• HABARI MPYA

  Sunday, February 13, 2022

  CHELSEA YAWA KLABU BINGWA YA DUNIA 2022


  MABINGWA wa Ulaya, Chelsea usiku wa jana wamefanikiwa kutwaa taji la Klabu Bingwa ya Dunia ya FIFA kwa mara ya kwanza katika historia yao baada ya ushindi wa 2-1 dhidi ya Palmeiras ya Brazil Uwanja wa Mohammed Bin Zayed, Abu Dhabi, Falme za Kiarabu.
  Romelu Lukaku alianza kuifungia Chelsea dakika ya 54, kabla ya Raphael Veiga kuisawazishia Palmeiras kwa penalti dakika ya 64 na Kai Havertz akafunga bao la ushindi dakika ya 117 kwa penalti pia.
  Katika mchezo huo, mabingwa wa Copa Libertadores walimaliza 10 kufuatia Luan kutolewa kwa kadi nyekundi dakika ya 120 na ushei baada ya kuonyeshwa kadi ya pili ya njano.
  Baada ya mchezo huo, imetipotiwa shabiki mmoja wa  Palmeiras aliuawa usiku wa jana nje ya Uwanja wa klabu hiyo kufuatia vurugu zilizoibuka mtaani baada ya timu yao kuchapwa 2-1 na Chelsea.
  Mpelelezi wa Jeshi la Polisi Jijini Sao Paulo, Cesar Saad amewaambia Waandishi wa Habari kwamba mshukiwa amekamatwa na kwamba watu wengine 15 walijeruhiwa katika tukio lililohuisha mapigano dhidi ya Polisi au baina yao mashabiki.
  Mashabiki wengi wa Palmeiras wana utamaduni wa kukutana maeneo ya Uwanja wa klabu hiyo kutazama mechi inapocheza ugenini.
  Mapema katika mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu, mabingwa wa Afrika, Al Ahly waliwachapa mabingwa wa Asia, Al Hilal 4-0 Uwanja wa Al Nahyan  Jijini Abu Dhabi.
  Mabao ya timu ya Misri yakifungwa na Hamdi Fathi dakika ya nane, Yasser Ibrahim dakika ya 17, Ahmed Radwan dakika ya 40 na Amr El Soleya dakika ya 64.
  Mabingwa wa Asia, Hilal walimaliza pungufu ya wachezaji wawili kufuatia wachezaji wawili kutolewa kwa kadi nyekundu kipindi cha kwanza, Mohammed Kanno dakika ya 28 na Matheus Pereira dakika ya 14.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: CHELSEA YAWA KLABU BINGWA YA DUNIA 2022 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top