• HABARI MPYA

  Jumapili, Machi 01, 2020

  SAMATTA APIGA BAO TAMU LAKINI ASTON VILLA YACHAPWA 2-1 MANCHESTER CITY FAINALI KOMBE LIGI ENGALND

  Na Mwandishi Wetu, LONDON
  MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta amefungia timu yake, Aston Villa bao la kufutia machozi ikichapwa 2-1 na Manchester City katika fainali ya Kombe la Ligi England usiku wa leo Uwanja wa Wembley Jijini London.
  Samatta aliyejiunga na Villa Januari akitokea KRC Genk ya Ubelgiji, timu yake ya kwanza Ulaya iliyomtoa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), alifunga bao hilo dakika ya 41 akimalizia pasi ya kiungo Mholanzi, Anwar El Ghazi.
  Na hiyo ilifuatia Manchester City inayofundishwa na kocha Mspaniola, Pep Guardiola kutangulia kwa mabao ya mshambuliaji wake tegemeo, Muargentina Sergio Aguero dakika ya 20 akimalizia pasi ya Philip Foden na Rodri Hernandez akimalizia pasi ya İlkay Gundogan dakika ya 30.

  Mbwana Samatta akiifungia Aston Villa bao la kufutia machozi ikichapwa 2-1 na Manchester City katika fainali ya Kombe la Ligi England leo Uwanja wa Wembley 

  Baada ya kazi yake nzuri ambayo hata hivyo haikuisaidia Aston Villa kupata taji, kocha Dean Smith alimpumzisha Samatta dakika ya 80 na kumuingiza kinda wa England, Keinan Davis.
  Ushindi wa leo unamaanisha Manchester City inatwaa taji la Carabao kwa mara ya tatu mfululizo na kujifariji katika msimu ambao hawana matokeo mazuri kwenye Ligi Kuu. 
  Kikosi cha Aston Villa kilikuwa; Nyland, Guilbert, Engels, Mings, Elmohamady/Trezeguet dk70, Nakamba, Douglas Luiz, Targett, El Ghazi/Hourihane dk70, Samatta/Davis dk80 na Grealish.
  Man City: Bravo, Walker, Stones, Fernandinho, Zinchenko, Gundogan/De Bruyne dk58, Rodri, Silva/Bernardo Silva dk76, Sterling, Aguero/Jesus dk83 na Foden.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SAMATTA APIGA BAO TAMU LAKINI ASTON VILLA YACHAPWA 2-1 MANCHESTER CITY FAINALI KOMBE LIGI ENGALND Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top