• HABARI MPYA

    Wednesday, November 07, 2012

    VIONGOZI SIMBA WANALEA MARADHI, LEO KASEJA, KESHO KAPOMBE, YETU MACHO


    INADAIWA Nahodha wa Simba, Juma Kaseja ameamua kuachana na timu hiyo na tayari amewaaga wachezaji wenzake na kuwaambia yeye na klabu hiyo basi.
    Kwa mujibu wa wachezaji wenzake, Kaseja ameamua Simba basi, baada ya kuumizwa kwa jinsi alivyodhalilishwa na mashabiki Jumamosi Morogoro.
    Na Mahmoud Zubeiry
    “Juma hapa ndio basi kaka, Kasema yeye na Simba basi, amesononeshwa mno na jinsi alivyodhalilishwa baada ya mechi ya Morogoro,”alisema mchezaji mmoja wa Simba baada ya mazoezi ya timu hiyo Uwanja wa Kinesi jana.
    Kaseja alitukanwa na kutishiwa maisha na mashabiki wa Simba baada ya mechi dhidi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro wakimtuhumu kufungwa mabao ya kizembe.
    Ezekiel Kamagwa, Ofisa Habari wa Simba, ni rafiki yangu, na tumesoma naye shule moja licha ya kufanya naye kazi ofisi moja pia, alinisimulia tukio la Kaseja kuanzia Morogoro uwanjani, hadi kwenye basi njiani akaniambia alilia baada ya kuona aliyokuwa akifanyiwa Kaseja.
    Kwa kifupi, Kamwaga alisema Kaseja alitukanwa yeye, familia yake hadi na mama yake na pia akatishiwa maisha.
    Kisa, kufungwa kwenye mechi na Mtibwa mabao mawili. Najaribu kujiuliza Icer Casillas, aliyefungwa mabao sita Real Madrid ikichapwa na Barcelona nchini Hispania kwa nini hadi leo ni kipa namba moja wa klabu hiyo na anaheshimika kwa kiasi kikubwa, ikiwa Kaseja anasulubiwa kwa kipigo cha Mtibwa?
    Sahau kuhusu yote, huyo ni binadamu kama binadamu wengine wote, kukosea si ajabu, lakini hiyo siyo hukumu ya kumpa.
    Simba ina benchi la ufundi, na hapana shaka limeyaona mapungufu ya Kaseja hivyo kama kuna umuhimu wa mabadiliko yatafanywa, ila si mashabiki kwenda kumdhalilisha kama walivyofanya.
    Wanapata wapi ujasiri huo na hiyo ni tabia gani ya kishenzi? Lakini tujiulize, hawa ni mashabiki wa kawaida tu au wana ajenda zao nyingine?
    Nastaajabu sana viongozi wa siku hizi wa soka katika nchi hii, wanachezewa hadi barazani kwao. Wanatiwa vidole mpaka sehemu za hatari na watu ambao wanadhibitika, tena kwa urahisi sana.
    Watu waliomfanyia fujo Kaseja hawakuwa wakazi wa Morogoro, ni watu ambao walitoka Dar es Salaam kwenda Morogoro kushuhudia mechi. Ni watu ambao naamini kabisa tunawajua na tuna uwezo wa kuwachukulia hatua, tukiamua- ili liwe fundisho kwa wajinga wengine.
    Watu wakishakuwa kwenye macho ya watu wengi wanakuwa na ujasiri wa kufanya lolote, kwa sababu wanajua hakuna watakachofanywa. Lakini tunalea maradhi mabaya sana.
    Yule aliyekuwa Mwenyekiti wa Yanga, Wakili Lloyd Nchunga alivamiwa hadi nyumbani kwake na mashabiki, lakini taarifa ikasema watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi. Tunajua ukweli, lakini kwa kuwa tumeridhika na tumeona hiyo ndiyo staili ya maisha ya soka ya Tanzania, tunachukulia poa tu.
    Hawa watu sasa wanatukana, wanadhalilisha, ila kwa sababu naamini wanadekezwa, ipo siku watakuja kupiga hadi kuua. Kutoka hapo, kama ambavyo ilivyo desturi ya nchi yetu, tahadhari huchukuliwa baada ya hatari, basi ndipo hatua itachukuliwa.
    Kamwaga ananiambia wale wajinga walipaki gari lao karibu na basi la Simba likiwa njiani kurejea Dar es Salaam wakataka kumtoa Kaseja kwenye basi wampige na baada ya kumkosa, hasira zao zikaishia kumtukana.
    Nilistaajabu sana, hao watu walifika Dar es Salaam salama, na kama ni hivyo kesho watashindwa nini kumfanyia hivyo na Shomari Kapombe au Mwinyi Kazimoto?
    Viongozi waliokuwa katika msafara wa Simba walishindwaje kutoa taarifa Polisi ili msafara wa watu hao waliofanya ushenzi huo ukamatwe na wahusika wachukuliwe hatua? Tunalea maradhi.
    Na kama kweli tumeamua kulea maradhi, basi tusubiri maafa yakitokea ndipo tutachukua hatua. Nashangaa sana, viongozi wa klabu zetu na soka Tanzania kwa ujumla kama hawawezi hata haya mambo madogo madogo, sasa tutarajie wataweza nini?
    Namheshimu sana Juma Kaseja, kama mmoja wa makipa bora waliowahi kutokea Tanzania na ningependa ajue, yanayomtokea yeye sasa yalimtokea pia hata Athumani Mambosasa na Mwameja Mohamed, makipa wengine bora kabla yake pale Simba na Tanzania kwa ujumla.
    Mambosasa na Mwameja nao, baada ya kuitumikia Simba vizuri na kuipa heshima kubwa, hawakuagwa vizuri, walidhalilishwa hivyo kwa kuambiwa wamefungisha na kufanyiwa udhalili.
    Hii ni desturi ambayo tunailea miaka nenda, rudi sasa, ila naamini iko siku italeta maafa makubwa, iwapo hatua hazitachukuliwa, kwa sababu wahenga walisema mtoto umleavyo ndivyo akuavyo na kama hatuwezi kumkunja samaki mbichi, sijui itakuwaje hapo baadaye. Alamsiki.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: VIONGOZI SIMBA WANALEA MARADHI, LEO KASEJA, KESHO KAPOMBE, YETU MACHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top