• HABARI MPYA

    Friday, May 22, 2020

    MECHI ZOTE ZILIZOSALIA ZA LIGI KUU TANZANIA BARA NA MICHUANO YA ASFC KUCHEZWA DAR PEKEE

    Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
    MECHI zilizosalia za Ligi Kuu ya Tanzania Bara inayotarajwa kuanza tena Juni 1, mwaka huu zitachezwa Dar es Salaam pekee katika viwanja vya Taif, Uhuru na Azam Complex.
    Hayo yamesemwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari leo Jijini Dar es Salaam.
    Waziri Mwakyembe amesema kwamba pamoja na michuano hiyo, Dar es Salaam pia watakuwa wenyeji wa Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) iliyofikia hatua ya robo Fainali.
    Akizungumza na Waandishi wa Habari leo, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe amesema kwamba lengo la kufanya hivyo ni kuziepushia gharama ya kusafiri timu zinazoshiriki ligi hiyo.

    “Tunaruhusu ligi nne tu kwa kuanzia kwa uangalizi, ikienda vizuri tutafungulia kote. Tunafungulia Ligi Kuu, tunafungulia Ligi Daraja la Kwanza, Azam Federation Cup na Ligi Daraja la Pili, nafikiri itakuwa nne hizo,”amesema Waziri Mwakyembe.
    Waziri huyo amesema kwamba lengo tumpate bingwa wa ligi hizo, lakini si hivyo tu, tumpate mwakilishi wa Kombe la Shirikisho Afrika.  
    Kuhusu mechi za Ligi Daraja la Kwanza na la Pili, Waziri Mwakyembe amesema kwamba zitachezwa Jijini Mwanza kwenye viwanja vya CCM Kirumba na Nyamagana na kwamba katika mashindano yote mashabiki hawataruhusiwa kungia uwanjani.
    “Kila timu tutairuhusu iwe na idadi kadhaa ya washangiliaji… kusiwe kimya kabisa kama msiba”, amesema Waziri Mwakyembe.
    Machi 17, mwaka huu TFF ilisimamisha ligi zake zote ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kufuatia mlipuko wa virusi vya ugonjwa wa corona duniani kote.  
    Ligi Kuu ilisimama huku Simba SC ikiwa inaongoza kwa pointi zake 71, ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 54 baada ya timu zote kucheza mechi 28, wakati vigogo, Yanga SC ni wa tatu kwa pointi zao 51 za mechi 27 na Namungo wa nne wakiwa na pointi 50 za mechi 28.
    Hali ni mbaya kwa Singida United inayoshika mkia kwa pointi zake 15 za mechi 29, nyuma ya Mbao FC pointi 22 mechi 28, Alliance FC pointi 29, mechi 29, Mbeya City pointi 30 mechi 29 na Ndanda FC pointi 31 mechi 29.
    Na katika ASFC timu zilizofanikiwa kutinga Robo Fainali ni Alliance FC ya Mwanza, Namungo FC ya Ruangwa, Lindi, Ndanda FC ya Mtwara, Kagera Sugar ya Bukoba, Azam FC, Simba SC, Yanga SC za Dar es Salaam na Sahare All Stars ya Tanga, timu pekee ya Daraja la Kwanza.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MECHI ZOTE ZILIZOSALIA ZA LIGI KUU TANZANIA BARA NA MICHUANO YA ASFC KUCHEZWA DAR PEKEE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top