• HABARI MPYA

    Friday, November 04, 2016

    RAIS MAGUFULI AWATUMIA SALAMU SIMBA SC; "NAPENDA MICHEZO, SIPENDI WAVUNJA VITI"

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Joseph Magufuli amesema kwamba bora kwenda kuangalia michuano ya mchangani kama Ndondo Cup kuliko mechi ya Simba na Yanga ambayo mashabiki wanavunja viti baada ya kufungwa.
    Rais Magufuli ameyasema hayo Ikulu mjini Dar es Salaam leo wakati alipokutana na Wahariri wa vyombo mbalimbali vya Habari nchini kwa ajili ya maswali na Majibu kuazimisha mwaka wake mmoja madarakani.
    Pamoja na kuzungumzia kwa muhtasari mwaka wake mmoja madarakani namna alivyoweza kuleta mabadiliko kiutawala na kiuchumi, lakini mwishoni Rais Magufuli akagusia kidogo kuhusu michezo.

    Rais Magufuli amesema bora akaangalie Ndondo Cup kuliko Simba na Yanga wakivunja viti

    “Napenda michezo, lakini sipendi kuona timu zinang’oa viti. Bora nikaangalie Ndondo Cup kuliko kwenda kuangalia timu zikifungwa zinang’oa viti,”alisema Magufuli.
    Aidha, Rais huyo wa tano wa Tanzania baada ya Julius Kambarage Nyerere (sasa Nyerere), Ali Hassan Mwinyi, Benjamin William Mkapa Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, aliipongeza Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo juu ha hatua iliozchukua baada ya vurugu za kuvunja viti kwenye mechi ya Simba na Yanga.
    “Niipongeze Wizara kwa hatua iliyochukua kuzizuia kutumia Uwanja. Lazima ifike wakati tuwe na uchungu. Tuwe na mioyo ya kizalendo na kujali vitu vyetu na ni kuvitunza. Uwanja ule umejengwa kwa kodi za Watanzania wote, lazima uheshimiwe,”alisema Rais Magufuli.  
    Rais alikuwa anazungumzia tukio la Oktoba 1, mwaka huu katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati mashabiki wa Simba SC walipofanya vurugu hadi kuvunja viti.
    Mashabiki wa Simba walifanya vurugu Uwanja wa Taifa Oktoba 1, mwaka huu baada ya Yanga kupata bao la kuongoza lililofungwa na mshambuliaji Mrundi, Amissi Joselyn Tambwe katika mchezo wa Ligi Kuu.
    Tambwe alifunga bao lake dakika ya 26, akimalizia pasi ndefu ya beki Mbuyu Twite na kugeuka mbele ya beki wa Simba, Novat Lufunga kabla ya kufumua shuti lililomshinda kipa Vincent Angban.
    Bao hilo lilizua kizaazaa, wachezaji wa Simba wakimvaa refa Martin Saanya wakidai mfungaji, Tambwe aliushika mpira kabla ya kufunga.
    Katika vurugu hizo, Saanya alimtoa kwa kadi nyekundu Nahodha wa Simba SC, Jonas Mkude dakika ya 29 kwa sababu ndiye aliyekuwa mstari wa mbele.
    Na mchezo ukasimama kwa takriban dakika tano baada ya mashabiki wa Simba kuanza kufanya vurugu waking’oa viti na kutupa uwanjani.
    Polisi walitumia milipuko ya gesi za kutoa machozi kuwatuliza mashabiki hao na mchezo ukaendelea hadi Simba SC wakasawazisha dakika ya 87 kwa bao la Shizza Kichuya.
    Oktoba 2, Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Nape Nnauye akasema Rais kwamba Magufuli alikuwa anautazama mchezo huo moja kwa moja kupitia Azam TV na akajionea mwenyewe vurugu na chanzo chake.
    Nape akasema Rais Magufuli alikasirika mno na akataka hatua kali zichukuliwe, lakini akamtuliza na mwishowe hatua iliyochukuliwa ni kuzizuia timu hizo kutumia Uwanja huo.  
    Aidha, Serikali pia ikazuia mapato ya mchezo huo hadi hapo itakapokata gharama za uharibifu uliosababishwa na vurugu hizo. 
    Nape alisema kwamba mbali na uvunjwaji wa viti, pia mageti mawili ya kuingilia, moja la upande wa Yanga na lingine wa Simba yalivunjwa.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: RAIS MAGUFULI AWATUMIA SALAMU SIMBA SC; "NAPENDA MICHEZO, SIPENDI WAVUNJA VITI" Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top