• HABARI MPYA

  Tuesday, May 16, 2017

  YANGA NAO KUFUNGA NDOA NA SPORTPESA KESHO

  Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
  KLABU ya Yanga kesho inatarajiwa kusaini mkataba wa udhamini na Kampuni ya SportPesa, ambayo tayari imesaini na mahasimu wao, Simba.
  Kwa mara nyingine, vigogo wa soka Tanzania na mahasimu wa jadi, Simba na Yanga wanatarajiwa kuwa chini ya udhamini mmoja, baada ya awali wote kudhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kati ya mwaka 2007 na 2016.
  TBL iliachana na Simba na Yanga na kwa ujumla ilijitoa kwenye kudhamini soka, hadi timu ya taifa, Taifa Stars kufuatia mabadiliko ya umiliki wa kampuni hiyo.
  Na miezi michache baada ya kupoteza udhamini wa TBL kupitia bia ya Kilimanjaro Premium Lager, hatimaye Simba na Yanga zitakuwa zinavaa jezi zenye kufanana tena maandishi kifuani, SportPesa.
  Mkurugezi wa Utawala wa SportPesa, Tarimba Abbas (kulia) kesho atasaini na Yanga

  Wakati haijulikani Yanga itavuna kiasi gani katika udhamini wa miaka mingapi, Simba SC imevuna Sh. Bilioni 4.96 kwa miaka mitano.
  Mkurugezi wa Utawala wa SportPesa, Tarimba Abbas alisema wiki iliyopita wakati wa kusaini mkataba huo kwamba mwaka wa kwanza watatoa Sh. Milioni 888 na miaka itakayofuata wataongeza asilimia 5 kabla ya miaka miwili ya mwisho kutatoa kiasi cha Sh. Bilioni 1 na kwamba fedha hizo zitatolewa kwa awamu nne kwa mwaka.
  Alisema kutakuwa pia na motisha klabu hiyo ikishinda mataji, mfano kwa ubingwa wa Ligi Kuu watapewa Sh. Milioni 100, Ligi ya Mabingwa Afrika Sh. Milioni. 250 na Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati au Kombe la Kagame watapewa zawadi pia.
  Na Tarimba akasema kwamba Simba watapaswa kuyathibitisha matumizi ya fedha hizo kwamba yalifanyika kwa maendeleo ya soka.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA NAO KUFUNGA NDOA NA SPORTPESA KESHO Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top