzuri katika mechi dhidi ya Msumbiji, lakini akakosa bao.
    HABARI kubwa katika magazeti ya jana ilikuwa ni tamko la mshambuliaji chipukizi Tanzania, John Raphael Bocco kujiuzulu timu ya taifa, Taifa Stars kwa sababu ya kukwepa kuzomewa na mashabiki.
    Bocco ambaye anafahamika kwa jina la utani Adebayor, amekerwa mno na kitendo cha mashabiki kumzomea na kumsakama kwamba hafungi mabao na ndio maana kachukua uamuzi huo.
    Huyu ni kijana mwenye umri wa miaka 23, akiwa amezaliwa Agosti 5, mwaka 1989 kwa mujibu wa wasifu wake.
    Kijana ambaye unaweza kusema anainukia vizuri katika soka ya Tanzania, ambaye miaka michache ijayo baada ya kukomaa zaidi kisoka anaweza kuwa tegemeo la  nchi.
    Bocco ambaye amewahi kufanya majaribio Israel na wakala wake Yussuf Bakhresa akadanganya wananchi eti amefuzu kama alivyofanya kwa Mrisho Ngassa, amekwishawasilisha barua Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) juu ya uamuzi wake huo.
    Inasikitisha. Tena inasikitisha sana kwa kijana mdogo kama Bocco, ambaye badala ya kutumia vizuri fursa aliyonayo kuinua kipaji chake anachukua maamuzi ya kitoto.
    Mashabiki wanamzomea anakosa mabao, je wanamsingizia? Hapana, anakosa kweli. Kwa nini wanamzomea, wanamzomea kwa sababu anakosa mabao. Wanataka nini, wanataka afunge.
    Basi, hiyo ndio kesi. Kitendo cha Bocco kujiuzulu amewadhihirishia wapenzi wa soka nchini, hasa wale wambao wamekuwa wakimzomea kwamba hana msaada kwa taifa, kitu ambacho si kweli.
    Bocco anahitaji muda aendelee kukomaa kisoka, ili aanze kukonga nyoyo za mashabiki kwa kiwango wanachotaka wao.
    Hawezi kuwa amekomaa kwa kucheza mashindano ya CECAFA, Challenge na mechi za Ligi Kuu ya Bara hata kama anaongoza kwa mabao.
    Anaongoza kwa mabao katika ligi ambayo inanuka rushwa, timu zote zilizo kwenye mbio za ubingwa zinatuhumiwa kucheza mchezo mchafu wa kupanga matokeo.
    Bocco anafunga mabao mawili dhidi ya Yanga, wakati mtaani kumezagaa tuhuma baadhi ya wachezaji wa Yanga walihujumu timu.
    Wakati huo huo, akiwa kwenye timu ya taifa anabaki yeye na kipa zaidi ya mara tatu anakosa mabao.
    Wakati timu ya taifa ya Bara inachukua Kombe la Challenge  mwaka juzi, Bocco akiwemo kikosini, alishindwa kufunga mabao hadi ikabidi Nurdin  Bakari awe anatumiwa kama mshambuliaji na ndio akawa anafunga hadi timu ikaingia Robo Fainali. 
    Kutoka hapo, mikwaju ya penalti iliyokuwa inapigwa Nsajigwa Shadrack ilitubeba hadi tunachukua Kombe. Mwaka jana alikuwepo kikosini Bara na timu haikufika popote.
    Lakini bado anataka mashabiki wasiseme. Hili ni tatizo la wachezaji wengi wa Tanzania kujiona wanajua kuliko uwezo wao halisi. Bocco bado. Tena bado sana.
    Naomba sana Mungu, Azam FC itwae tiketi ya kuiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya Afrika na mshambuliaji wao kiongozi awe Bocco, waanze kucheza mechi dhidi ya timu ngumu kama TP Mazembe, ES Setif, Zamalek, Enyimba, Sfaxien, Waydad na nyinginezo, kwani naamini hizo ndizo zitamkomza mchezaji huyo.
    Nakubaliana na hoja ya mashabiki wengi wa soka nchini, kwamba sisi waandishi wa habari tunawaharibu wachezaji kwa kuwasifia sana, wakati uwezo wao mdogo.
    Lakini wakati mwingine tunalazimika kuwatukuza kwa sababu hao ndio wetu. Messi atabakia kuwa wa Argentina tu na Ronaldo wa Ureno- Tanzania wetu ni akina Tegete, Mgosi, Samatta, Bocco, Kisambale na wengineo.
    Lakini inasikitisha wachezaji wetu miaka mingi sasa wameshindwa kujitambua, zaidi wanajiona tayari wamefika kiwango cha juu na hii kwa sababu ya kukosa mitazamo ya mbali.
    Bocco hakupaswa kuumia kwa kuzomewa na mashabiki pale Uwanja wa Taifa, alitakiwa kuumia kwa kushindwa majaribio Israel.
    Amepoteza utajiri. Amepoteza fursa nzuri ya kuwa mchezaji mkubwa duniani.
    Lakini kwa sababu kabla hajapanda ndege kuanza safari ya kwenda Israel alikwishafeli majaribio kutokana na kutojiamini kwake, haikumuumiza na ndiyo maana aliporudi nchini hatukuona tofuti.
    Amekuwa na bahati, kwanza ya kukutana na makocha wazuri na pili wanomkubali ambao wanakuwa na matumaini naye, hivyo wanampa nafasi sana kuanzia klabu yake hadi timu ya taifa.
    Labda hilo linampa jeuri, anajiona anajua sana kiasi cha kufikia kukataa kuzomewa anapowanyima raha mashabiki.
    Shabiki anataka tiketi yake kwenda uwanjani kushangilia, anafika huko anakutana na mtu ambaye ni ‘kipofu’ kila anapokaribia lango, je afanye nini.
    Bocco anatakiwa kujua hao mashabiki ndio wenye mpira wao dunia nzima. Soka ipo kwa ajili yao na wachezaji wapo kwa ajili yao na ndiyo maana hata yeye amekwishashangiliwa sana na mashabiki hao hao.
    Alipowafunga bao Yanga alielekea upande wa jukwaa kushangilia na mashabiki, ambao ndio hao hao akiwa na jezi ya timu ya taifa na anakosa mabao wanamzomea.
    Hapa nataka nikumbushe kitu kimoja, ligi yetu imegubikwa na skendo na za rushwa na ndio maana utaona Yanga japokuwa Kenneth Asamoah anaongoza kwa mabao, lakini kwa wanamuona hafai na wanataka kumtema.
    Boniphace Ngairah Ambani alikuwa mfungaji bora Ligi akiwa na jezi ya Yanga, lakini hawakuona tabu kumtema- kwa sababu wenyewe wenye timu zao wanajua kwa nini anafunga.
    Hivyo Bocco pia anatakiwa kutojivunia mafanikio yake Ligi Kuu na kujiona yeye sasa ndiye Ronaldo wetu, hapana- anatakiwa kututhibitishia zaidi kwa kutufungia mabao akiwa na jezi zenye rangi ya bendera ya nchi iliyopata Uhuru wake Desemba 9, mwaka 1961.
    Anatakiwa kuondoa dhana kwamba mashabiki hawampendi na wanamsakama, hapana ajue tu kwamba mashabiki wa soka Tanzania wana hasira na timu yao hata kabla yeye hajazaliwa.
    Wana kiu ya mafanikio hata kabla Azam FC haijafikiriwa kama itakuja katika soka ya Tanzania.
    Bocco bado sana- kwa maana zote hajakomaa kisoka wala kifikra na mbaya zaidi anataka kuingia kwenye kundi waliokata tamaa, au kuridhika na soka la bongo.
    Na kwa uamuzi wake wa kujiuzulu timu ya taifa anaweza kuwa amejiweka katika wakati mgumu mbele ya mashabiki hao hao- kwani inajengeka picha ya vita baina yake na wao.
    Mimi nasema mashabiki kuzomea wako sahihi, ikiwa hawaipati furaha wanayoitarajia na ndiyo maana siku hizi wamebaini njia mpya ya kukata kiu yao kwa kushangilia timu za wageni.
    Hii ni changamoto kwa wachezaji wetu ambayo inabidi wapambane nayo.
    Kukimbia changamoto ni udhaifu na Bocco anatakiwa kushauriwa mara mbili, tena na watu ambao wenye uwezo wa kujenga hoja za ushawishi ili atengue uamuzi wake wa kujiuzulu timu ya taifa.
    Siku zote mchezaji ndiye anaihitaji timu ya taifa, kwanza mbali na uzalendo wake tu, lakini pia kwa heshima yake.
    Leo timu ya taifa ina matatizo, haina matokeo mazuri, lakini sababu ni ndogo tu, kubwa uongozi mbovu wa TFF, Bocco anaisusa, lakini baadaye ikija kuwa vizuri, mchezaji huyo ataitamani tu na kujutia uamuzi wake.
    Hata wachezaji wakubwa duniani kama Ronaldo, Messi, Drogba nao kuna wakati wanaingia kwenye makucha ya mashabiki.
    Messi ni mchezaji mkubwa, lakini kwao hana heshima kwa sababu hajafanya chochote katika timu ya taifa na tulimuona kwenye fainali za Kombe la Dunia Afrika Kusini akishindwa kuisaidia Argentina kufika mbali.
    Drogba, Yaya Toure, Gervinho walishindwa kuisaidia Ivory Coast kutwaa Kombe la Mataifa ya Afrika, je mashabiki wawafurahie kwa kipi?
    Messi ni mwanasoka bora wa dunia mara tatu, lakini akikutana na Ronaldinho anaweza kuwa mnyonge kwa jambo dogo tu- ni iwapo Gaucho ataamua kumsimulia fainali za Kombe la Dunia 2002 zilivyokuwa.
    Mwisho wa hadithi hiyo ni kwamba Brazil ilikuwa bingwa na Dinho aling’ara sana tu- katika fainali zilizofanyika wakati Bocco akiwa ana umri wa miaka 13.
    Je, Messi baada ya fainali za Kombe la Dunia za 2006 na 2010 anaweza kusema ana nini cha kujivunia?
    Hivyo basi, hata Bocco asione kuongoza kwake kwa mabao katika Ligi Kuu ya Bara basi ndio amemaliza hapana.
    Bocco alichotakiwa kufanya ni kufanyia kazi mapungufu yake, ili siku moja aje kuwasuta mashabiki.
    Na hii si kwa Bocco tu, bali kwa wachezaji wengine wote wenye mtazamo kama wake, wanatakiwa kufanyia kazi mapungufu yao na si kuleta majivuno wakati ‘hawana lolote’.
    Soka ipo kwa ajili ya mashabiki na ndio maana kuna yale majukwaa- na wachezaji wote wanatakiwa kujua, mabosi wao wakubwa ni hao mashabiki kwa sababu ndio wateja wao na kama mteja ni mfalme, basi Bocco ajue amechemka kwa uamuzi wake.
    Maswali matatu ya msingi Bocco anatakiwa kujizuliza. Kwa nini anazomewa? (anakosa mabao sana), je, anasingiziwa? (hapana), sasa kwa nini asuse timu ya taifa? Alamsiki.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: JOHN BOCCO AFANYIE KAZI MAPUNGUFU YAKE, ASISUSE TIMU YA TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top