• HABARI MPYA

    Wednesday, August 15, 2012

    COASTAL UNION WANAKIPIGA KENYA NA AKINA BANKA

    Wachezaji wa Coastal Union

    Na Princess Asia
    MABINGWA wa zamani wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Coastal Union ya Tanga leo watashuka dimbani kwenye Uwanja wa Mbarak Sports kumenyana na Bandari ya huko, inayoundwa na wachezaji kibao wa Tanzania.
    David Naftali
    Beki wa Bandari inayopigania kurejea Ligi Kuu ya Kenya kutoka Daraja la Kwanza, David Naftali ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwa simu kutoka Mombasa kwamba wanatarajiwa mchezo huo utakuwa mzuri kwa sababu Coastal Union imesajili vizuri na wao (Bandari) timu yao nzuri pia.  
    Bandari yenye nyota wengine wa Tanzania, zaidi ya Naftali kama Meshack Abel, kiungo Mohamed Banka na mshambuliaji Thomas Maurice, kwa sasa inaongoza ligi hiyo kwa pointi zake 44, ikifuiatiwa na Kariobang Sharks yenye pointi 40.
    Coastal Union inayojivunia ufadhili wa Bin Slum na Simba Cement, imepania kufanya vizuri msimu ujao, ili kukumbushia enzi zile ikitikisa katika soka ya Tanzania miaka ya 1980 na 1990, kabla ‘haijafulia’.  
    Mfadhili Mkuu wa Coastal Union, Nassor Bin Slum aliiambia BIN ZUBEIRY wiki iliyopita, kwamba Wagosi hao wa Kaya watakuwa tishio katika msimu ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kutokana na usajili mzuri waliofanya.
    Nassor ambaye pia ni mfadhili wa Villa Squad ya Kinondoni, alisema kwamba uongozi wa Coastal ulikuwa makini na wenye utulivu wa hali ya juu katika zoezi la usajili, kuhakikisha kwamba wanasajili wachezaji watakaorejesha hadhi ya timu hiyo, iliyokuwa tishio siku za mwanzoni za soka ya Tanzania.
    “Mchezaji kama Razack Khalfan, huyu ni bora kabisa mwenye kiwango cha kucheza timu ya taifa, huwezi kupata sababu kwa nini Yanga walimuacha, ila msimu ujao watamuona. Bado kuna wanaume wengine wa shoka kibao tumesajili, kwa kweli msimu ujao tutatisha,”alisema Nassor.
    Mabingwa hao wa 1988, tayari wamekamilisha usajili wa msimu ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na wametaja kikosi chao, kupitia facebook page yao.
    Kikosi cha Coastal msimu kitaundwa na makipa; Juma Mpongo, Abraham Chove na Rajab Kaumba, mabeki; Said Sued (Nahodha) Mbwana Kibacha (Nahodha Msaidizi) Othman Omary, Juma Jabu, Ismail Suma, Jamal Machelenga, Cyprian Lukindo na Philipp Mugenzi.
    Viungo watakuwa ni Jerry Santo, Razack Khalfan, Mohamed Binslum, Khamis Shango, Mohamed Issa, Mohamed Soud, Suleiman Kassim ‘Selembe’, Lameck Dayton, Joseph Mahundi, Aziz Gilla na Shaffih Kaluani, wakati washambuliaji ni Nsa Job, Atupele Green, Danny Lianga na Pius Kisambale.
    Kikosi hicho kitakuwa chini ya Kocha Mkuu, mshambuliaji wake wa zamani, Juma Mgunda, atakayekuwa akisaidiwa na beki wa zamani wa Pan African, Habibu Kondo, kocha wa viungo, mchezaji wake wa zamani, Ally Jangalu na kocha wa makipa Bakari Shime.
    Msimu ujao, kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu, mkoa wa Tanga utakuwa na timu mbili Ligi Kuu, zaidi ya Coastal nyingine ni Mgambo FC iliyopanda msimu huu, hivyo kukumbushia enzi zile zile za African Sports ‘Wana Kimanumanu’ na Wagosi hao wa Kaya.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: COASTAL UNION WANAKIPIGA KENYA NA AKINA BANKA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top