• HABARI MPYA

  Sunday, February 13, 2022

  SIMBA YAICHAPA ASEC 3-1 KOMBE LA SHIRIKISHO


  WENYEJI, Simba Sports Club wameanza vyema mechi za Kundi D Kombe la Shirikisho Afrika baada ya ushindi wa 3-1 dhidi ya mabingwa wa zamani Afrika, ASEC Mimosas jioni ya leo Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
  Mabao ya Simba SC yamefungwa na kiungo Msenegal, Pape Ousmane Sakho dakika ya 12 kwa til-tak akimalizia krosi ya beki wa kulia, Shomari Salum Kapombe ambaye alifunga bao la pili kwa penalti dakika ya 79.
  Penalti hiyo ilitolewa baada ya kipa wa ASEC, Abdoul Karim Cissé kugongana na winga wa Simba, Yussuf Valentine Mhilu kwenye boksi.
  Na ilikuja baada ya kiungo Stephane Aziz Ki kuisawazishia ASEC dakika ya 60, kufuatia kumhadaa beki Mkongo wa Simba, Hennock Inonga Baka ‘Varane’ kabla ya kumchambua kipa namba moja Tanzania, Aishi Salum Manula.
  Kiungo wa kimataifa wa Malawi, Peter Banda akaihakikishia Simba SC pointi tatu katika mechi ya kwanza ya Kundi D kwa bao lake zuri dakika ya 81 akimalizia pasi ya Nahodha, John Raphael Bocco.
  Mechi nyingine ya kundi hilo, wenyeji, RSB Berkane wameichapa 5-3 Union Sportive Gendarmerie Nationale Uwanja wa MAnispaa ya Berkane Jijini Berkane. Mechi ijayo Simba itakuwa ugenini kuwafuata Union Sportive Gendarmerie Nationale Jumapili ijayo Uwanja wa Jénérali Seyni Kountché Jijini Niamey nchini Niger.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA YAICHAPA ASEC 3-1 KOMBE LA SHIRIKISHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top