MABINGWA wa Tanzania, Simba SC wamepoteza mechi ya kwanza Kundi D Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuchapwa 2-0 na wenyeji, RSB Berkane usiku wa Jumapili Uwanja wa Manispaa ya Berkane nchini Morocco.
Mabao ya Berkane yote yalipatikana kipindi cha kwanza la kwanza shuti la mpira wa adhabu la kiungo wa kimataifa wa Mauritania, Adama Ba dakika ya 32 na la pili kiungo Mmorocco, Charki El Bahri dakika ya 41.
Mechi nyingine ya kundi hilo jana, wenyeji, Union Sportive Gendarmerie Nationale (USGN) wameichapa AS des Employés de Commerce (ASEC) Mimosas 2-0 mabao ya Wilfried Gbeuli dakika ya 63 na Victorien Adebayor dakika ya 90 Uwanja wa Jénérali Seyni Kountché mjini Niamey nchini Niger.
Sasa Berkane inaongoza Kundi D kwa pointi zake sita, ikifuatiwa na USGN na Simba zenye pointi nne kila moja, wakati ASEC yenye pointi tatu inashika mkia.
Mechi zijazo ASEC Mimosas watakuwa wenyeji wa USGN Jijini Abidjan nchini Ivory Coast na Simba watawakaribisha Berkane Jijini Dar es Salaam Machi 13.
0 comments:
Post a Comment