• HABARI MPYA

    Wednesday, April 04, 2012

    KAMATI YA LIGI HAIITENDEI HAKI YANGA, IMEKAA KINAZI

    KAMATI ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania katika kikao chake cha juzi jioni ilifikia uamuzi wa kuipokonya klabu ya Yanga pointi tatu kwa kile ilichokiita kosa kumtumia beki Nadir Haroub Ally ‘Cannavaro’ katika mechi ya ligi hiyo dhidi Coastal Union ya Tanga, Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

    Coastal ilikata rufaa baada ya kufungwa 1-0 na Yanga Jumamosi Uwanja wa Mkwakwani, Tanga ikipinga klabu hiyo kumtumia Cannavaro ambaye inadai alikuwa hajamaliza adhabu yake ya kukosa mechi tatu baada ya kupewa kadi nyekundu kwa vurugu kwenye mechi dhidi ya Azam FC

    Ikumbukwe mwishoni mwa wiki iliyopita, Mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Kamanda Mstaafu wa Jeshi la Polisi, Kanda Maalum Dar es Salaam, Alfred Tibaigana alisitisha adhabu zote zilizotolewa na Kamati ya Ligi, kuwafungia wachezaji watano wa Yanga kwa kufanya fujo kwenye mechi na Azam FC, ikiwemo kumpiga refa.

    Awali, Kamati ya Ligi iliyokutana Machi 12, mwaka huu iliwafungia wachezaji watano wa Yanga kwa tuhuma za utovu wa nidhamu walioufanya kwenye mechi ya Azam FC, Machi 10, mwaka huu, Uwanja wa Taifa.

    Iliyowafungia ni mabeki Stefano Mwasyika aliyempiga ngumi refa Israel Nkongo mwaka mmoja na faini ya Sh Milioni 1, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ mechi sita na faini ya Sh. 500,000, viungo Nurdin Bakari mechi tatu na faini Sh. 500,000 sawa na Omega Seme na mshambuliaji Jerry Tegete.

    Lakini Kamati ya Tibaigana ikawaachia huru wachezji hao baada ya kuridhika na utetezi wa klabu hiyo juu ya adhabu hizo.

    Akitangaza kusitisha adhabu hiyo, Tibaigana alisema kwa mujibu wa taratibu za TFF, Kamati ya Ligi haina mamlaka ya kumfungia mchezaji yeyote wala kutoa adhabu, isipokuwa Kamati ya Nidhamu.

    Baada ya kufuta adhabu zote akidai kwamba Kamati ya Ligi haina mamlaka ya kutoa adhabu, ispokuwa Kamati yake, Tibaigana alipanga kukutana na Wajumbe wenzake wa Kamati hiyo jana kujadili suala hilo.

    Lakini ajabu juzi, Kamati ya Ligi Kuu imekutana tena na kupitia rufaa ya Coastal Union na kuamua kuiopokonya Yanga pointi, jambo ambalo dhahiri haliko sahihi na yeyote hawezi kusita kusema kamati hiyo haikutumia busara kukutana juzi kabla ya Kamati ya Tibaigana kukutana jana.

    Kukutana kwao juzi ni kama kutaka kuzidi kuleta vurugu na kulifanya suala hili liwe kubwa, bila sababu za msingi.



    KAMATI YA LIGI DHIDI YANGA:

    Binafasi nina shaka na Kamati hii ya Ligi Kuu kama inaweza kuitendea haki Yanga katika suala hili kwa ujumla, kutokana na Wajumbe waliomo kwenye kamati hiyo.

    Mwenyekiti ni Wallace Karia huyu ni mtu ambaye Coastal Union ndio imempa tiketi ya kuingia ndani ya TFF, Makamu Mwenyekiti wake ni Said Mohamed kutoka Azam FC, Wajumbe wengine ni pamoja  Damas Ndumbaro ambaye ni mpenzi wa Simba, Geoffrey Nyange huyu ni Makamu Mwenyekiti wa Simba SC na kwenye vikao vingi vya Kamati hiyo yeye ndiye huwa mwenye sauti.

    Hao ni baadhi tu ya Wajumbe, wengine ni Steven Mnguto, Seif Ahmed, Henry Kabera, ACP Ahmed Msangi, Meja Charles Mbuge na Ahmed Yahya.

    Kwa kuzingatia kuwa Yanga inasaka pointi za kutetea ubingwa wake na wapinzani wake wakuu ni Simba SC na Azam, Kamati yenye wajumbe kutoka klabu hizo dhahiri inaweza kufanya chochote kumuangamiza mpinzani wao.

    Lakini hata isifanye hivyo, kwa mgongano wa kimaslahi tu, Mzee Said (Azam), Karia Coastal iliyocheza na Yanga na kufungwa hadi kukata rufaa, Kaburu na Ndumbaro wa Simba, pekee wanaipa hoja Yanga kupinga maamuzi yoyote ya Kamati ya Ligi.

    Ndiyo, Azam na Simba wanashindana nao katika mbio za ubingwa na nafasi ya pili, ambazo hutoa fursa kwa timu kushiriki michuano ya Afrika wakati Coastal ndio ambao waliwafunga, wakakata rufaa.

    Na ukitazama namna ambavyo Kamati hii imekuwa ikikutana haraka sana kujadili masuala yanayoihusu Yanga kuanzia lile la Azam na hili la Coastal, tofauti na ilivyozoeleka katika soka ya nchi hii, wazi unapata wasiwasi juu yake.

    Ni kama kuna ajenda fulani, ambayo inawezekana baadhi ya Wajumbe hawaijui na wanakokotwa tu, lakini hadi kufikia wengine kutotaka kufuata taratibu na kutishia kujiuzulu kulinda maamuzi yao, hakika inatia shaka kama ndani ya Kamati hiyo Yanga inaweza kutendewa haki.

    Kimsingi TFF ilikosea katika kuunda Kamati hii, kwa kuweka viongozi wa juu wa Azam na Simba na Yanga wakamteua Mjumbe tu wa Kamati ya Utendaji, Seif ambaye tena ni wa kuteuliwa si wa kupigiwa kura na wanachama.

    Yanga kama bingwa wa nchi, hata katika uundwaji wa Kampuni ya Ligi Kuu kama ingeanza kufanya kazi mwaka huu, maana yake Mwenyekiti wake ndiye angekuwa Mwenyekiti wa Kampuni hiyo, ila kwa sababu ambazo huwezi kujua sababu zake, Yanga haina uwakilishi wa nguvu kwenye Kamati ya Ligi Kuu.  



    SUALA LA CANNAVARO

    Na kwa sababu haina uwakilishi wa nguvu kwenye Kamati ya Ligi, ndiyo maana adhabu zilizotolewa kwa wachezaji wao zilikuwa kali mno, kwa mfano ya Cannavaro tofauti na uzito wa kosa lake.

    Watu wanajifanya wataalamu wa kutafsiri kanuni na wanatumia fursa hiyo kupotosha mno umma wa wapenda soka nchini hii, hususan katika suala la Cannavaro.

    Refa Nkongo alikiri hadharani kwamba Cannavaro hakupiga ngumi, bali ni Mwasyika ambaye naye mchezaji huyo alikiri na sasa anahaha kuomba radhi hadi Chama cha Marefa ili apunguziwe adhabu.

    Lakini ajabu wanasema Cannavaro kwa kuwa alimkimbilia refa kwa kasi na alipomkaribia akazuiwa na wachezaji wenzake, alitaka kupiga naye anastahili kupewa adhabu sawa na mtu aliyepiga.

    Ndumbaro ni Mwanasheria Kitaalamu, anataka kuwaambia wapenzi wa soka kwamba anayeua na anayetaka kuua wanapewa hukumu sawa? Iweje hivyo wakati katika sheria hizo hizo kuna kipengele cha muuwaji ambaye hakukusudia?

    Bila kuzuiwa na mtu yeyote, Cannavaro inawezekana alikuwa anatishia kwa sababu hata katika sheria watu wanahukumiwa kwa kutishia tu. Lakini bado hukumu ya mtu aliyetishia na aliyetekeleza zipo tofauti.

    Cannavaro hakupiga refa, anaishia kwenye kutishia na kwa sababu hiyo adhabu yake lazima iendane na uzito wa kosa lake na kwa sababu kanuni zipo wazi, ndio maana inatia shaka mno juu ya Kamati hiyo ya Ligi dhidi ya Yanga.



    VITA YA UBINGWA LIGI KUU:

    Azam, Simba au Yanga yeyote anaweza akawa bingwa msimu huu na yeyote anaweza kuwa wa pili na wa tatu mwishoni mwa msimu.

    Simba inaongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 50 baada ya kucheza mechi 22, Azam FC ni ya pili kwa pointi zake 47 baada ya kucheza mechi 22 pia na Yanga iliyocheza mechi 21 ni ya tatu kwa pointi zake 46, bila kutoa zile zilizokatwa na Kamati ya Ligi juzi.

    Kumekuwa kuna tuhuma za muda mrefu kuhusu hujuma na upangaji matokeo katika Ligi Kuu ya Bara ambazo inasikitisha TFF haijazifanyia kazi kwa muda mrefu sasa, ingawa ni kazi nyepesi tu baada ya vyanzo vya ushahidi kupatikana.

    Katika dakika kama hizi ligi inaelekea ukingoni ndipo sasa mapambano ya kile wanachokiita wenyewe ‘fitina’ yanakuwa mazito- sasa iwapo TFF (Kamati ya Utendaji) haitakuwa makini, ligi itaingia doa.



    MUSTAKABALI WA KAMPUNI:

    Klabu za Ligi Kuu zimekuwa katika harakati za kuanzisha Kampuni ya kuendesha Ligi Kuu badala ya ilivyo sasa ligi hiyo kuendeshwa na TFF.

    Hakuna shaka wengi wanajua mimi ni muumini wa kampuni na nimekuwa nikiunga mkono jitihada hizo. Lakini sasa kwa mwenendo wa Kamati tu ya Ligi, ambayo inaundwa na viongozi wa klabu hizo hizo za Ligi Kuu kuonekana kuna dalili za ubinafsi ndani yake napata shaka hata juu ya huo mustakabali wa kampuni.

    Kampuni safi, ipo dunia nzima. Lakini kwa kuwa wajumbe wa Kamati ya Ligi Kuu ndio hao hao viongozi walio kwenye harakati za uundwaji wa Kampuni. Na kuwa kuwa tumekwishasoma picha yao kupitia maamuzi yao dhidi ya Yanga, hakika inatia shaka hata juu ya mustakabali mzima wa hiyo kampuni.



    HITIMISHO:

    Kamati ya Ligi Kuu haikustahili kukutana juzi, ikiwa jana Kamati ya Tibaigana ilipanga kukutana- lakini yote kwa yote kuna dalili za kutosha, Kamati hiyo haiwezi kuitendea haki Yanga kwa sababu za kimgongano wa maslahi. Nawasilisha. Alamsiki.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KAMATI YA LIGI HAIITENDEI HAKI YANGA, IMEKAA KINAZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top