• HABARI MPYA

    Sunday, October 09, 2016

    KWA NINI MKATABA WA YANGA SC KUKODISHWA ULISAINIWA KIZANI?

    TAARIFA zilianza kuvujishwa Jumatano ya Oktoba 5, kwamba klabu ya Yanga SC imekodishwa kwa Kampuni ya Yanga Yetu, ambayo inaelezwa inamilikiwa na Mwenyekiti wa klabu, Yussuf Manji.
    Lakini taarifa yenyewe ilikuwa inasema kwamba, Mkataba baina ya Yanga Yetu na Baraza la Wadhamini wa Yanga SC ulisainiwa Septemba 3, mwaka huu – yaani mwezi mmoja uliopita.
    “Bodi ya Wadhamini wa Young Africans Sports Club, (ambayo hapa inajulikana kama Mmiliki”) imeingia tarehe 3 September, 2016 Mkataba wa kukodishwa na kampuni ijulikanayo Yanga Yetu Limited (inayojulikana hapa kama “Mkodishwaji” kwa muhtasari wa maazimio yaliyoafikiwa katika Mkutano Mkuu wa Young Africans Sports Club uliofanyika tarehe 6 Agosti, 2016 ulitambua kuwa Young Africans Sports Club (anayejulikana hapa kama “YANGA”).
    Leo sitaki kuzama ndani kuchambua vipengele vya Mkataba huo na mapungufu yake, kwa sababu kazi hiyo nitaifanya Jumatano – kwa Jumapili hii ninataka kuzungumzia shaka ya kwanza ya Mkataba huu ambayo ni pamoja na kutangazwa zaidi ya mwezi mmoja baada ya kusainiwa kwake.
    Taarifa ya Bodi ya Wadhamini wa Yanga ilimalizia kwa kusema; “Mwisho, tumeombwa na Bw. Yusuf Manji tutangaze hadharani Mkataba Huu, hata hivyo bado tunajadiliana kama kutangazwa huko kutakuwa kwa manufaa ya Klabu, kwa kuwa, kwa upande mmoja ni vema kuwa na uwazi, lakini kwa upande mwingine washindani wa Klabu yetu wataiga Mkataba wetu kwa manufaa yao,”.
    Mkanganyiko wa maelezo katika kipengele hiki ni sehemu ya wasiwasi wa kwanza wa Mkataba  huo – lakini kikubwa tu, kwa nini Baraza na Yanga Yetu hawakufanya zoezi lao kwa uwazi mbele ya vyombo vya Habari.
    Haiyumkiniki mikataba mizito kama hii yenye kubadilisha historia ya klabu kubwa kama Yanga ikafanywa kwa siri namna hii.
    Sijui Baraza la Wadhamini la Yanga, ambalo linapingwa na Baraza la Michezo kla Taifa (BMT) lilifikiria nini kufanya maamuzi ya ovyo namna hii.
    Yanga ni baba wa soka ya Tanzania – ndiyo klabu kongwe zaidi – labda Wajumbe wa Baraza la Wadhamini wa klabu hiyo, hawajui au wamesahau nitawakumbusha.
    Japokuwa historia inasema Yanga ilizaliwa mwaka 1935 na Simba mwaka 1936, lakini ukizama ndani utagundua kwamba, huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa utani na upinzani wa jadi, baina ya miamba hiyo ya soka nchini.
    Kulikuwa kuna timu inaitwa New Youngs, ambayo mwaka 1938 ilisambaratika na baadhi ya wachezaji wake wakaenda kuunda timu iliyokuwa ikiitwa Sunderland, ambayo hivi sasa inajulikana kama Simba.
    Kabla ya kutokea vurugu zilizoisambaratisha New Youngs, vijana wa Dar es Salaam walikuwa wana desturi ya kukutana viwanja vya Jangwani kufanya mazoezi na baada ya muda wakaamua kuunda timu yao, waliyoipachika jina Jangwani.
    Ndani ya kipindi kifupi tu, timu hiyo iliteka hisia za wengi, waliojitokeza kujiandikisha uanachama wa klabu hiyo. Miongoni mwa waliovutika na uanachama wa klabu hiyo ni Tarbu Mangara (sasa marehemu) na ilipofika mwaka 1926, walifanya mkutano wa kwanza katika eneo ambalo hivi kuna shule ya sekondari ya Tambaza.
    Miongoni mwa yaliyojadiliwa kwenye mkutano huo ni kuiboresha timu hiyo, ambayo wachezaji wake wengi walikuwa wafanyakazi wa Bandarini na mashabiki wake wengi walikuwa wabeba mizigo wa bandarini.
    Baada ya mkutano huo, timu hiyo ilibadilishwa jina na kuwa Navigation, iliyotokea kuwa moto wa kuotea mbali katika timu za Waafrika enzi hizo, kabla ya uhuru wa Tanganyika. Timu kama Kisutu, Kitumbini, Gerezani na Mtendeni zilikuwa hazifui dafu kwa wana Jangwani hao.
    Ikiwa inatamba kwa jina la Navigation, wanachama wa timu hiyo walikuwa wakitembea kifua mbele na kuwatambia wapinzani, kwamba wao ndiyo zaidi. Kwa sababu katika kipindi hicho, Italia ilikuwa inatamba kwenye ulimwengu wa soka, wanachama wa timu hiyo nao waliamua kuibadilisha jina timu yao na kuiita Taliana.
    Taliana ilipata mafanikio ya haraka na haikushangaza ilipopanda hadi Ligi Daraja la Pili Kanda ya Dar es Salaam, mwanzoni mwa miaka ya 1930. jina la Taliana waliamua kuachana nalo mapema, kabla ya kuingia kwenye ligi hiyo, hivyo wakaanza kujiita New Youngs.
    Lakini kila ilipokuwa ikibadilisha jina, ilikuwa ikifanya vitu pia, kwani wakiwa na jina la New Youngs, waliweza kutwaa Kombe la Kassum, lililoshirikisha timu mbalimbali za Dar es Salaam. 
    Hatimaye ukawadia mwaka mbaya kwa New Youngs, 1938 wakati baadhi ya wachezaji walipojitoa na kwenda kuanzisha Sunderland. Kwa sababu hiyo, waliobaki wakaamua kubadili jina na kuwa Young Africans, jina ambalo mashabiki wake wengi walishindwa kulitamka vizuri hivyo kujikuta wakisema Yanga.
    Kwa historia hii, pamoja na ukweli uliopo kwamba klabu hii ilitumika na waasisi wa taifa hili katika harakati za Uhuru – unagundua hii si klabu ya mchezo mchezo kama wengine wanavyofikiria.
    Ilikopitia kutoka New Youngs, Navigation, Taliana hadi Young Africans, maarufu Yanga unawezaje kwenda kuikodisha ‘uchochoroni’?
    Katika zama hizi za uwazi na ukweli, Baraza la Wadhamini la Yanga na Mkodishaji wa klabu walikwepa nini kufanya zoezi hili zito mbele ya Vyombo vya Habari?
    Siku chache zilizotangulia, Manji alikwenda kuikabidhi Yanga kiwanja eneo la Geza Ulole, Kigamboni, Dar es Salaam ijenge Uwanja wa kisasa na kituo cha kukuza vipaji vya vijana.
    Siku hiyo Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Mchemba aliinuliwa ofisini akawe mgeni rasmi, lakini katika shughuli nzito zaidi na ya kihistoria kwa klabu, Mkataba umesainiwa chemba na kuja kutangazwa mwezi mmoja baadaye. 
    Mkataba huu ulipaswa kusainiwa kwenye Mkutano na Waandishi wa Habari kwa uwazi na ingependekeza zaidi kama kiongozi mmoja mkubwa wa Serikali angekuwepo kwa ushuhuda. 
    Siku zote nasema, Jerry Muro na Baraka Deusdedit ni ‘watoto wadogo’ mno ambao siyo tu hawaijui Yanga bali hata Uyanga wao kwa kuwa ulijulikana baada ya kuajiriwa na klabu ni wa mashaka mashaka na hawa sidhani kama wanaweza kuwa na uchungu na klabu.
    Wenye uchungu na klabu ni watu kama akina Francis Mponjoli Kifukwe ambao wamepata nayo tabu hii klabu wakati fulani, ila nao imefikia wakati wanachukua maamuzi mazito kizani.  
    Inawezekana mpango huu ukawa mzuri na umekuja katika wakati mwafaka, kwamba Yanga inahitaji kubadilika kwa namna yoyote, lakini wasiwasi wa kwanza ni Mkataba ni kusainiwa kizani. 
    (Kunako majaaliwa – Juamatano nitaanza kuuchambua Mkataba wenyewe  kwa kuanza na hatari ya kuruhusiwa kusajiliwa kampuni ya Yanga Yetu, ambayo ndiyo imeikodisha Yanga SC)
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KWA NINI MKATABA WA YANGA SC KUKODISHWA ULISAINIWA KIZANI? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top