• HABARI MPYA

    Sunday, October 02, 2016

    VURUGU ZA JANA, SERIKALI YAZIFUKUZA SIMBA NA YANGA UWANJA WA TAIFA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    WAZIRI wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Nape Moses Nnauye anatarajiwa kuwa na Mkutano na Waandishi wa Habari Saa 5:00 asubuhi ya leo na kubwa ni kutangaza kuufunga Uwanja wa Taifa kwa mechi za Simba na Yanga na mashindano yote ya ndani kwa ujumla.
    “Nakutana na Waandishi wa habari saa tano kamili Uwanja wa Taifa kwa ajili ya kupitia madhara yaliyotokana na vurugu za uharibifu wa miundo mbinu ya michezo, uwanja wa Taifa,”amesema leo Nape.
    Hatua hiyo inafuatia vurugu zilizofanywa na mashabiki wa Simba jana baada ya Yanga kupata bao la kuongoza lililofungwa na mshambuliaji Mrundi, Amissi Joselyn Tambwe.
    Mashabiki wa Simba SC wakivunja viti jana Uwanja wa Taifa baada ya bao la Tambwe

    Tambwe alifunga bao lake dakika ya 26, akimalizia pasi ndefu ya beki Mbuyu Twite na kugeuka mbele ya beki wa Simba, Novat Lufunga kabla ya kufumua shuti lililomshinda kipa Vincent Angban.
    Bao hilo lilizua kizaazaa, wachezaji wa Simba wakimvaa refa Martin Saanya wakidai mfungaji, Tambwe aliushika mpira kabla ya kufunga.
    Katika vurugu hizo, Saanya akamtoa kwa kadi nyekundu Nahodha wa Simba SC, Jonas Mkude dakika ya 29 kwa sababu ndiye aliyekuwa mstari wa mbele.
    Na mchezo ukasimama kwa takriban dakika tano baada ya mashabiki wa Simba kuanza kufanya vurugu waking’oa viti na kutupa uwanjani.
    Polisi walitumia milipuko ya gesi za kutoa machozi kuwatuliza mashabiki hao na mchezo ukaendelea hadi Simba SC wakasawazisha dakika ya 87 kwa bao la Shizza Kichuya.
    Lakini kutokana na uharibifu mkubwa uliotokea, Waziri Nape anatarajiwa kutoa tamko zito leo.
    Ikumbukwe tayari Uwanja mwingine ambao hutumiwa na Simba na Yanga, wa Uhuru, Dar es Salaam nao umefungwa kwa ukarabati- lakini pia nao ni wa Serikali.
    Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas amesema kwamba baada ya hatua hiyo timu za Dar es Salaam zinatakiwa zitafute viwanja kwa mujibu wa kanuni ya sita ya Ligi Kuu kuanzia kipengele 1-6.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: VURUGU ZA JANA, SERIKALI YAZIFUKUZA SIMBA NA YANGA UWANJA WA TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top