• HABARI MPYA

    Tuesday, October 11, 2016

    TFF YASEMA HAITAMBUI YANGA KUKODISHWA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limesema kwamba halitambui mabadiliko ya umiliki wa klabu ya Yanga SC licha ya kuwepo kwa taarifa za klabu hiyo kukodishwa na kampuni ya Yanga Yetu.
    Akizungumza na Waandishi wa Habari leo, Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa amesema kwamba pamoja na hayo wanalifanyia kazi suala la klabu kukodishwa na Yanga Yetu.
    Mwesigwa amesema kwamba wameuandikia barua uongozi wa Yanga kuuomba Mkataba wa ukodishwaji wa klabu hiyo pamoja na nyaraka nyingine muhimu zenye kuonyesha mchakato ulipoanzia hadi kufika hatua hiyo.
    Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa (katikati) akizungumza na Waandishi wa Habari leo

    Mwesigwa amesema hatua hiyo imefuatia mazungumzo ya awali baina ya TFF na sekretarieti ya Yanga kuomba ufafanuzi wa kinachoendelea kwenye klabu hiyo, ambayo hata hvyo hayakufanikiwa. “Katibu wa Yanga alituambia tuwasiliane Baraza la Wazee na kwa kawaida, sisi (TFF) tunawasiliana na uongozi na si Baraza la Wazee,”amesema Mwesigwa.
    Amesema wao TFF kwa mwongozo wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) wanapaswa kumjua mmiliki halisi wa Yanga kwa mujibu wa sharia ili waweze kujua pia wajibu wa kila mmoja katika masuala mbalimbali ya klabu. 
    “Tumewaandikia barua Yanga ili watufahamishe, kama kuna tatizo tulishughulikie. Kwanza ni muhimu taratibu za ndani zifuatwe ikiwemo kufahamishana nani ni nani kwa sasa Yanga na pia ni wajibu wetu kuhakikisha klabu inakuwa kwenye mikono salama,”amesema.
    Tayari Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kupitia kwa Katibu wake, Mohammed Kiganja limesema halitambui klabu ya Yanga SC kukodishwa kwa kampuni ya Yanga Yetu, kwa kuwa taratibu haazikufuatwa na Baraza la Wadhamini la klabu hiyo halitambuliki. 
    Kiganja alisema wiki iliyopita kati ya Wajumbe wa Baraza la Wadhamini la Yanga lililoundwa Julai 5, mwaka 1973 ni wawili tu wanaotambulika na walio hai hadi sasa, ambao ni Dk. Jabir Idrisa Katundu na Juma Mwambelo, ambaye kwa sasa hajihusishi na masuala ya klabu hiyo, wakati wengine wamekwishafariki dunia. 
    Alisema ili Yanga ikodishwe, inatakiwa kwanza kifanyike kikao cha Kamati ya Utendaji itakayochambua hoja na kukubaliana au kutokukubaliana kabla ya kwenda kwenye Mkutano Mkuu wa wanachama, uwe wa dharura au kawaida na maamuzi yatakayofikiwa katika Mkutano yatapelekwa Baraza la Wadhamini, ambalo ndilo litawasilisha suala hilo kwa Msajili.
    Alisema sheria ya BMT ya mwaka 1967 kifungu namba 11 (1) inasema chama chochote kinachofanya mabadiliko ya jina, anuani, madhumuni au kifungu chochote cha Katiba yake kitatakiwa kiidhinishwe ya Msajili wakati Kifungu namba 11 (3) Msajili anaweza kuyakataa maombi ya kubadili kifungu chochote cha Katiba kama ataona kuwa mabadiliko yanaweza kuhatarisha usalama na kuvuruga amani, au kama kuna malengo ya kuwanufaisha wachache au kama hayazingatii sera za michezo na sheria za BMT.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TFF YASEMA HAITAMBUI YANGA KUKODISHWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top