• HABARI MPYA

  Jumamosi, Mei 30, 2020

  MBWANA SAMATTA AFICHUA; “UMALIZIAJI AU KULENGA SHABAHA NDIYO ZOEZI NINALOLIPENDA ZAIDI”

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta amesema kwamba anapenda zaidi kujifunza kufunga mabao kuliko aina nyingine yoyote ya mazoezi.
  Samatta ameposti picha akiwa mazoezini na klabu yake, Aston Villa, Uwanja wa Bodymoor Heath na kuambatanisha na ujumbe; “Zoezi la umaliziaji au kulenga shabaha ndiyo zoezi ninalolipenda zaidi,”.
  Samatta anatarajiwa kuwa mfungaji mpya tishio barani Ulaya na hiyo ni baada ya bao alilofunga akiwa KRC Genk ya Ubelgji dhidi ya Liverpool kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Novemba 5, 2019 Uwanja wa Anfield kuteuliwa Bao Bora la Msimu na klabu yake hiyo ya zamani iliyochapwa 2-1 siku hiyo.
  Ni Januari tu mwaka huu KRC Genk ilimuuza Mbwana Samatta klabu ya Aston Villa baada ya kuwa naye tangu Januari 2016 ilipomnunua TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). 
  Samatta aliyekuwa anacheza Anfield kwa mara ya kwanza usiku wa Novemba 5 mwaka jana, aliifungia KRC Genk bao hilo dakika ya 40 kwa kichwa akimalizia krosi ya kiungo Mbelgiji, Bryan Heynen.
  Mbwana Samatta akiifungia KRC Genk dhidi ya Liverpool kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Novemba 5, 2019 Uwanja wa Anfield
  Na hiyo ilifuatia mabingwa wa Ulaya, Liverpool kutangulia kwa bao la Georginio Wijnaldum dakika ya 14 akitumia makosa ya safu ya ulinzi ya KRC Genk, kabla ya Alex Oxlade-Chamberlain kuwafungia Wekundu wa Anfield bao la ushindi dakika ya 53 akimalizia pasi ya Mohamed Salah.
  Inaaminika ni kazi yake nzuri Anfield na kwa ujumla kiwango chake kwenye Ligi ya Mabingwa ndiyo ilimfungulia milango ya kuhamia England baada ya kusajiliwa Aston Villa kwa dau la Pauni Milioni 10 akisaini mkataba wa miaka minne na nusu.
  Samatta mwenye umri wa miaka 27 sasa, aliibukia klabu ya African Lyon wakati ikiitwa Mbagala Market ya kwao, Mbagala kabla ya kujiunga na Simba SC, zote za Dar es Salaam na baadaye TP Mazembe ya Lubumbashi, DRC ambayo ndiyo haswa ilimkuza kisoka kabla ya kuhamia Ulaya mwaka 2016.
  Samatta aliifunga Genk mabao 76 katika mechi 191 na kwa sasa ndiye Nahodha wa timu yake ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, ambayo ameifungia mabao 20 katika mechi 56 tangu mwaka 2011.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MBWANA SAMATTA AFICHUA; “UMALIZIAJI AU KULENGA SHABAHA NDIYO ZOEZI NINALOLIPENDA ZAIDI” Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top