• HABARI MPYA

    Wednesday, November 07, 2012

    KASEJA BADO HASOMEKI SIMBA

    Daniel Akuffo kushoto akimfariji Kaseja Jumamosi mjini Morogoro. Kushoto kabisa na Haruna Chanongo

    Na Mahmoud Zubeiry
    NAHODHA wa Simba, Juma Kaseja kwa siku ya pili mfululizo leo hajafika kwenye mazoezi ya timu yake inayojiandaa na mchezo wa mwisho wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, utakaopigwa Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, huku kukiwa kuna habari ameamua kuachana na timu hiyo.
    Mazoezi ya Simba yanaendelea kwenye Uwanja wa Kinesi, Urafiki, Dar es Salaam jioni hii, lakini Kaseja hayupo na Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga amesema wanaendelea kumpa nafasi kwa kuwa wanafahamu yupo katika wakati mgumu kwa sasa, baada ya fujo alizofanyiwa na mashabiki Jumamosi Morogoro.
    Jana ilielezwa kwamba Kaseja amewaaga wachezaji wenzake na kuwaambia yeye na klabu hiyo basi.
    BIN ZUBEIRY ilifika kwenye mazoezi ya Simba jioni ya jana Uwanja wa Kinesi na kukuta wachezaji wote wakiendelea na mazoezi kujiandaa na mechi ya Toto, kasoro Kaseja na Amir Maftah.
    Alipoulizwa Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema kwamba Maftah ana ruhusa maalum kwa sababu ameoa hivi karibuni, lakini Kaseja hawana taarifa zake, ila; “Nadhani hatakuwa vizuri kisaikolojia baada ya kufanyiwa fujo Jumamosi,”alisema Kamwaga.
    Lakini BIN ZUBEIRY ilipozungumza na wachezaji wenzake, walisema Nahodha wao amewaaga kwamba yeye na Simba basi, kwani ameumia sana kwa jinsi alivyodhalilishwa na mashabiki Jumamosi Morogoro.
    “Juma hapa ndio basi kaka, Kasema yeye na Simba basi, amesononeshwa mno na jinsi alivyodhalilishwa baada ya mechi ya Morogoro,”alisema mchezaji mmoja wa Simba baada ya mazoezi Kinesi leo.
    Kaseja alitukanwa na kutishiwa maisha na mashabiki wa Simba baada ya mechi dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro wakimtuhumu kufungwa mabao ya kizembe.
    Lakini tayari uongozi wa Simba umelaani vikali vurugu na vitisho alivyotolewa kipa wao huyo namba moja,  na kusema wanafikiria kuwachukulia hatua kali watu waliomfanyia hivyo Nahodha wao huyo.
    Juhudi za kumpata Kaseja mwenyewe kuzungumzia suala hilo, hazikuweza kufanikiwa kwani simu yake ilikuwa haipatikani.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: KASEJA BADO HASOMEKI SIMBA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top