• HABARI MPYA

    Friday, May 19, 2017

    OMOG: SIMBA USHINDI TU KESHO, MAMBO MENGINE BAADAYE

    Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
    KOCHA Mcameroon wa Simba SC, Joseph Marius Omog amesema anahitaji ushindi katika mchezo wa kesho dhidi ya Mwadui FC ili kuamsha morali kuelekea fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), au Azam Sports Federation Cup dhidi ya Mbao FC.
    Simba SC watakuwa wenyeji wa Mwadui FC kesho Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kabla ya Mei 27 kwenda kumenyana na Mbao FC katika fainali ya ASFC Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.
    Na ikionekana kama haina nafasi tena ya kutwaa ubingwa mbele ya Yanga SC, kocha Omog amesema hawezi kuupuzia mchezo huo, anataka ushindi.
    Joseph Omog anahitaji ushindi katika kesho dhidi ya Mwadui FC ili kuamsha morali kuelekea mechi na Mbao FC

    “Nahitaji kushinda katika mchezo huo, kwani kushinda mechi hiyo ndiyo mwanzo wa maandalizi ya mchezo unaofuata dhidi ya Mbao,”amesema Omog akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online leo Dar es Salaam.
    Omog amesema wachezaji wake wote wapo fiti kuelekea mchezo huo na wamepania kushinda ili kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kujiamini kabla ya kukutana na Mbao FC katika Fainali ya Kombe.
    Pazia la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara linafungwa kesho kwa michezo saba kuchezwa viwanja tofauti – na mbali na Simba na Mwadui, mabingwa watetezi, Yanga watakuwa wageni wa Mbao FC Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
    Mechi nyingine ni kati ya Azam na Kagera Sugar Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, Maji Maji na Mbeya City Uwanja wa Maji Maji, Songea, Stand United na Ruvu Shooting Uwanja wa Kambarage, Shinyanga, Mtibwa Sugar na Toto Africans Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro, Tanzania Prisons na African Lyon Uwanja wa Sokoine, Mbeya na Ndanda FC na JKT Ruvu Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.
    Yanga inaongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 68 za mechi 29, ikifuatiwa na Simba yenye pointi 65 za mechi 29 pia.
    Lakini kutokana na mpango wao wa kukata rufaa FIFA kutaka warudishiwe pointi tatu za Kagera Sugar, Simba wanaamini wakishinda kesho na Yanga wakafungwa na Mbao, wanaweza kutimiza ndoto za ubingwa.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: OMOG: SIMBA USHINDI TU KESHO, MAMBO MENGINE BAADAYE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top