• HABARI MPYA

    Saturday, August 18, 2012

    BAKHRESA AFURAHIA MAFANIKIO YA BOCCO ADEBAYOR SUPER SPORT

    Bocco 'Adebayor'

    Na Mahmoud Zubeiry
    WAKALA wa wachezaji anayetambuliwa na Shirikisho la Soka Ulaya (FIFA), Yussuf Said Bakhresa amezipokea kwa furaha habari za mteja wake, John Raphael Bocco ‘Adebayor’ wa Azam FC kufanya vizuri katika majaribio yake kwenye klabu ya SuperSport United ya Afrika Kusini.
    “Nimezipokea kwa furaha sana habari za Bocco na ninamuombea kila la heri, afanikiwe acheze soka ya kulipwa. Ni dhamira yangu muda mrefu kuhakikisha Bocco anacheza soka ya kulipwa na kama utakumbuka niliwahi kumpeleka Ulaya,”alisema Yussuf.
    “Mimi nataka klabu inayotaka kumnunua iilipe tu klabu yake, mimi sitataka hata senti moja yao, kwa sababu najua wachezaji wa Tanzania bado hawajakubalika sana katika soko la soka ya kulipwa, hivyo kufanya tamaa kunaweza kusababisha umharibie mchezaji mwenyewe wakati mwingine,”alisema Yussuf, ambaye mwaka 2009 alimpeleka Mrisho Ngassa majaribio West Ham United.
    SuperSport United itakuwa na mechi ya kwanza ya Nusu Fainali ya MTN8 Jumapili dhidi ya Orlando Pirates kwenye Uwanja wa Peter Mokaba na katika maandalizi ya mchezo huo, ilipata changamoto nzuri kutoka kwa mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Bocco ‘Adebayor’.
    Bocco ambaye byupo kwenye majaribio Super Sport tangu Jumamosi, alikuwa akiipa mikiki ya kutosha safu ya ulinzi ya timu hiyo kabla ya kuivaa Pirates kesho katika mechi kali nay a kusisimua.
    Super Sport ilivutiwa na soka ya Bocco, katika michuano ya Klabu Bingwa ya soka Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, mwezi uliopita, hivyo kumuita kwa majaribio, ambayo akifuzu ataweka historia ya kuwa mchezaji wa pili wa Tanzania kuchezea klabu hiyo, baada ya Suleiman Matola 2005 hadi 2007, akitokea Simba SC.
    Katika Kombe la Kagame, Bocco ambaye ataondoka Jumamosi kwenda kujaribiwa, alifunga mabao matano na kushika nafasi ya tatu katika wafungaji bora, nyuma ya Hamisi Kiiza na Said Bahanuzi wa Yanga, aliyeibuka mfungaji bora.
    Lakini Bocco pia alikuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu uliopita, kwa mabao yake 18 akiwapiku hadi washambuliaji wa kigeni waliocheza ligi hiyo msimu huo, Emmanuel Okwi, Kenneth Asamoah, Davies Mwape na Dalington Enyiana.
    Tangu aipandishe Ligi Kuu Azam FC msimu wa 2008/2009 kwa mabao yake, akiibuka mfungaji bora wa Ligi Daraja la Kwanza, Bocco amekuwa akiingia kwenye mbio za kuwania kiatu cha dhahabu cha Ligi Kuu, msimu wa kwanza akizidiwa na Boniphace Ambani aliyekuwa Yanga, msimu wa pili Mussa Mgosi aliyekuwa Simba na msimu wa tatu na Mrisho Ngassa, kabla ya msimu uliopita kutimiza ndoto zake za kuwa mfungaji bora wa ligi hiyo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BAKHRESA AFURAHIA MAFANIKIO YA BOCCO ADEBAYOR SUPER SPORT Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top