• HABARI MPYA

  Friday, May 12, 2017

  YANGA NA MBEYA CITY YARUDISHWA SAA 10:30 JIONI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MCHEZO wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kati ya wenyeji, Yanga SC na Mbeya City ya Mbeya utafanyika Saa 10:30 jioni kesho badala ya Saa 12:00 jioni kama ilivyotangazwa awali.
  Taarifa ya Yanga SC jioni ya leo imesema kwamba mchezo huo umerudishwa Saa 10:30 jioni baada ya mambo ya ratiba ya matumizi ya Uwanja wa Taifa siku hiyo kurekebishwa kidogo.
  “Maamuzi haya yamezingatia matakwa na masilahi ya wadau wa soka nchini ambao wana kiu na hamu ya kuutazama mchezo huo, lakini pia wakiwa ni sehemu ya wadau wa mchezo wa riadha itakayofanyika uwanja wa taifa jumamosi hiyo hiyo,”imesema taarifa ya Yanga leo.
  Yanga itaingia kwenye mchezo huo ikitoka kurejea kileleni mwa Ligi Kuu baada ya ushindi wa mabao 2-1 Jumanne dhidi ya Kagera Sugar ya Bukoba Uwanja wa Taifa.
  Na kwa ushindi huo, mabingwa hao watetezi wanafikisha pointi 62, sawa na Simba SC, lakini timu ya Jangwani inapanda juu kwa wastani mzuri wa mabao na pia wana mchezo mmoja mkononi. 
  Usukani wa Ligi Kuu unaweza kurejea mikononi mwa Simba SC iwapo wataifunga Stand United jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Wekundu hao wa Msimbazi watacheza mechi yao ya 29 leo watakapowakaribisha Stand United, huku wakihitaji lazima kushinda ili kuweka hai matumaini ya ubingwa.
  Matokeo yoyote tofauti na ushindi, wazi yatawatoa Simba kwenye mbio za ubingwa na haswa kama Yanga nao watashinda kesho dhidi ya Mbeya City Uwanja wa Taifa.
  Mechi nyingine ya Ligi Kuu leo ni kati ya wenyeji, Azam FC na Toto Africans Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, wakati kesho mbali na Yanga kumenyana na Mbeya City, Mtibwa Sugar wataakuwa wenyeji wa Mwadui FC Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro.
  Mechi nyingine za kesho ni kati ya JKT Ruvu na Maji Maji ya Songea Uwanja wa Maji Maji, 
  Tanzania Prisons na Ndanda Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya na Jumapili African Lyon itamenyana na Ruvu Shooting.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA NA MBEYA CITY YARUDISHWA SAA 10:30 JIONI Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top