![]() |
| Christopher Edward |
Na Prince Akbar
MSHAMBULIAJI chipukizi wa Simba SC, Christopher Edward leo anatarajiwa kutawazwa kuwa mfungaji bora wa michuano ya BankABC Sup8R baada ya fainali, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Hiyo inatokana na kwamba, Edward anaongoza hadi sasa kwa mabao, akiwa ametimiza mabao matano, akifuatiwa na Shaaban Kisiga ‘Malone’ wa Mtibwa Sugar mwenye mabao matatu.
Na ni kiungo huyu chipukizi wa Simba leo anatarajiwa kuwa mwiba mchungu kwa safu ya ulinzi ya Mtibwa- hasa leo akicheza pamoja na Ramadhan Singano ‘Messi’ an atarajiwa kuwa hatari zaidi.
Messi na Edward, wote wapo pia timu ya wakubwa ya Simba na wamekuwa wakikomazwa hadi timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars chini ya kocha Kim Poulsen.
Kanuni za mashindano haya ni kushirikisha timu zilizoshika nafasi tatu za juu katika Ligi Kuu za Bara na visiwani na mbili zilioongoza katika kupanda Ligi Kuu zote mbili, lakini kwa Bara, Yanga waliokuwa washindi wa tatu msimu uliopita, walijitokea na nafasi yao ikachukuliwa na Mtibwa Sugar ambayo ilishika nafasi ya nne kwenye Ligi Kuu.
Pamoja na nyota huyo wa Simba kuwania ufungaji bora, atapata heshima tu, kwani waandaaji wa michuano hiyo hawajatenga zawadi kwa ajili ya mpachika mabao bora.
Bingwa wa michuano hiyo mipya itakayokuwa ikifanyika kila mwaka, ataondoka na Sh. Milioni 40, mshindi wa pili Sh. Milioni 20, wa tatu Sh. Milioni 15 sawa na wa nne, wakati washiriki wengine wataondoka na Sh. Milioni 5 kila moja.



.png)
0 comments:
Post a Comment