• HABARI MPYA

    Monday, May 15, 2017

    HANS POPPE AREJEA SIMBA SIKU MOJA TU BAADA YA KUJIUZULU

    Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
    MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe amesema kwamba alijitoa kwenye uongozi klabu hiyo kuepuka kuwa sehemu ya watu wasio waungwana, lakini sasa mambo yamewekwa sawa amerudi.
    Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online leo, Hans Poppe amesema kwamba jana walikutana na Rais wa Simba, Evans Elieza Aveva katika kikao pamoja na Wajumbe wengine hadi Saa tisa usiku na kufikia mwafaka.
    “Jana tumekutana mpaka tisa usiku tumeyamaliza vizuri tusonge mbele” amesema Poppe, ambaye mapema jana aliualalamikia uongozi wa Simba chini ya Rais wake, Aveva umemfanyia mambo yasiyo ya kiungwana, mwanachama Mohammed ‘Mo’ Dewji. 
    Hans Poppe amerejea madarakani Simba SC siku moja tu baada ya kujiuzulu 

    Hans Poppe aliandika barua ya kujiuzulu Ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba na maana yake kujivua pia na uongozi wa Kamati ya Usajili na ya ujenzi wa Bunju Complex baada ya kuchukizwa na kutohusishwa katika mkataba wa udhamini wa kampuni ya SportPesa.
    “Siyo kushirikishwa mimi tu, bali Wajumbe wengine wa Kamati ya Utendaji pia, lakini kubwa zaidi tuna makubaliano na Mo (Dewji) kuwa tukitaka kuingia mkataba na yeyote Yule, hakatai lakini tumshirikishe, sasa tunasaini mkataba kwa kumzunguka ni kukosa uungwana na siwezi kuwa sehemu ya hilo,”alisema.
    Poppe amesema kwamba alijaribu sana kutaka kukutana na viongozi wa Simba kujadili nao suala hilo, lakini walikuwa wanamkwepa ndiyo maana ameamua kujiuzulu; “Hatujakaa, kila nikiwaambia tulijadili wanaingilia huku wanatokea kule,”.
    Dewji anayetaka kununua hisa Simba, amesikitishwa na uongozi wa klabu hiyo kwa kuingia mkataba wa udhamini na kampuni ya SportPesa bila kumshirikisha.
    Na habari ambazo hazijathibitishwa na upande wowote, zinasema Mo Dewji, Mbunge wa zamani wa Singida Mjini ameuandikia barua uongozi wa klabu hiyo chini ya Rais wake, Evans Aveva kudai alipwe fedha zake, Sh Bilioni 1.4 alizokuwa anaikopesha Simba kwa kulipa mishahara ya wachezaji na benchi la Ufundi, Sh Milioni 80 kila mwezi.
    Imedaiwa Mo Dewji alikuwa anatoa fedha hizo kwa makubaliano zitalipwa wakati mpango wake wa kununua hisa za klabu utakapokamilika. Mo alikubaliana na uongozi wa Simba kununua asilimia 51 ya hisa kwa Sh. Bilioni 20 mara baada ya mchakato wa mabadiliko ya Katiba utakapokamilika.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HANS POPPE AREJEA SIMBA SIKU MOJA TU BAADA YA KUJIUZULU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top