• HABARI MPYA

    Saturday, October 08, 2016

    BARAZA LA WAZEE YANGA LAMJIBU KIGANJA, LASEMA LILIFUATA TARATIBU KUMPA TIMU MANJI

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    BARAZA la Wadhamini la Yanga SC, limesema kwamba kabla ya kufikia uamuzi wa kuikodisha timu kwa kampuni ya Yanga Yetu, inayomilikiwa na Mwenyekiti wa klabu hiyo, Yussuf Manji liliomba msaada wa kisheria kutoka kwa magwiji wa sheria nchini.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE leo Dar es Salaam, Mjumbe wa Baraza la Wadhamini la Yanga, Francis Mponojoli Kifukwe amesema kwamba baada ya kuandaa muswada wa kukodisha timu kwa pamoja na wakodishwaji, waliupeleka kwa wanachama wao ambao magwiji wa sheria nchini kuomba msaada wa kisheria.
    Kifukwe amewataja magwiji hao kuwa ni Profesa Mgongo Fimbo, Jaji John Mkwawa na Alex Mgongolwa ambaoe wote waliuafiki muswada huo na kuusifia, kwamba ni nafasi adimu klabu inapata.
    Francis Kifukwe (katikati) akiwa na Seif Magari (kulia) na Abdallah Bin Kleb (kushoto) 
    “Baada ya kupata msaada huo wa mawazo ya kisheria kutoka kwa magwiji hao wa Sheria, tukajiridhisha na kwa kuwa taratibu zilikwishafutwa tukaafiki huo mpango na kuuupitisha,”amesema Kifukwe.
    Kuhusu madai ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kwamba Baraza la Wadhamini liliopitosha mpango huo halitambuliwi, Kifukwe amesema si kweli.
    “Kwanza huyo mtu anayetajwa Juma Mwambelo, hajawahi kuwa Mjumbe wa Baraza la Wadhamini la Yanga. Baada ya Baraza la Wadhamini wa zamani wa klabu wengi wao kufariki dunia, liliundwa Baraza lingine na BMT ilishirikishwa, ambalo ndilo tumo ndani yake,”amesema.
    Kifukwe, Rais wa zamani wa Yanga SC, amewataja Wajumbe wanaounda Baraza hilo mbali ya yeye, wengine ni Kapteni Mstaafu, George Mkuchika, Mama Fatuma Karume, Amri Ramadhan, Juma Kambi na Abeid Mohammed.
    Na kuhusu madai ya Baraza la Wadhamini kuikodisha timu ya soka kwa Yanga Yetu bila ridhaa ya BMT, Kifukwe alisema; “Maamuzi ya wanachama hayahitaji Baraka za BMT, sana kama kuna mapungufu wameyaona wauandikie uongozi kuuelekeza cha kufanya,”.
    Kifukwe amesema kwa upande wake hana shaka kabisa na mpango huo wa kuikodisha timu utakuwa wenye manufaa na taratibu zilifuatwa kwa sababu maazimio yalifikiwa katika Mkutano wa Agosti 6 na Baraza la Wadhamini limekuja kuyapitisha.
    Juzi Katibu wa BMT, Mohammed Kiganja alisema hawatambui klabu ya Yanga SC kukodishwa kwa kampuni ya Yanga Yetu, kwa kuwa taratibu haazikufuatwa na Baraza la Wadhamini la klabu hiyo halitambuliki. 
    Alisema kati ya Wajumbe wa Baraza la Wadhamini la Yanga lililoundwa Julai 5, mwaka 1973 ni wawili tu wanaotambulika na walio hai hadi sasa, ambao ni Dk. Jabir Idrisa Katundu na Juma Mwambelo, wakati wengine wamekwishafariki dunia. 
    “Mwembelo pamoja na kwamba bado yupo hai, lakini kwa muda sasa hahusishwi tena mambo yanayoendelea ya klabu hiyo,” alisema.
    Alisema ili Yanga ikodishwe, inatakiwa kwanza kifanyike kikao cha Kamati ya Utendaji itakayochambua hoja na kukubaliana au kutokukubaliana kabla ya kwenda kwenye Mkutano Mkuu wa wanachama, uwe wa dharura au kawaida na maamuzi yatakayofikiwa katika Mkutano yatapelekwa Baraza la Wadhamini, ambalo ndilo litawasilisha suala hilo kwa Msajili.
    “Sheria ya BMT ya mwaka 1967 kifungu namba 11 (1) kinasema chama chochote kinachofanya mabadiliko ya jina, anuani, madhumuni au kifungu chochote cha katiba yake kitatakiwa idhini ya Msajili. Kifungu namba 11 (3) Msajili anaweza kuyakataa maombi ya kubadili kifungu chochote cha Katiba kama ataona kuwa mabadiliko yanaweza kuhatarisha usalama na kuvuruga amani, au kama kuna malengo ya kuwanufaisha wachache au kama hayazingatii sera za michezo na sheria za BMT,” alisema Kiganja.
    Katibu huyo wa BMT alisema kwamba mchakato huo wa Yanga kukodishwa ungekuwa halali tu kama taratibu hizo zingefuatwa na kupita kote.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BARAZA LA WAZEE YANGA LAMJIBU KIGANJA, LASEMA LILIFUATA TARATIBU KUMPA TIMU MANJI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top