• HABARI MPYA

    Thursday, April 06, 2017

    MKWASA AWASIHI WACHEZAJI YANGA WAWE WAVUMILIVU

    Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
    KATIBU wa Yanga, Charles Bonifce Mkwasa amewasihi wachezaji wa timu hiyo wawe wavumilivu katika kipindi hiki kigumu, wakati viongozi wanahangaika kuweka mambo sawa.
    Mkwasa ameyasema hayo jana usiku akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online kwa simu kutoka Morogoro, kufuatia kuwapo taarifa za wachezaji kutaka kugoma kwa sababu ya madai ya mishahara yao.
    Mkwasa alisema kwamba iwapo wachezaji watagoma wakati klabu inakabiliwa na mchezo mgumu dhidi ya MC Alger ya Algeria Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam watakosea sana.
    Kuweni wavumilivu; Wachezaji wa Yanga wametakiwa kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kigumu
    Alikiri hali bado ngumu kifedha klabuni kufuatia, matatizo yanayomkabili Mwenyekiti wao, Yussuf Manji ambaye pia ndiye mdhamini, lakini uongozi unafanya jitihada za dhati kuhakikisha mambo yanakaa sawa.
    “Nipo nje kidogo ya Dar es Salaam, nipo Morogoro msibani kwa kaka yangu. Kwa kweli kama wataamua kugoma kisa mshahara wa mwezi mmoja na malimbikizo ya deni lao la nyuma, binafsi watanisikitisha sana,”alisema.
    Mkwasa alisema mikakati mingi ya ukusanyaji fedha za kuendesha timu inafanyika wakati huu, ikiwemo kwa njia ya wanachama kuchangishana, kuomba misaada na kudai malimbikizo ya fedha zao za haki za matangazo ya Televisheni kutoka Bodi ya Ligi.
    “Tumeshaandaa mchakato wa kufanya harambee ya kuichangia klabu yetu pia kuna fedha tunasubiri ambazo zimeshikiliwa na Bodi ya Ligi, hizo fedha zikitoka basi tumekusudia kuwalipa haraka,”amesema kiungo huyo wa zamani wa timu hiyo ya Jangwani.
    Mkwasa amewasihi wachezaji wa Yanga kuwa wavimulivu kidogo katika kipindi hiki kigumu, kwani muda si mrefu hali itakaa sawa.
    Kiingilio cha chini katika mchezo wa kwanza wa mchujo wa kuwania kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika kati ya wenyeji, Yanga na MC Alger ya Algeria kitakuwa cha Sh. 5,000.
    Mchezo unatarajiwa kufanyika Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na viingilio vingine vitakuwa Sh. 20,000 kwa VIP B na C na 30,000 kwa VIP A.   
    Marefa wa mchezo huo pamoja na wapinzani wao, MCAlger wote wanatarajiwa kuwasili kuanzia leo mchana mjini Dar es Salaam.
    Mchezo wa Aprili 8 utachezeshwa na Louis Hakizimana atakayepuliza filimbi akisaidiwa na Theogene Ndagijimana na Jean Bosco Niyitegeka wote kutoka Rwanda, wakati mchezo wa marudiano Aprili 14 nchini Algeria utachezeshwa na marefa wa Guinea, ambao ni Yakhouba Keita, Aboubacar Doumbouya na Mamady Tere na mshindi wa jumla atafuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika mwaka huu.
    Mwaka jana pia Yanga ilitolewa katika Ligi ya Mabingwa na kuangukia kwenye kapu la kuwania hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho ambako ilifuzu baada ya kuitoa Sagrada Esperanca ya Angola. 
    Yanga SC imeangukia Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kutolewa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa baada ya sare ya 0-0 na wenyeji, Zanaco Uwanja wa Taifa wa Mashujaa, Lusaka nchini Zambia ikitoka kulazimishwa sare ya 1-1 kwenye mchezo wa kwanza Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MKWASA AWASIHI WACHEZAJI YANGA WAWE WAVUMILIVU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top