• HABARI MPYA

    Tuesday, February 14, 2012

    PUMZIKA KWA AMANI WHITNEY






    Na Abdul Mohammed
    KIFO cha msanii Whitney Houston wa Marekani ni pigo kubwa katika sanaa ya muziki
    duniani.
    Hakuna mpenzi wa muziki hususan wa miaka ya 1980 na 1990 aliyekuwa akifuatilia
    wanamuziki wa majuu halafu akawa hamjui Whitney Houston.
    Sauti yake nyororo inayopaa na kushuka katika mpango mzuri ni kati ya mambo
    yaliyotosha kuwakosha mashabiki wa muziki duniani kote.
    Nje ya hilo kifo hicho kinabaki kuwa somo kubwa kwa wasanii wetu na jamii ya watanzania na dunia kwa ujumla.
    Hii ni kutokana na ukweli kwamba mazingira ya kifo chake kilichotokea akiwa
    hotelini bado yametawaliwa na utata.
    Utata ambao unatosha kuhitimisha hoja kuu ya msingi kwamba maisha ya msanii huyo
    yalianza kutetereka na kuwa katika hatihati kutokana na utumiaji wa dawa za
    kulevya maarufu unga.
    Kwa maana nyingine Whitney Hoston (48) alikuwa Teja kama
    ambavyo wengi wetu tumezowea kuwaita watumaiji wa ulevi wa aina hiyo.
    Kwa mashabiki wa Whitney gumzo katika maisha yake ilikuwa ni katika mambo matatu.
    Kwanza ni maisha yake katika muziki na nyimbo kadhaa alizoimba na kutamba pamoja na filamu maarufu ya Bodyguard.
    Pili ni maisha yake binafsi na mambo anayofanya ikiwamo uhusiano wake na aliyekuwa
    mumewe Boby Brown.
    Na tatu ni namna ambavyo maisha yake yalitawaliwa na utumiaji wa dawa za kulevya
    yaani jinsi Whitney alivyokuwa Teja la kutupwa.
    Katika muziki pamoja na mahusiano yake ya kimapenzi na Boby Brown nimekichagua kibao
    cha ‘We Have Something in Common’
    Kibao walichoimba baada tu ya ndoa na kufanikiwa kupata mtoto wao wa kike Kristina.
    Katika kibao hicho Whitney anaimba akitamba jinsi anavyompenda Bobby huku akisisitiza
    kwamba atakuwa imara pindi mumewe atakapokuwa dhaifu
    Pengine ni sahihi kuyakumbuka baadhi ya mashairi ya wimbo huo kama
    ifiatavyo:

    I’m the type of girl who
    understand my man (Mimi ni aina ya msichana anayemfahamu mwanaume wake)
    I’ll be strong when he’s
    weak, I will hold his hand (Nitakuwa imara akiwa dhaifu, nitashikamana naye)
    I’ll stand by your side till
    the very end
    (Nitakuwa naye sambamba hadi mwisho).
    Katika hili Whitney alijitahidi kushikama na kila alichokiimba, alimuelewa Bobby na
    udhaifu wake kwani hata alipokamatwa kwa makosa kadha wa kadha ikiwamo kukutwa
    na bangi bado alikuwa akimtetea.
    Inakumbukwa siku aliyopigwa na Bobby na Bobby kutiwa ndani lakini siku apotolewa alikuwa wa kwanza kumrukia na kumkumbatia.
    Alimtetea kwamba pamoja na udhaifu wote unaozungumzwa lakini kwake Bobby ni kila kitu na
    kwamba ataendelea kushikamana naye.
    Alidhihirisha nia ya kuwa sambamba na Bobby hadi mwisho lakini hatimaye yalimshinda.
    Dalili za kumshinda zilianza kuonekana mapema hususan pale naye alipojiingiza katika
    utumiaji dawa za kulevya.
    Tatizo hili lilianza kumkwaza mapema kwani uwezo na umahiri wake katika kuimba
    taratibu ulianza kufifia.
    Alifurukuta na kuibuka upya akidai kwamba ameacha utumiaji wa unga baada ya kukutana na
    washauri nasaha lakini mabadiliko hayo yalikuwa ya muda.
    Kuna wakati alishindwa kuimba vizuri nyimbo zake za zamani zilizompa umaarufu.
    Kifupi ni kwamba unga na dawa za kulevya vilimharibu, Whitney kwani hakuwa yule
    aliyezoeleka na kuteka hisia za mashabiki duniani kote.
    Wakati hali ikianza kubadilika Whitney alitangaza kutengena na Bobby, taarifa ambazo
    hapana shaka ziliwapa matumaini wapenzi wake.
    Matumaini yalikuwa kwamba huenda walau angerudi katika ubora wake baada ya kuachana na
    huyo mumewe ambaye inadaiwa ndiye aliyemfanya awe mtumiaji wa dawa za kulevya.
    Matumaini zaidi yaliongezeka baada ya habari kwamba alikuwa na mpenzi mpya Ray J ambaye
    alichukua nafasi ya Bobby.
    Zaidi ya hilo mwaka 2002 Whitney aliwahi kukiri wakati akiaandamwa na kashfa ya utumiaji dawa na Bobby kudaiwa kuwa ndiye kiini ambako alisema shetani na adui yake ni yeye
    mwenyewe na si mtu mwingine.
    Alikri kutumia dawa za kulevya aina ya cocaine pamoja na kuvuta bangi jambo ambalo
    lilitoa picha kwamba anajua nini anakifanya na nini anatakiwa kukiepuka.
    Hata hivyo baada ya hali kutulia mambo yalibadilika, Whitney alirudi katika matatizo
    na hadi kifo kimemkuta moja kwa moja kifo hicho kinahusishwa na ulevi.
    Na ingawa hadi sasa taarifa rasmi za nini hasa kimesababisha kifo chake
    hazijatolewa lakini suala la kwamba unga umechangia kifo cha msanii huyo
    haliwezi kuwekwa pembeni.
    Na kwa kuwa tayari ziko habari kwamba alirudi katika utumiaji unga ni wazi kwamba
    kifo cha msanii huyo kimetokana na unga huo huo kwamba alikufa akiwa Teja.
    Si Whitney pekee aliyefariki na kifo chake kuhusishwa na utumiaji wa dawa za
    kulevya, wako wasanii kadhaa waliopitia katika matatizo hay ohayo.
    Na hapa nianze kwa kumtaja Brenda Fasie wa Afrika Kusini ambaye akiwa nchini Tanzania aliwahi kuulizwa kama anatumia dawa za kulevya au la.
    Badala ya kujibu swali hili akawa mkali kwa mwandishi na kusema kwamba hawezi kujibu
    swali hilo.
    Brenda alikufa mwaka 2004 akiwa katika makazi yake ya Buccleuch wakati huo akiwa na
    miaka 39.
    Awali ilielezwa kwamba alikufa kwa ugonjwa wa pumu lakini baadaye uchunguzi wa madaktari
    ulibainisha kwamba dozi kubwa ya cocaine aliyobugia ilichangia kifo chake.
    Msanii mwingine ni Amy Winehouse wa Uingereza, huyu naye aliingia katika matatizo ya
    utumiaji dawa za kulevya.
    Na kifo chake kilitokea katika mazingira hayo hayo yanayohusisha ulevi.
    Akiwa amekufa walinzi wake waliamini amelala kutokana na kawaida yake ya kulewa unga
    na kuchelewa kuamka.
    Hata hivyo baadaye ilibainika kwamba alikuwa amekufa na polisi kukuta chupa tatu za
    pombe kali aina ya Vodka, chupa mbili zikiwa kubwa na moja ndogo.
    Hao ni wasanii wa nje, je tumeanza kujiangalia na sisi wenyewe. Wasanii wetu wa Tanzania hawana tatizo hili.
    Katika muziki wa dansi na sanaa nyinginezo hakuna kabisa mateja, lakini tusiishie kwa
    wasanii tu, je ni vipi kwa watanzania wenzetu wengine ambao tayari ni mateja?
    0754310170
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: PUMZIKA KWA AMANI WHITNEY Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top