• HABARI MPYA

  Wednesday, October 05, 2016

  KILA KLABU IBEBE MSALABA WAKE, LAKINI SIMBA NA YANGA ZIENDELEE KUCHEZA UWANJA WA TAIFA

  KWA mujibu Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Nape Moses Nnauye – Rais Dk John Pombe Magufuli alikasirishwa na vurugu zilizotokea Jumamosi wakati wa mchezo wa watani, Simba na Yanga.
  Nape alizungumza na Waandishi wa Habari Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam siku moja tu baada ya mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baina ya mahasimu hao wa jadi kwenye Uwanja huo huo.
  Mashabiki wa Simba Jumamosi walifanya vurugu Uwanja wa Taifa baada ya Yanga kupata bao la kuongoza lililofungwa na mshambuliaji Mrundi, Amissi Joselyn Tambwe katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
  Tambwe alifunga bao lake dakika ya 26, akimalizia pasi ndefu ya beki Mbuyu Twite na kugeuka mbele ya beki wa Simba, Novat Lufunga kabla ya kufumua shuti lililomshinda kipa Vincent Angban.
  Bao hilo lilizua kizaazaa, wachezaji wa Simba wakimvaa refa Martin Saanya wakidai mfungaji, Tambwe aliushika mpira kabla ya kufunga.
  Katika vurugu hizo, Saanya alimtoa kwa kadi nyekundu Nahodha wa Simba SC, Jonas Mkude dakika ya 29 kwa sababu ndiye aliyekuwa mstari wa mbele.
  Na mchezo ukasimama kwa takriban dakika tano baada ya mashabiki wa Simba kuanza kufanya vurugu waking’oa viti na kutupa uwanjani.
  Polisi walitumia milipuko ya gesi za kutoa machozi kuwatuliza mashabiki hao na mchezo ukaendelea hadi Simba SC wakasawazisha dakika ya 87 kwa bao la Shizza Kichuya.
  Na Jumapili Nape akasema Rais Magufuli alikuwa anautazama mchezo huo moja kwa moja kupitia Azam TV na akajionea mwenyewe vurugu na chanzo chake.
  Nape akasema Rais Magufuli alikasirika mno na akataka hatua kali zichukuliwe, lakini akamtuliza na mwishowe hatua iliyochukuliwa ni kuzizuia timu hizo kutumia Uwanja huo.  
  Aidha, Serikali pia imezuia mapato ya mchezo huo hadi hapo itakapokata gharama za uharibifu uliosababishwa na vurugu hizo. 
  Nape alisema kwamba mbali na uvunjwaji wa viti, pia mageti mawili ya kuingilia, moja la upande wa Yanga na lingine wa Simba yalivunjwa.
  Awali ya hapo, Kaimu Mkurugenzi wa Michezo, Alex Nkenyenge alisema kwamba zaidi ya viti 1781 vilivunjwa jana, wakati kati ya Sh. Milioni 350 na 400 zikikusanywa katika mchezo huo, ambao mashabiki waliingia kwa tiketi za Elektroniki.
  Iko wazi, mashabiki wa Simba ndiyo waliofanya uharibifu uwanjani na vurugu zilizosababisha mageti kuvunjika tukubali zilitokana na kero za ugeni wa matumizi ya tiketi za Elektroniki.  
  Na ukirejea kwenye adhabu iliyotolewa na Serikali, kuzizuia Simba na Yanga kutumia Uwanja wa Taifa – binafsi naona si sahihi kwa sababu kila kitu siku ile kilitokea kwa sababu na kila sababu ni ya kibinadamu.
  Refa Saanya aliyeruhusu bao la mkono la Tambwe, alifanya kosa la kibinadamu – ambalo hapana shaka sasa anajutia.
  Wachezaji wa Simba wakaamsha hasira za mashabiki wao kwa kwenda kumzonga refa, badala ya kupeleka mpira kufuatia bao hilo na kusababisha vurugu hadi uvunjwaji wa viti.
  Wachezaji wa Simba walifanya kosa la kibinadamu hapa – na mashabiki wao nao wakafanya kosa la kibinadamu pia.
  Tuchukulie hata hatua kali iliyochukuliwa na Serikali dhidi ya Simba na Yanga ni ya kibinadamu pia – ambayo msingi wake ni kosa la kibinadamu la refa Martin Saanya.
  Na hapo ndipo unapoonekana umuhimu mwingine wa kufanya jambo lingine la kibinadamu; Kusameheana. Na si kusameheana tu, bali kutoa adhabu nyingine lakini si kuzuia matumizi ya Uwanja.
  Kila klabu ibebe msalaba wake. Simba walipe gharama na viti na uharibifu mwingine wote waliofanya ikiwemo geti – pamoja na faini. Yanga kadhalika walipe gharama za geti na nyingine kama zipo.
  Uwanja wa Taifa umejengwa kwa ajili ya matumizi ya kimichezo na Simba na Yanga ndiyo vitu vikubwa vinavyoweza kuvutia watu wengi wa kuupendezesha Uwanja – tunazifungia ili iweje?
  Vurugu za kimichezo zinatokea kote duniani na hivi karibuni tulishuhudia mitafaruku ya aina hiyo katika fainali za Euro 2016 nchini Ufaransa, lakini hakuna Uwanja wala timu iliyofungiwa.
  Adhabu kubwa ambazo huchukuliwa na bodi kubwa za soka ni timu kucheza bila mashabiki iwapo mashabiki wake watafanya vurugu za athari kubwa.
  Tuwapongeze askari wetu wa Jeshi la Polisi nchini walifanya kazi yao vizuri kuzuia munkari wa mashabiki wa Simba uzisababishe athari kubwa zaidi ya ung’olewaji wa viti.  
  Ninaona adhabu ya kuzizuia Simba na Yanga kutumia Uwanja wa Taifa ni kubwa sana na ambayo imelenga kukomoa zaidi na si kufundisha. 
  Bora kila klabu ibebe msalaba wake, kwa kulipa gharama za uharibifu iliyofanya na faini juu – lakini ziendelee kucheza Taifa.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KILA KLABU IBEBE MSALABA WAKE, LAKINI SIMBA NA YANGA ZIENDELEE KUCHEZA UWANJA WA TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top