• HABARI MPYA

    Tuesday, May 26, 2020

    CHINA: MWALUSAKO ALINIPIGANIA NIPANGWE YANGA NIKIWA MDOGO

    “Nimepatwa na mshituko mkubwa kupokea taarifa za habari za kifo chako kaka (Lawrence Peter Mwalusako).
    Nikiwa ni muumini wa kukubali uwezo wa mtu na kumuheshimu kwa uwezo wake, sikupaswa kusubiri kulisema hili mpaka umauti umekukuta.
    Napata taabu sana nami kuangukia kwenye kilema tulichonacho Watanzania wengi, kumsifia mtu mara tu anapokua ametuaga duniani.
    Ilikua mwaka 1986 mwishoni, ukiwa mmoja wa wachezaji waandamizi ndani ya klabu ya YANGA na hasa baada kutoka kufika fainali za Afrika Mashariki na Kati pale Dar es Salaam.
    Ulilazimisha mimi nichezeshwe mechi dhidi ya Mwadui ya Shinyanga Uwanja wa Taifa, kwani nimekwishaiva kiuchezaji sasa baada ya kukaa kambini na timu ya wakubwa kwa msimu mzima nikijifunza.

    Marehemu Lawrence Mwalusako (wa pili kushoto waliochuchumamaa katika kikosi cha Yanga SC mwaka 1987. Wa pili kulia waliochuchumaa ni Athumani China.

    Ulikuwa uamuzi mgumu na uliohitaji ujasiri mkubwa kutowachezesha aliyekuwa kapteni wa timu marehemu Juma Mkambi na kumuacha nje pamoja na mkongwe mwingine, Charles Boniface Mkwasa na chipukizi aliyekuwa anakuja juu wakati huo Muhidini Cheupe na kunipanga mimi.
    Lakini juu ya kuwa na wote hao kwenye nafasi moja, wewe ulishikilia na kusimama na uamuzi wako na kuutetea kwa nguvu zako zote mpaka kocha wa wakati huo, Kapteni mmoja wa jeshi la wananchi alisalimu amri na kunipanga kuanza mchezo huu.
    Nikushukuru sana, kwani toka siku ile sijui hata siku yangu nyingine niliyojadiliwa au kukaa nje bila kuanza mechi yoyote katika maisha yangu yote ya mpira mpaka leo hii.
    Hakika uliona mbali na maono yako yalikua ni ya kweli nitakukumbuka daima milele na nakutakia mapumziko mema na ya milele katika safari yetu hii ambayo wewe mwenzetu umetangulia tu nasi tupo nyuma yako tunakufuata,”.
    (Imeandikwa na mchezaji wa zamani wa Yanga SC, kiungo Athumani Abdallah China ambaye kwa sasa anaishi Uingereza)
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: CHINA: MWALUSAKO ALINIPIGANIA NIPANGWE YANGA NIKIWA MDOGO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top