• HABARI MPYA

    Friday, August 17, 2012

    BOCCO ADEBAYOR APAGAWISHA SUPER SPORT UNITED IKIJIANDAA KUIVAA PIRATES JUMAPILI

    Bocoo 'Adebayor' akipoza koo baada ya kumaliza mazoezi leo. Picha kwa hisani ya Meneja wa Azam FC, Patrick 'Torres' Kahemele. 

    Na Mahmoud Zubeiry
    WAKATI SuperSport United inajiandaa na mechi ya kwanza ya Nusu Fainali ya MTN8 Jumapili dhidi ya Orlando Pirates kwenye Uwanja wa Peter Mokaba, mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, John Raphael Bocco ‘Adebayor’ amekuwa akiipa changamoto nzuri safu ya ulinzi ya timu hiyo.
    Bocco yupo kwenye majaribio Super Sport tangu Jumamosi na anaendelea na mazoezi na timu hiyo, akiipa mikiki ya kutosha safu ya ulinzi ya timu hiyo kanla ya kuivaa Pirates.
    Tayari wakala wa mshambuliaji huyo wa Azam FC, Yussuf Bakhresa amesema hataweka tamaa ya fedha iwapo mchezaji huyo atafuzu.
    Yussuf anayetambuliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), ambaye awali miaka mitatu iliyopita alimpeleka Israel Adebayor huyo wa Chamaz kwa majaribio na akafanya vizuri, alisema kwamba anachojali ni mchezaji huyo kupata timu itakayompa maslahi bora na kumuendeleza zaidi kisoka.
    “Mimi nataka klabu inayotaka kumnunua iilipe tu klabu yake, mimi sitataka hata senti moja yao, kwa sababu najua wachezaji wa Tanzania bado hawajakubalika sana katika soko la soka ya kulipwa, hivyo kufanya tamaa kunaweza kusababisha umharibie mchezaji mwenyewe wakati mwingine,”alisema Yussuf, ambaye mwaka 2009 alimpeleka Mrisho Ngassa majaribio West Ham United.
    Super Sport ilivutiwa na soka ya Bocco, katika michuano ya Klabu Bingwa ya soka Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, mwezi uliopita, hivyo kumuita kwa majaribio, ambayo akifuzu ataweka historia ya kuwa mchezaji wa pili wa Tanzania kuchezea klabu hiyo, baada ya Suleiman Matola 2005 hadi 2007, akitokea Simba SC.
    Katika Kombe la Kagame, Bocco ambaye ataondoka Jumamosi kwenda kujaribiwa, alifunga mabao matano na kushika nafasi ya tatu katika wafungaji bora, nyuma ya Hamisi Kiiza na Said Bahanuzi wa Yanga, aliyeibuka mfungaji bora.
    Lakini Bocco pia alikuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu uliopita, kwa mabao yake 18 akiwapiku hadi washambuliaji wa kigeni waliocheza ligi hiyo msimu huo, Emmanuel Okwi, Kenneth Asamoah, Davies Mwape na Dalington Enyiana.
    Tangu aipandishe Ligi Kuu Azam FC msimu wa 2008/2009 kwa mabao yake, akiibuka mfungaji bora wa Ligi Daraja la Kwanza, Bocco amekuwa akiingia kwenye mbio za kuwania kiatu cha dhahabu cha Ligi Kuu, msimu wa kwanza akizidiwa na Boniphace Ambani aliyekuwa Yanga, msimu wa pili Mussa Mgosi aliyekuwa Simba na msimu wa tatu na Mrisho Ngassa, kabla ya msimu uliopita kutimiza ndoto zake za kuwa mfungaji bora wa ligi hiyo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BOCCO ADEBAYOR APAGAWISHA SUPER SPORT UNITED IKIJIANDAA KUIVAA PIRATES JUMAPILI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top