• HABARI MPYA

  Sunday, October 20, 2013

  MDOGO WAKE MSUVA NI NOMA, APIGA MBILI ZOTE BARUTI FC IKIBEBA KOMBE NA MAMILIONI YA DK FENELLA MUKANGARA

  Na Mahmoud Zubeiry, Ubungo
  MICHUANO ya Kombe la Umoja na Amani, iliyoandaliwa na Waziri wa Habari Vijana Utamaduni na Michezo, Dk Fenella Mukangara imefikia tamati jana kwenye Uwanja wa shule ya Msingi Ubungo Msewe kwa timu ya Baruti FC kuibuka mabingwa, baada ya kuwafunga Kimara United mabao 2-0 katika fainali.
  Shujaa wa Baruti FC alikuwa ni James Msuva, mdogo wa mshambuliaji wa Yanga SC, Simon Msuva aliyefunga mabao yote hayo kipindi cha pili katika fainali kali na ya kusisimua iliyoshuhudiwa na Dk Fenella mwenyewe aliyekuwa mgeni rasmi.
  James Msuva akiwa amebebwa juu na wachezaji wenzake baada ya fainali ya Kombe la Umoja na Amani jana Uwanja wa shule ya Msingi Ubungo Msewe, ambayo alifunga mabao yote mawili katika ushindi wa 2-0.

  Kinda huyo wa umri wa miaka 16, aliyehitimu kidato cha Nne alifunga bao la kwanza dakika ya 75 kwa shuti la nje kidogo ya eneo la mita 18 baada ya kutanguliziwa pasi na Abubakar Kambi.
  Msuva ambaye pamoja na kuchezea timu ya mtaani kwake ya Baruti FC pia yupo katika akademi ya Wakati Ujao, alifunga bao la pili kutokana na juhudi za Kambi aliyepiga shuti lililodunda na kumchanganya kipa kabla ya mdogo huyo wa winga wa Yanga kuupitia mpira na kuutumbukiza nyavuni.
  Nahoda wa Baruti FC, Ibrahim Mpepo akiwa ameinua juu Kombe la Umoja na Amani jana, huku kipa Arafat Kantimbo kulia akiwa ameshika jezi. Kushoto kwake ni Dk Fenella na Juma Simba Katibu Mwenezi wa CCM Dar es Salaam.


  Dk Fenella akimkabidhi jezi Nahodha wa Barurti FC

  Dk Fenella akimkabidhi fedha taslimu Sh. 200,000 mfungaji bora wa mashindano hayo, James Msuva 

  Ulikuwa mchezo mkali uliovuta mashabiki wengi uwanjani, wa rika tofauti na jinsia zote pia, ambao kwa hakika walifurahishwa na kile kilichofanya na Dk Fenella- kuandaa mashindano hayo.
  Vijana wadogo walicheza soka ya kuvutia kana kwamba wanafundishwa na walimu waliobobea, kumbe ni makocha wa mtaani tu wasio na mafunzo ya kitaaluma.
  Pamoja na kufungwa, Kimara United ilionyesha upinzani na ndiyo iliyocheza vema zaidi kipindi cha kwanza, kabla ya kuja ‘kutepeta’ dakika 20 za mwisho na kuwaachia Kombe wapinzani wao.
  Pamoja na kuwa shujaa wa fainali, Msuva mdogo pia ameibuka mfungaji bora wa mashindano hayo kwa kufikisha jumla ya mabao saba na kuzawadiwa jumla ya Sh. 200,000, wakati mabingwa Baruti FC wamepewa Kombe, Sh. Milioni 2 na seti ya jezi.
  James Msuva wa pili kushoto akikimbia kushangilia na wenzake baada ya kufunga bao la pili


  Beki wa Baruti FC akipambana na mshambuliaji wa Kimara United

  Kipa wa Kimara United, Saleh Malande akipangua mchomo mkali

  Mshambuliaji wa Baruti FC akimtka beki wa Kimara United

  James Msuva akimtoka beki wa Kimara United

  Beki wa Kimara United kulia akimchezea rafu James Msuva

  Beki wa Kimara United akimpelekea guu mchezaji wa Baruti FC

  Beki wa Baruti FC akimdhibiti mshambuliaji wa Kimara United

  Mabingwa wakiwa katika picha ya pamoja na mgeni rasmi, Dk Fenella aliyeshika Kombe 

  Kikosi cha Kimara United katika picha ya pamoja na Dk Fenella kabla ya mechi

  Nahodha wa Kimara United, Saleh Malande kula akimtambulisha Dk Fenella kwa wachezaji wa timu hiyo kabla ya mechi

  Mashabiki walikuwa wengi na walijawa mizuka

  Washindi wa pili, Kimara United wamepewa Sh. Milioni 1, seti ya jezi na mipira miwili na washindi wa tatu katika mashindano hayo yaliyoshirikisha timu 32 za Manispaa ya Kinondoni, wamepewa Sh. 500,000 na mipira miwili.    
  Kikosi cha Baruti FC kilikuwa; Arafat Kantimbo, Abdallah Saleh, Nassor Ramadhani, Doto Odhiambo/Joseph Julius dk68/Alex Jackson dk85, Ibrahim Mpepo, Jerome Mayuni, Joseph Mapeche, Abubakar Kambi, Charles Msalaka, James Msuva na Ahmed Ally/Joseph Malipesa dk46.
  Kimara United; Saleh Malande, Martin Raymond/Robert Jacob dk64, Gabriel Peter, Frank Haule, Isaya Hebron, Athumani Yakoub/Hamisi Jonas dk46, Kelvin Herrod, Salum Bawazir, Abdallah Shauri/Suleiman Shaaban dk83, Malik Dalhi na Iddi Suleiman.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MDOGO WAKE MSUVA NI NOMA, APIGA MBILI ZOTE BARUTI FC IKIBEBA KOMBE NA MAMILIONI YA DK FENELLA MUKANGARA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top