• HABARI MPYA

  Ijumaa, Machi 27, 2020

  WAJUMBE WAWILI YANGA SC WAJIUZULU KWA TUHUMA ZA KUUTILIA SHAKA UDHAMINI WA KAMPUNI YA GSM

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  WAJUMBE wawili Kamati ya Utendaji ya Yanga SC, Shijja Richard na Rodgers Gumbo wamejiuzulu wadhifa huo leo, kufuatia tuhuma za kuhusishwa katika orodha ya wajumbe wanne wa klabu wanaodaiwa kuutilia shaka udhamini wa kampuni ya GSM.
  Shijja, Mwandishi wa habari za michezo wa zamani, aliyewahi kugombea Urais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) katika uchaguzi uliopita na kuangushwa na Wallace Karia, amesema kwamba ameamua kwa hiari yake kujiuzulu nafasi zote za uongozi katika klabu yangu ya Yanga. 
  “Yanga ni kubwa kuliko mimi na kuliko mtu yeyote. Yamezungumzwa mengi, lakini mimi sitazungumza chochote. Wakati utaongea. Ukweli hata usipousema, huwa una tabia ya  kujitokeza wenyewe japo taratibu lakini huwa unadumu milele,”amesema Shijja katika taarifa yake.


  Kwa upande wake,  Gumbo katika taarifa yake jioni ya leo amesema; “Nimeamua kwa ridhaa yangu mwenyewe kujiuzulu nafasi zangu zote za uongozi ndani ya Yanga. Yanga ni taasisi kubwa kuliko mimi Gumbo hivyo basi katika kuwajibika kwangu aidha niwe nimefanya au sikufanya kosa nimeamua kukaa pembeni ya Uongozi ili kuiacha Yanga ikiwa salama,”.
  Lakini Gumbo amesema hatazungumza chochote, ila anaamini ipo siku ukweli utajulikana na kwa sasa anabaki kuwa Mwanachama mtiifu kwa Maslahi ya Yanga. 
  Pamoja na kuwa na mkataba wa udhamini wa vifaa vya michezo, kampuni ya GSM imekuwa ikijitolea kufanya mambo zaidi kuisaidia Yanga, lakini inadaiwa baadhi ya Wajumbe akiwemo Shijja, Salum Rupia, Rodgers Gumbo na Frank Kamugisha wanadaiwa kutilia shaka hilo. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: WAJUMBE WAWILI YANGA SC WAJIUZULU KWA TUHUMA ZA KUUTILIA SHAKA UDHAMINI WA KAMPUNI YA GSM Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top