• HABARI MPYA

    Saturday, May 23, 2020

    UNAKATAAJE TWANGA PEPETA KUJIITA KISIMA CHA BURUDANI?

    Na Said Mdoe, DAR ES SALAAM
    KUNA bendi za dansi zimejaaliwa hazina ya nyimbo pendwa, unasikiliza zaidi ya nyimbo kumi na vidole vyako havikushawishi kusogeza mbele hata wimbo mmoja.
    Sitaki kuzungumzia Msondo na Sikinde ambazo unapokuja kwenye suala la nyimbo pendwa ni lazima usalimu amri kwao, ziko kwenye sayari peke yao. Hapa naizungumzia African Stars Band "Twanga Pepeta" ambayo tangu izindue albam yake ya kwanza mwaka 1999, imekuwa mbabe mpya wa muziki wa dansi hapa nchini.
    Sitaigusa  African Stars Band ile iliyoasisiwa na marehemu Mafumu Bilal mwaka 1994, bali andiko langu litaegemea zaidi kuanzia mwaka 1998 baada ya bendi hiyo kufanya mageuzi kwenye muziki wake na kuanza kuutumia mtindo wa Twanga Pepeta.
    Mwaka huo wa 1998 wakati bendi hiyo ikiwa inapiga bila kiingilio kwa nguvu za mashabiki wao au kwa kusaidiwa na mikataba ya baadhi ya makampuni, ndipo ikatokea nafasi adimu kwao na wakaitumia vizuri.
    Tukio hilo lilitokea mwenzi Disemba, Twanga Pepeta wakaalikwa kusindikiza uzinduzi wa albam ya bendi pendwa kwa wakati huo, Diamond Sound. Ilikuwa hatari kila aliyekuwepo ndani ya ukumbi wa Silent Inn Mwenge alistaajabu kwa namna The African Stars walivyoshambulia jukwaa na huo ndio ukawa mwanzo wa mafanikio ya bendi hiyo, watu wakaanza kumiminika wanapotumbuiza, wimbo wao wa “Kisa cha Mpemba” ukatawala vituo vya radio.
    Kama zilivyo Msondo Ngoma na Sikinde, Twanga Pepeta ilikumbana na mitihani mikubwa ya mara kwa mara ambayo kama si uimara, utulivu na uzoefu wa wamiliki basi ingeweza kabisa kuisababishia anguko kuu bendi hiyo.
    Wakati Twanga Pepeta ikianza kustawi kwenye soko la ushindani wa muziki wa dansi mwaka 2000 ikapata pigo la kuondokewa na msanii wake tegemeo, Banza Stone aliyehamia TOT.
    Ilikuwa ni pigo kubwa kwa Twanga hasa kutoka na ukweli kuwa aidha kwa kukusudia au kwa bahati mbaya, bendi hiyo ilijikuta ikimkuza Banza Stone na kumfanya alama yao kubwa na hivyo walilazimika kutumia njia hiyo hiyo kwa Ally Chocky ili kufunika maumivu ya kuondoka kwa Banza. 
    Pengo la Banza likazibwa, Ally Chocky akawa nyota mpya wa bendi akitakata vizuri katika albam ya “Jirani” ikiwa ni ya pili baada ya “Kisa Cha Mpemba” ya mwaka 1999 ambayo ndiyo iliyopambwa vilivyo na makali ya Banza Stone.
    Ndani ya mwaka huo huo wa 2000 Twanga Pepeta ikapata msukosuko mwingine mkubwa wa kuondokewa na wasanii tegemeo akiwemo kiongozi wa bendi Adolph Mbinga na mwimbaji Rogart Hegga ambao walikwenda kuasisi bendi mpya ya Mchinga Sound.
    Pigo hili nalo lilipita salama huku ujio wa albam yao ya tatu “Fainali Uzeeni” ya mwaka 2001 ukiandika historia na kuleta mapinduzi mapya ya muziki wa dansi. Albam hii ikawa ndiyo ya kwanza kwenda kuzinduliwa na bendi zetu ndani ya ukumbi mkubwa na wa gharama, Diamond Jubilee ambao kabla ya hapo ulikuwa ukitumika zaidi kwa maonyesho ya wasanii wakubwa wa kimataifa.
    Mwaka 2002 Twanga Pepeta wakaibuka na albam ya nne “Chuki Binafsi” ambayo nayo ilikuwa moto wa kuotea mbali kabla ya mwaka uliofuata, 2003 kuachia albam ya tano “Ukubwa Jiwe” iliyokuwa na nyimbo zinazotamba hadi leo kama “Walimwengu” na “Aminata”.
    Baada ya hapo, Twanga Pepeta ikiwa kwenye kilele cha mafanikio, ikapata pigo lingine, safari hii ikiwa ni kuondokewa na Ally Chocky ambaye alishajijengea himaya kubwa ndani ya bendi hiyo, akaenda kuanzisha bendi yake ya Extra Bongo huku akizoa baadhi mashabiki wa Twanga. 
    Ulikuwa mtihani mzito sana. Kuelekea maandalizi ya albam mpya, bendi ikatoa nyimbo mbili “Family Conflict” na “African Unity” bila kuwa na ‘staa’ wa ujazo wa Chocky au Banza, wimbo mmoja ukapokewa vizuri, huku mwingine ukichukuliwa kama msindikizaji.
    Lakini miezi michache baadae bendi ikaimarika tena hasa pale aliporejeshwa Banza Stone na kuibuka na wimbo wa “Mtu Pesa” uliokwenda kubeba jina la albam yao ya sita  iliyozinduliwa mwaka 2004, mwaka uliofuata wakaachia albam ya “Safari 2005”.
    Mwaka 2006 wakati kipaji cha Banza Stone kikianza kugubikwa na makandokando mengi ikiwemo migogoro ya hapa na pale ya kiafya huku Ally Chocky aking’ara sana na bendi ya Mchinga Generation, Twanga Pepeta wakachukua hatua iliyoleta mpasuko mkubwa na kupelekea kuzaliwa kwa kundi jipya la Twanga Chipolopolo lililomilikiwa na Aset kama ilivyo The African Stars.
    Ni kwamba Twanga Pepeta waliamua kumruidisha kundini Ally Chocky.  Baadhi ya wasanii wa bendi hiyo wakiwemo Banza Stone, Msafiri Diouf na Victor Nkambi hawakuridhika na hatua hiyo na wakaamua kusuka kundi jipya la Twanga Chipolopolo  ambalo kiasili lilitokana na bendi ya The African Revolotion iliyopitia mitindo kama Chumvi Chumvi, Tam Tam na Diko Diko.
    Majanga hayo hayakuiyumbisha Twanga Pepeta bali yalizidi kuikomaza bendi na licha ya kupata upinzani mkali kutoka kwa ndugu zao wa Chipolopolo, bado iliweza kuibuka na albam kali iliyokwenda kwa jina la “Password”. Mwaka 2007 wakaachia albam ya “Mtaa wa Kwanza” kabla Ally Chocky hajatimkia TOT miezi kadhaa baadae.
    Kutoka hapo Twanga Pepeta ikaamua kusuka bendi bila kutegemea nyota ya mtu mmoja hali iliyopelekea mwaka 2008 kupita bila kushuhudia albam mpya kutoka kwa bendi hiyo, ikiwa ni mara ya kwanza kupitisha mwaka bila albam tangu walivyoanza kufanya hivyo mwaka 1999.
    Ndipo mwaka mwaka 2009 walipoibuka na albam ya “Mwana Dar es Salaam” huku waimbaji wake wengi kama Luizer Mbutu, Chaz Baba, Khalid Chokoraa, Kalala Jr, Rogart Hegga, Saleh Kupaza na Dogo Rama wote wakihakikisha hakuna mtawala kati yao, walifanya kazi kama timu sambamba na marapa Msafiri Diouf na Ferguson. Hivi ndivyo Twanga ilivyo hadi sasa, hata pale walipowahi kuwarudisha kundini watu kama Mwinjuma 
    Baada ya hapo zikafuata albam nyingine tatu “Dunia Daraja” (mwaka 2011), “Nyumbani ni Nyumbani” ya mwaka 2013 na “Usiyaogope Maisha” iliyozinduliwa jijini Mwanza mwaka 2016.
    Miongoni mwa mitihani mikubwa iliyoikumba Twanga Pepeta kati ya mwaka 2010 hadi 2015  ni ya kuondokewa na wasanii nyota katika vipindi tofauti ambapo wengine walienda kuanzisha bendi ya Mapacha Watatu, baadhi walinyakuliwa na Mashujaa Band bila kusahau Extra Bongo, Ruvu Stars Band na Double M Plus. 
    Twanga Pepeta ambayo imekuwa kimbilio la wasanii wengi wa dansi la kizazi kipya, imefanikiwa kufanya maonyesho yake barani Ulaya katika nchi za Uingereza, Uholanzi, Finland na Norway. Mwinyuma Muumini "Kocha wa Dunia" naye amewahi kuitumikia bendi hii katika vipindi vitatu tofauti.
    Kuanzia mwaka 1999 Twanga Pepeta inayojulikana kama Kisima cha Burudani, ndiyo bendi iliyotoa albam nyingi kuliko bendi nyingine yoyote ile ndani ya Tanzania. Ndiyo bendi yenye nyimbo nyingi kuliko yoyote ile katika kipindi cha miaka 21 iliyopita. Albam 13 na nyimbo zaidi ya 80.
    Kuanzia mwaka 1999 Twanga Pepeta ndiyo bendi  iliyosababisha kuzaliwa kwa bendi nyingi kutoka ubavuni kwake, lakini pia Twanga ndiyo bendi iliyodhohofisha bendi nyingi pale ilipokuwa ikipenyeza nguvu yake kwenye usajili na kunyakua wasanii muhimu.
    Katika kipindi fulani kilichodumu kwa zaidi ya miaka mitatu, Twanga Pepeta ndiyo bendi pekee iliyoweza kufanya maonyesho mawili kwa siku moja kwenye kumbi mbili tofauti na watu wakafurika. Ilifanya hiyo kila Jumapili ambapo jioni  ilikuwa Leaders Club Kinondoni na usiku goma likahamia TCC Club Chang'ombe.
    Hii ni moja ya bendi chache sana zenye mtaji mkubwa wa  rasilimali watu,  mashabiki wenye uwezo wa kujitoa kwa hali na mali ili kupigania ustawi wa bendi. Takwimu zisizo rasmi zinaonyesha pia kuwa hii ndio bendi iliyofanya maonyesho mengi zaidi ndani ya miaka 20 iliyopita.
    Wakati Twanga Pepeta ikiwa mbioni kuachia albam yao ya 14 tangu kuanzishwa kwake, nadiriki kusema sioni dhambi yoyote kwa bendi hii hata kama ingejiita Bahari ya Burudani, achilia mbali Kisima cha Burudani.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: UNAKATAAJE TWANGA PEPETA KUJIITA KISIMA CHA BURUDANI? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top