![]() |
| MABINGWA; Yanga walipotwaa Kombe la Kagame mwezi uliopita |
Na Mahmoud Zubeiry
YANGA inaondoka leo saa
10:00 jioni kwenda Kigali, Rwanda kuweka kambi ya kujiandaa na msimu mpya wa
Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Kocha Mkuu wa Yanga,
Mbelgiji Tom Saintfiet ameiambia BIN ZUBEIRY asubuhi ya leo, kwamba
kikosi kizima kinakwenda Kigali, hadi wachezaji majeruhi Salum Telela na Said
Bahanuzi.
Kuhusu beki wa
kimataifa wa Rwanda, Mbuyu Twite mwenye asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Kongo (DRC), Mtakatifu Tom alisema atajiunga na timu Kigali. Kwa sasa, Mbuyu
yupo nyumbani kwao kwa asili, DRC kwa mapumziko mafupi kabla ya kuja kuanza
maisha mapya Jangwani.
Kikosi kamili cha Yanga
ni; Makipa; Yaw Berko, Ally Mustafa
‘Barthez’ na Said Mohamed.
Mabeki; Shadrack Nsajigwa (Nahodha), Godfrey Taita,
Juma Abdul, Oscar Joshua, David Luhende na Stephano Mwasika, Nadir Haroub
‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Mbuyu Twite, Ibrahim Job na Ladislaus Mbogo.
Viungo; Athuman Idd ‘Chuji’, Juma Seif ‘Kijiko’ na
Salum Telela, Nizar Khalfan, Shamte Ally, Idrisa Rashid, Omega Seme, Haruna
Niyonzima, Rashid Gumbo na Nurdin Bakari.
Washambuliaji; Said Bhanaunzi ‘Spider Man’, Hamisi
Kiiza ‘Diego’, Didier Kavambagu na Jerry Tegete.
Kiungo Frank Domayo na mshambuliaji Simon Msuva,
wanaendelea kukomazwa katika kikosi cha kwanza, wakitokea kikosi cha pili. Awali
Yanga ilikuwa icheze na Coastal Union, lakini mechi hiyo imefutwa.
Akiwa anaingia mwezi wa
pili tangu aanze kazi Yanga, tayari Tom amekwishaweka Kombe moja kwenye kabati
la mataji la Yanga, ambalo ni la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe
la Kagame.
Yanga ilitwaa Kombe la
Kagame kwa mara ya pili mfululizo wiki mbili zilizopita, Uwanja wa Taifa, Dar
es Salaam kwa kuifunga Azam FC mabao 2-0, ambayo yalitiwa kimiani na Hamisi
Kiiza ‘Diego Milito’ na Said Bahanuzi ‘Spider Man’.
Hiyo kwa ujumla ilikuwa
mara ya tano mfululizo, Yanga inatwaa Kombe hilo, baada ya awali kuchukua mwaka
jana, wakiifunga Simba katika fainali bao 1-0, Uwanja wa Taifa mfungaji Kenneth
Asamoah ambaye ametemwa, ingawa siku hiyo Kiiza pia alifunga bao safi, ambalo
refa alilikataa.
Yanga ilichukua kwa
mara ya kwanza Kombe hilo, mwaka 1975 ikiifunga tena Simba katika fainali,
mabao 2-0 wafungaji Sunday Manara ‘Computer’ na Gibson Sembuli (sasa marehemu)
Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Ikachukua tena mwaka
1993, Uwanja wa Nakivubo, Kampala, Uganda kwa kuifunga SC Villa mabao 2-1,
yaliyotiwa kimiani na Said Nassor Mwamba ‘Kizota’ (sasa marehemu) na Edibily
Jonas Lunyamila.
Ilichukua tena mwaka
1999, ikiifunga tena SC Villa, Uwanja wa Nakivubo, kwa penalti 5-3, kufuatia
sare ya 1-1 ndani ya dakika 120, Yanga ikisawazisha bao kupitia kwa Lunyamila,
baada ya Hassan Mubiru kutangulia kuifungia Villa, siku hiyo Manyika Peter
akicheza penalti mbili za Waganda.
Aidha, kwa kutwaa Kombe
hilo chini ya Mbelgiji huyo, Yanga imeendeleza rekodi yake ya kutwaa mataji ya
michuano hiyo, chini ya makocha wa kigeni baada ya mwaka 1975 kuchukua chini ya
Tambwe Leya aliyekuwa raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kabla ya
kuchukua uraia wa Tanzania, (sasa marehemu), 1993 chini ya Nzoyisaba Tauzany
aliyekuwa raia wa Burundi kabla ya kuchukua uraia wa Tanzania, mwaka 1999 chini
ya Raoul Shungu wa DRC na mwaka jana chini ya Mganda, Sam Timbe.



.png)
0 comments:
Post a Comment