• HABARI MPYA

    Tuesday, March 17, 2020

    TFF YASIMAMISHA LIGI KUU KUTII AGIZO LA WAZIRI MKUU, YAVUNJA RASMI NA KAMBI YA TAIFA STARS

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limesimamisha ligi zake zote ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kufuatia mlipuko wa virusi vya ugonjwa wa COVID 19 ambao umeingia nchini.  
    Pia TFF imevunja kambi ya timu ya taifa, Taifa Stars ambayo ilikuwa inajiandaa na fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) zilizopangwa kuanza Aprili 4 hadi 25, mwaka huu nchini Cameroon.
    Taarifa ya TFF imesema kwamba kikao cha Kamati ya Uongozi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara kilichoitishwa na Rais wa shirikisho hilo, Wallace Karia leo kitafanyika kama kawaida kesho Saa 3:00 asubuhi hoteli ya Golden Tulip Jijini Dar es Salaam, lakini kwa lengo la kutoa mwelekeo wa utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu.

    Tayari Ligi mbalimbali duniani, ikiwemo michuano ya Afrika imesimamishwa kwa hofu ya maambukizi ya ugonjwa huo hatari – na leo Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limetoa tamko la kuahirisha fainali za CHAN.
    Na hiyo ni baada ya CAF kuahirisha mechi za tatu na za nne za kufuzu Fainali za Kombe za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2021 baina ya Tanzania na Tunisia zilizokuwa zifanyike mwishoni mwa mwezi huu Tunis na Dar es Salaam zimeahirishwa.
    Kwa ujumla CAF imesimamisha mechi zote za kufuzu za mashindano ya Afrika kwa ushauri wa Shirika la Afya Dunani (WHO) kufuatia mlipuko wa virusi COVID-19 hadi hapo itakapaoamuliwa vinginevyo.
    Mechi zilizofutwa ni za tatu za na za nne kufuzu Fainali za AFCON 2021 ambazo zilipangwa kufanyika kati ya Machi 25 na 31 mwaka huu, kufuzu Fainali za Kombe la Dunia la Wanawake chini ya umri wa miaka 20 zilizopangwa kufanyika kati ya Machi 20 na 22 na marudiano Machi 27 na 29 mwaka huu.
    Aidha, CAF pia imesitisha mechi za kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa (AFCON) kwa Wanawake 2020 zilizopangwa kufanyika kati ya Aprili 8 na 14 mwaka 2020 – na ratiba mpya ya michuano hiyo itatangazwa kwa wakati.
    Ligi Kuu inasimama huku Simba SC wakiwa wanaongoza kwa pointi zao 71, wakifuatiwa na Azam FC pointi 54 baada ya wote kucheza mechi 28, wakati vigogo, Yanga SC ni wa tatu kwa pointi zao 51 za mechi 27 na Namungo wa nne wakiwa na pointi 50 za mechi 28.
    Hali ni mbaya kwa Singida United inayoshika mkia kwa pointi zake 15 za mechi 29, nyuma ya Mbao FC pointi 22 mechi 28, Alliance FC pointi 29, mechi 29, Mbeya City pointi 30 mechi 29 na Ndanda FC pointi 31 mechi 29.

    Jioni ya leo, Waziri Mkuu, Majaliwa ametoa tamko la kusimamisha michezo yote nchini kwa siku 30 ikiwa ni pamoja na kufunga shule zote, kuanzia za mwanzo, Msingi hadi Sekondari Kidato cha sita kufuatia ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona (COVID-19) kuingia nchini.
    Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema hayo wakati akitoa msimamo wa Serikali kuoitia vyombo vya habari kuhusiana ugonjwa huo.
    “Tumefunga shule zote kuanzia za awali hadi kidato cha sita, tumesitisha michezo yote ikiwemo ligi kuu na Serikali imefikia uamuzi huo ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo nchini” alisema Waziri Mkuu.
    Akitaja hatua mbalimbali ambazo Serikali inaendelea kuchukua ni pamoja na kuzuia mikusanyiko yote ambayo si ya lazima kufanyika kama vile semina na shughuli mbalimbali za kijamii.
    Aidha, Waziri Mkuu Majaliwa, alisema kuwa Serikali imeendelea kufuatilia abiria wanaoingia nchini kupitia maeneo ya viwanja vya ndege na mipakani, kwa kuwapima abiria ili kubaini kama wanamaambukizi, sambamba na kuimarisha maabara ili iweze kupima na kutambua endapo kuna maambukizi.
    “Tumetenga kambi maalum eneo la Mloganzila jijini Dar es Salaam, kituo cha afya cha Buswelo huko Mwanza, hospitali ya Mawenzi ya mkoani Kilimanjaro pamoja na hospitali za Mnazi mmoja, Zanzibar na Chakechake huko Pemba, ambazo zitatumika kuhudumia wagonjwa wa Corona” alisema Waziri Mkuu.
    Sambamba na hilo, Waziri Mkuu alisema kuwa jitihada nyingine zilizofanywa na Serikali ni kusitisha shughuli za Mwenge na badala yake fedha hizo shilingi bilioni moja zimeelekezwa Wizara ya Afya ili kuwezesha shughuli mbalimbali zitakazosaidia kupambana na ugonjwa huo na tayari shilingi milioni 500 zimeshakabidhiwa Wizara ya Afya.
    Aidha, Waziri Mkuu ametoa angalizo kwa Wizara ya Afya na wafanyabiashara na kusisitiza: “Wizara ya Afya ihakikishe vifaa vya kinga ikiwemo vimiminika vya kuthibiti maambukizi (hand sanitizer) vinapatikana katika maduka yote husika na kwa bei ya kawaida na Serikali itachukua hatua kwa wafanyabiashara watakaobainika kufanya ulanguzi wa viaa hivyo.”
    Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya kote nchini kufuatilia kwa karibu na kufanya uchunguzi kuhusu wageni watakao ingia katika maeneo, na wananchi wametakiwa kutoa taarifa katika namba za bure za 0800110037/0800110124 na 0800110125 pindi watakapohisi kuwa na dalili za ugonjwa wa Corona ili Serikali iweze kuchukua hatua za haraka.
    Ugonjwa wa Corona ulioanza Disemba mwaka jana nchini China, umesambaa  zaidi katika nchi 150 duniani, na mgonjwa wa kwanza kugundulika nchini  ni Machi 16 mwaka huu ambaye aliwasili nchini kutoka Ubelgiji.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TFF YASIMAMISHA LIGI KUU KUTII AGIZO LA WAZIRI MKUU, YAVUNJA RASMI NA KAMBI YA TAIFA STARS Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top