• HABARI MPYA

  Jumatatu, Machi 09, 2020

  WIZARA ZA MICHEZO ZANZIBAR NA TANZANIA ZAAZIMIA KUREJESHA LIGI YA MUUNGANO ‘KIMAPINDUZI’

  Na Salum Vuai, WHUMK
  WIZARA zenye dhamana ya michezo Zanzibar na Tanzania, zimeazimia kuyaongeza hadhi mashindano ya Kombe la Mapinduzi kwa kuyapa sura halisi ya Muungano.
  Azma hiyo imebainika katika kikao cha viongozi na watendaji wa wizara hizo kilichomalizika mwishoni mwa wiki kwenye ukumbi wa ZSSF Kariakoo mjini Zanzibar.
  Katika kikao hicho cha siku tatu, mawaziri wa wizara hizo walijadiliana na kusaini makubaliano ya kushirikiana kwenye mambo mbalimbali kwa dhamira ya kuimarisha Muungano wa pande mbili, Zanzibar na Tanzania Bara.
  Ushauri wa kurejesha Ligi ya Muungano ya mpira wa miguu iliibuliwa na Waziri wa Vijana, Utamaduni Sanaa na Michezo wa Zanzibar Balozi Ali Abeid Karume, ambaye alisema ilipokuwepo ilisaidia kupata kikosi bora cha timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars.
  Balozi Karume alisema kurejeshwa kwa ligi hiyo kutaongeza hamasa na kustawisha vuguvugu la soka na michezo mingine kwa jumla, sambamba na mapenzi kwa klabu za hapa nchini na timu za Taifa.
  Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale Mahmoud Thabit Kombo aliyekuwa Mwenyekiti wa kikao hicho, alisema kwa kiasi fulani, kufutwa kwa Ligi Kuu ya Muungano kumewakosesha uhondo mashabiki na kupunguza ari ya kushindana kwa wachezaji.
  Akitoa ufafanuzi juu ya ushauri huo, Mkurugenzi wa Michezo Tanzania Bara Yussuf Singo, alisema Ligi ya Muungano ililazimika kufutwa kwa kupoteza uhalisia juu ya sababu za kuanzishwa kwake.
  “Ligi Kuu ya Muungano ilianzishwa kwa kushirikisha timu nne zinazoshika nafasi za kwanza na ya pili kwenye Ligi Kuu za Bara na Zanzibar ili kupata wawakilishi wa mashindano ya klabu bingwa na Kombe la Shirikisho Afrika,” alisema Singo.
  Aidha alisema, katika miaka ya karibuni, kumeanzishwa mashindano kadhaa Tanzania Bara ambayo mara nyengine yanaingilia ratiba za Ligi Kuu ya huko, akiyataja baadhi kuwa ni yale ya Azam yanayoandaliwa kupata mwakilishi wa Kombe la Shirikisho pamoja na Sport Pesa, huku suala la gharama likitatiza pia.  
  Hata hivyo, alifahamisha kuwa baada ya Zanzibar kupata uanachama shirikishi wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na kuwa na haki ya kutoa wawakilishi wake kwenye michuano hiyo, hakukuwa na mantiki ya kuendelea na Ligi Kuu hiyo.
  Lakini alisema, kumekuwa na mapendekezo yanayoendelea kujadiliwa juu ya kuangalia uwezekano wa kuyaongezea mvuto na idadi ya timu shiriki mashindano ya Kombe la Mapinduzi ili yabebe sura halisi ya Muungano.
  Kamishna wa Michezo katika Wizara ya Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo Zanzibar Sharifa Salim Khamis, alisema kurejesha ligi hiyo ni jambo jema, lakini kwa kuwa sababu yake haipo, wanachoangalia sasa ni kuliimarisha Kombe la Mapinduzi.
  Alisema wanakusudia kukutana baina ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na ZFF kwa  Zanzibar, ili kuhakikisha wanakuja na mfuno mzuri wa kuendesha mashindano hayo ambayo tayari yamepata umaarufu mkubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki.
  Alisema miongoni mwa mambo muhimu katika kuyapa nguvu mashindano hayo, ni kutafuta baraka za CAF ili iyakubali rasmi kuingia kwenye kalenda yake, hali aliyosema itavuta hisia za wapenda soka wa bara zima la Afrika.   
  Katika kikao hicho kilichomuhusisha pia Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Tanzania Bara Dkt. Harrison Mwakyembe, ilikubaliwa kuundwe kamati itakayofanya uchambuzi na kuandaa mapendekezo ya namna ya kurejesha na kuendesha michuano ya Kombe la Muungano.
  Pamoja na mambo mengine, uamuzi huo ulizingatia manufaa makubwa yaliyokuwepo wakati wa ligi hiyo katika kudumisha na kuendeleza Muungano sambamba na kuibua wachezaji bora wa timu ya Taifa.
  Aidha, katika dhamira hiyo hiyo ya kuimarisha Muungano, iliazimiwa kuwa mamlaka za uteuzi zishauriwe kuteua wajumbe wa Bodi ya Baraza la Michezo Tanzania (BMT) na Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar (BTMZ), kuwa na mwakilishi katika Bodi zao kutoka taasisi hizo kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizopo.
  Makubaliano mengine ni kuandaliwa bajeti za kuhudumia maandalizi na ushiriki wa timu za Taifa na kuziimarisha, pamoja na kufanyika vikao angalau mara mbili kwa mwaka ili kuzitafutia ufumbuzi changamoto za kimichezo zinazojitokeza.
  Kikao hicho cha kwanza kwa mwaka huu wa 2020 baina ya Wizara ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale, Wizara ya Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo zote za Zanzibar na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Tanzania Bara kilianza Machi 2 hadi 4, katika ukumbi wa ZSSF Kariakoo, kikilenga kukuza ushirikiano baina yao, kwa nia ya kuimarisha Muungano.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: WIZARA ZA MICHEZO ZANZIBAR NA TANZANIA ZAAZIMIA KUREJESHA LIGI YA MUUNGANO ‘KIMAPINDUZI’ Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top