• HABARI MPYA

    Wednesday, November 09, 2016

    KWA HERI PLUIJM; COACHES ARE HIRED TO BE FIRED HATA BILA YA SABABU

    WAKATI Franciscus Johannes ‘Hans’ van der Pluijm anakuja nchini kwa mara ya kwanza mwaka 2014 kufundisha Yanga SC, nilizama kutafuta wasifu wake.
    Kwa mujibu wa vyombo mbalimbali vya Habari nchini Ghana, historia ya Pluijm ‘imepambwa’ na kufukuzwa fukuzwa.
    Pluijm aliyezaliwa Januari 3 mwaka 1949, alianzia kwenye kucheza soka akiwa kipa kwao nchini Uholanzi kabla ya kuwa kocha.
    Enzi zake aliidakia kwa miaka 28 klabu ya FC Den Bosch akicheza mechi 338 ndani ya misimu 18 na alipostaafu baada ya kuumia goti akawa kocha wa timu hiyo.
    Alianza vyema ukocha akiiwezesha FC Den Bosch kutwaa ubingwa wa Daraja la Kwanza na kupanda Ligi Kuu na ndiye aliyempa nafasi ya kwanza mshambuliaji Ruud van Nistelrooy akiwa kinda wa miaka 17 tu kucheza kikosi cha kwanza cha timu hiyo.
    Aprili mwaka 1995, alisaini Mkataba wa miaka miwili na SBV Excelsior kabla ya kutimuliwa Januari 1997 na nafasi yake ikachukuliwa na Msaidizi wake, John Metgod. 
    Hiyo ilifuatia timu hiyo ya Rotterdam kushinda mechi mbili tu na sare tatu katika mechi 17 za msimu mzima.
    Baadaye akahamia Afrika mwaka 1999, alipokwenda kufundisha Ashanti Gold SC ya Ghana, akianza na Mkataba wa mwaka mmoja. 
    Ajax ya Uholanzi ikanunua hisa katika klabu hiyo Ijumaa ya Juni 18, mwaka 1999 asilimia 51 naye akatupiwa virago na kuhamia Saint-George SA ya Ethiopia kabla ya mwaka 2010 kujiunga na B-Juniors Feyenoord ya Ghana, ambayo ni tawi la timu hiyo ya Rotterdam.
    Mwaka 2012 alijiunga na Berekum Chelsea ambako pia alifukuzwa mwaka 2013 na kuhamia Medeama ya Ghana pia ambako nako alifukuzwa baada ya mechi saba tu, kufuatia matokeo mabaya mwanzo mwa msimu, akivuna pointi nane kati ya 21.
    Hivyo alikuja Yanga akiwa ametoka kufukuzwa SBV Excelsior ya kwao, Ashanti Gold SC, Berekum Chelsea na Medeama SC zote za Ghana.
    Historia inaonyesha ni timu mbili tu Pluijm hakufukuzwa kabla ya kuja Yanga, Saint-George ya Ethiopia na B-Juniors Feyenoord ya Ghana.
    Kwa wasifu huu, nakumbuka niliandika makala za kuwastaajabu Yanga kumchukua kocha kama huyu tena wakimuacha mwalimu mzuri Mholanzi mwingine, Ernie Brandts.
    Lakini wakati leo Pluijm anaweza akawa anaiongoza Yanga kwa mara ya mwisho – mimi niliyewastaajabu kuamuajiri, leo nawastaajabu tena kuachana naye.
    Awali niliwastaajabu kumchukua kocha aliyefukuzwa mara nyingi katika historia yake, lakini sasa nawastaajabu wanaachana na kocha aliyewapa mafanikio.
    Ni Yanga waliompa mkataba mpya Pluijm Julai tu mwaka huu baada ya kuridhishwa na kazi yake nzuri ya msimu uliopia akiipa timu mataji yote matatu ya nyumbani, kumfunga mtani Simba mechi zote na kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho kwa mara ya kwanza tangu 1998.
    Na zaidi katika hatua ya makundi mwaka huu, Yanga imeweka rekodi ya kushinda mechi, wakati mwaka 1998 ilifungwa na kutoa sare tu nyumbani na ugenini.
    Chini ya Pluijm kwa mara ya kwanza Yanga imezifunga timu za Kaskazini mwa Afrika (Al Ahly ya Misri na MO Bejaia ya Algeria zote 1-0) jambo ambalo timu haikuweza kabla tangu ina ‘Kompyuta’ ya mpira, Sunday Manara miaka 1970, baba wa Msemaji wa Simba, Hajji.
    Hivyo ndivyo vitu ambavyo wenzetu Wazungu na nchi nyingine zilizoendelea wanaangalia – rekodi kabla ya kufikia maamuzi. 
    Na zaidi kisoka Yanga imeimarika mno na sasa imekuwa timu ya ushindani nje na ndani. Chini ya Pluijm tumeishuhudia Yanga ngumu kuifunga. Tumeishuhudia Yanga inayoshinda hadi ugenini tena dhidi ya timu ngumu kama APR.
    Zaidi Yanga ya sasa imekuwa ikicheza soka safi ya pasi nyingi za kuburudisha. Sasa Yanga wanamuondoa Pluijm kwa sababu zipi?
    Lakini Yanga kama klabu wana uhuru wa kuamua mambo yao – kama walivyoamua kumtoa Brandts na kumuweka Pluijm na sasa wako huru kuamua vinginevyo.
    Tutamkumbuka Pluijm, kocha aliyebadili mfumo wa uchezaji wa Yanga, kutoka ‘butua butua’ na kukimbiza kukimbiza hadi pasi nyingi za kuburudisha zilizozima utemi wa SImba kwa timu hiyo ya Jangwani.
    Tutamkumbuka Pluijm, kocha aliyekuwa anawapa ushirikiano Waandishi wa Habari wa rika na matabaka yote kila walipomuhitaji. 
    Tutamkumbuka Pluijm, aliyejenga nidhamu ya uwajibikaji ndani ya Yanga na kuwafanya wachezaji wajitambue, hivyo kukuza viwango vyao. 
    Tutamkumbuka Pluijm kwa maisha yake ya ndani nan je ya Uwanja kama mtu wa watu. Sasa mimi na Watanzania wengine tunaanza kupata picha kwamba hata alikofukuzwa kabla ya kuja Yanga inawezekana ilikuwa bila sababu za kitaalamu.
    Yote kwa yote, Pluijm amejijengea heshima kubwa Tanzania. Kwa heri Pluijm; ewe ni uliye bora, lakini; Coaches are hired to be fired hata kama hakuna sababu za msingi. 
    Nenda Pluijm; Watanzania, hususan wana Yanga watakukumbuka. Tu, usiwasahau wachezaji wetu utakapopata timu huko uendako. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KWA HERI PLUIJM; COACHES ARE HIRED TO BE FIRED HATA BILA YA SABABU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top