• HABARI MPYA

    Sunday, May 10, 2015

    SIMBA SC ‘IBOMOE’ BENKI KUSAJILI WACHEZAJI KWELI, VINGINEVYO…

    JULAI 16, mwaka jana, Uwanja wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) nilifanya mahojiano na aliyekuwa kocha wa Simba SC, Zdravko Logarusic.
    Wakati tayari Simba SC imekwishakamilisha usajili wake na imeanza mandalizi ya msimu mpya, nilimuuliza Loga anaionaje timu kuelekea msimu mpya.
    Ingizo jipya kikosini wakati huo walikuwa vijana kama Peter Manyika, Hussein Sharrif ‘Casillas’, wote makipa, beki Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, kiungo Abdi Banda na washambuliaji Mkenya, Paul Kiongera, Ibrahim Hajib na Elias Maguri.   
    Mcroatia huyo akasema kwamba anahitaji wachezaji wapya watatu wa kimataifa katika kikosi chake, beki, kiungo mkabaji na mshambuliaji ili awe na timu bora ya ushindani.

    Alisema kwamba anahitaji wachezaji hao, wenye uzoefu ambao atawaunganisha na alionao ili kuwa na Simba bora.
    Namnukuu; “Hakika ninahitaji wachezaji wenye sifa za kimataifa, nahitaji beki mmoja, kiungo wa ulinzi na mshambuliaji, ili niwaunganishe na nilionao kupata kikosi bora,”alisema.
    Na akawazungumzia wachezaji wapya chipukizi waliosajiliwa, akisema kwamba wanatakiwa kujituma ili kufikia kiwango cha kimataifa, kwa sababu Simba SC ni timu kubwa na wao lazima waonyeshe uwezo mkubwa.
    “Wametoka timu ndogo ndogo na wana vipaji, lakini wanatakiwa kufanya bidii hapa, kwa sababu Simba ni timu kubwa, lazima waonyeshe uwezo wa kimataifa,”alisema.
    Kwa bahati mbaya Logarusic akafukuzwa Agosti na timu haikusajili aina ya wachezaji aliowataka kocha huyo, zaidi ya mshambuliaji Emmanuel Okwi aliyetua kwa ngekewa tu.
    Okwi alirejea Simba SC baada ya kujikuta katika mgogoro na iliyokuwa klabu yake, Yanga SC, nadiriki kusema ilikuwa ngekewa- kwa sababu kama si huo mgogoro angebaki Jangwani.
    Patrick Phiri, kocha Mzambia aliyeajiriwa baada ya kufukuzwa Logarusic naye akafukuzwa Desemba, timu ikiwa haina matokeo mazuri.
    Pamoja na kumfukuza Phiri, Simba SC ikafanya usajili mzito kidogo Desemba, ikiwachukua beki Juuko Murushid na washambuliaji Simon Sserunkuma na Dan Sserunkuma kuungana na Waganda wenzao, Joseph Owino na Okwi. 
    Kiongera alitemwa Desemba sababu ya maumivu ya goti, viungo Amri Kiemba na Haroun Chanongo walitolewa kwa mkopo kwa madai walikuwa hawajitumi.
    Mserbia Goran Kopunovic akarithi mikoba ya Phiri na akaanza vyema kwa kuipa timu Kombe la Mapinduzi Janauri.
    Kuingia kwenye Ligi Kuu, Goran amefanikiwa kuifanya Simba SC imalize katika nafasi ya tatu nyuma ya Yanga na Azam.
    Lakini kwa mwaka wa tatu, mwakani Simba SC hawatacheza michuano ya Afrika, wakiziacha Yanga na Azam ziendelee kuwakilisha nchi.
    Baada ya matokeo hayo, maoni mbalimbali yamekuwa yakitolewa kuhusu kuyumba kwa Simba SC, lakini hoja ya msingi inabaki katika muundo wa kikosi.
    Simba SC lazima iwe na kikosi mseto, chenye mchanganyiko wa wachezaji chipukizi na wazoefu, ili iweze kucheza ligi kwa ufanisi.
    Kwa sasa ukitazama vijana wengi wadogo waliosajiliwa hivi karibuni wamekomaa- iwapo wataongezewa wazoefu wa kiwango cha kimataifa kama alivyoshauri Logarusic, basi tarajia kitu tofauti msimu ujao kutoka Msimbazi.
    Wachezaji kama Hassan Kessy, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Hassan Isihaka, Jonas Mkude, Said Ndemla, Abdi Banda, Ibrahim Hajibu, Elias Maguri wote wanakuja vizuri.
    Pamoja na waoefu wachache kama Ivo Mapunda, Ramadhani Singano ‘Messi’, Okwi, Juuko- iwapo wataongezwa wachezaji watatu wengine wa kiwango cha kimataifa, Simba itakuwa vizuri msimu ujao.
    Na hapa Simba SC lazima iwe tayari kutumia fedha nyingi ili kupata wachezaji bora. Kama itaendelea na desturi ya kutaka wachezaji wa bei rahisi, itawawia vigumu kurudisha makali yao.
    Mchezaji mkubwa anataka dau kubwa la usajii pamoja na mshahara pia. Simba SC wawe tayari kutekeleza hayo ili wapate wachezaji kweli.
    Dan Sserunkuma alikuwa mfungaji bora Kenya, kweli- lakini muulize mtu yeyote atakuambia Ligi ya Tanzania ni ngumu zaidi kuliko huko alipotoka.
    Simon ni chipukizi mwenye kipaji- maana yake wote hawa wanahitaji muda ili kuweza kumudu mikiki ya Ligi Kuu ya Vodacom. 
    Tunaona hata Ulaya, timu zilizoyumba kama Manchester United zimeamua ‘kubomoa’ benki kusajili wachezaji wakubwa. Na kweli, Man U msimu huu kidogo tamu na huenda mwakani ikarejea Ligi ya Mabingwa.
    Sasa Simba SC waamue kusuka, au kunyoa, lakini ukweli ndiyo huo, wanahitaji kutumia fedha kusajili wachezaji wa kimataifa kweli. Alamsiki. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC ‘IBOMOE’ BENKI KUSAJILI WACHEZAJI KWELI, VINGINEVYO… Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top