• HABARI MPYA

    Saturday, March 21, 2020

    KARIA ATAHADHARISHA KLABU KUTOWARUHUSU WACHEZAJI NA MAKOCHA WAKE WA KIGENI KUREJEA KWAO

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia amezitahadharisha klabu kutowaruhusu wachezaji, makocha na watendaji wengine wote wa kigeni kurejea nchini kwao kufuatia kusimamishwa kwa Ligi zote nchini baada ya agizo la Serikali kufuatia mlipuko wa virusi vya ugonjwa wa COVID 19.  
    Karia amesema kwamba kuwaruhusu wafanyakazi wa kigeni kurejea kwao kipindi hiki cha mlipuko wa virusi vya corona dunia nzima ni kinyume cha agizo la Serikali na ni hatari zaidi kwa maambukizi.
    “Hatutawaruhusu tena kurudi nchini. Wachezaji wa kigeni watakaokwenda kwenye nchi zao katika kipindi hiki ambacho ligi imesimama, hawataruhusiwa kushiriki ligi ikiwa ni sehemu ya tahadhari dhidi ya Virusi vya Corona,”amesema Karia.
    Mwishoni mwa wiki TFF ilisimamisha ligi zake zote ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kufuatia mlipuko wa virusi vya ugonjwa wa COVID 19 ambao umeingia nchini.  
    Pia TFF ilivunja kambi ya timu ya taifa, Taifa Stars ambayo ilikuwa inajiandaa na fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) zilizopangwa kuanza Aprili 4 hadi 25, mwaka huu nchini Cameroon.
    Ligi Kuu inasimama huku Simba SC wakiwa wanaongoza kwa pointi zao 71, wakifuatiwa na Azam FC pointi 54 baada ya wote kucheza mechi 28, wakati vigogo, Yanga SC ni wa tatu kwa pointi zao 51 za mechi 27 na Namungo wa nne wakiwa na pointi 50 za mechi 28.
    Hali ni mbaya kwa Singida United inayoshika mkia kwa pointi zake 15 za mechi 29, nyuma ya Mbao FC pointi 22 mechi 28, Alliance FC pointi 29, mechi 29, Mbeya City pointi 30 mechi 29 na Ndanda FC pointi 31 mechi 29.
    Jioni ya leo, Waziri Mkuu, Majaliwa ametoa tamko la kusimamisha michezo yote nchini kwa siku 30 ikiwa ni pamoja na kufunga shule zote, kuanzia za mwanzo, Msingi hadi Sekondari Kidato cha sita kutokana na kuingia kwa ugonjwa wa virusi vya COVID 19, maarufu kama Corona.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KARIA ATAHADHARISHA KLABU KUTOWARUHUSU WACHEZAJI NA MAKOCHA WAKE WA KIGENI KUREJEA KWAO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top