• HABARI MPYA

    Sunday, November 06, 2016

    BINGWA KOMBE LA SHIRIKISHO KUPATWA LEO

    BINGWA wa Kombe la Shirikisho Afrika anatarajiwa kupatana jioni ya leo baada ya mchezo wa fainali utakaofanyika Uwanja wa Mazembe mjini Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
    Huo utakuwa mchezo wa marudiano baada ya Mouloudia Olympique Bejaia kulazimishwa sare ya kufungana 1-1 na Tout Puissant Mazembe ya DRC katika mchezo wa kwanza Jumamosi iliyopita  Uwanja wa Mustapha Tchaker mjini Blida, Algeria. 
    Kocha wa TP Mazembe, Hubert Velud hakubaliani na timu yake kupewa nafasi kubwa ya kuwafunga Mouloudia Olympique Bejaia katika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
    Mzaliwa wa Ufaransa, Velud hakubali kwamba Mazembe kushinda mataji tisa ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na Bejaia kuwa wanawania taji lao la kwanza mwaka huu kuna nafasi yoyote katika mchuano wao.
    Utabiri wake unatokana na mechi tatu za awali zikiwemo mbili za Kundi A zilizowakutanisha na Bejaia, ya kwanza ikimaliza kwa sare ya bila mabao na ya pili Mazembe wakishinda kwa mbinde 1-0 nyumbani, bao pekee la Rainford Kalaba na wiki iliyopita sare ya 1-1.
    "Fainali ni mchuano wa 50-50," amesema kocha huyo mwenye uzoefu mkubwa na klabu za Algeria na kuongeza. 
    “Mouloudia wamethibitisha ubora wao, na sishangai wamefuzu kuingia fainali ya Kombe la Shirikisho,".
    Mazembe, ambayo mataji yae tisa ya CAF iliyoshinda ni pamoja na Ligi ya Mabingwa, kikosi chake kinaundwa na nyota kutoka nchi tofauti barani Afrika zikiwemo DRC, Ghana, Ivory Coast, Mali na Zambia. 
    Miongoni mwao ni mchawi wa chenga wa Zambia na Nahodha, winga Kalaba, ambaye msimu huu amefunga mabao sita katika Kombe la Shirikisho, hivyo kuongoza kwa ufungaji kwa pamoja na Arsenio 'Love' Cabungula, ambaye klabu yake ya Angola ilitolewa katika mchujo.
    Kocha wa Bejaia na beki wa zamani wa Algeria, Nacer Sandjak amesema amefurahi kukutana na washindi wa pili wa mwaka 2013, Mazembe kuliko mabingwa wa 2015, Etoile Sahel kwenye fainali.   
    “Ikiwa ningetakiwa kuchagua baina ya timu hizo mbili, ningechagua kucheza na klabu ya Kongo kwa sababu Watunisia ni wagumu kukabiliana nao,” alisema.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BINGWA KOMBE LA SHIRIKISHO KUPATWA LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top