• HABARI MPYA

  Jumapili, Mei 24, 2020

  SIMBA SC KUANZA MAZOEZI YA PAMOJA JUMATANO KUJIANDAA KUMALIZIA LIGI KUU NA ASFC

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MABINGWA watetezi, Simba SC wanatarjiwa kuanza mazoezi ya pamoja Jumatano baada ya kuvunja kambi tangu katikati ya Macho kwa hofu ya mambukizi ya virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa COVID19.
  Akizungumza na Waandishi wa Habari jana Jijini Dar es Salaam, Mtendaji Mkuu wa Simba SC, Senzo Mazingisa Mbatha alisema kwamba wanafurahi kwamba mpira umerudi kuanzia Juni 1 na tayari wameanza mipango yao na wamepanga kuanza mazoezi Jumatano.
  “Wachezaji wetu wote ambao wapo nje ya Tanzania tunawasiliana nao na mmoja kati ya wachezaji hao atakuwepo nchini Jumatatu. Wengine tunatarajia watakuwepo nchini kabla hatujaanza mazoezi,”alisema.
  Mtendaji Mkuu wa Simba SC, Senzo Mazingisa Mbatha akizungumza na Waandishi wa Habari jana Jijini Dar es Salaam

  Aidha, Mazingisa ambaye ni raia wa Afrika Kusini aliongeza kwamba wanajikita kwenye jitihada za kuhakikisha wanatetea taji la Ligi Kuu ya Tanzania Bara na pia kushinda Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC).
  Pamoja na hayo, Simba SC inatarajiwa kuzindua app nyingine; “Hii ya sasa itaenda mpaka mwisho wa msimu. Kuanzia msimu ujao kwa baadhi ya huduma mtumiaji atailipia. Hiyo itakuwa moja ya njia ya mashabiki kuchangia klabu,”aliongeza.
  Ikumbukwe Machi 17, mwaka huu TFF ilisimamisha ligi zake zote ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kufuatia mlipuko wa virusi vya ugonjwa wa corona duniani kote.  
  Ligi Kuu ilisimama huku Simba SC ikiwa inaongoza kwa pointi zake 71, ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 54 baada ya timu zote kucheza mechi 28, wakati vigogo, Yanga SC ni wa tatu kwa pointi zao 51 za mechi 27 na Namungo wa nne wakiwa na pointi 50 za mechi 28.
  Hali ni mbaya kwa Singida United inayoshika mkia kwa pointi zake 15 za mechi 29, nyuma ya Mbao FC pointi 22 mechi 28, Alliance FC pointi 29, mechi 29, Mbeya City pointi 30 mechi 29 na Ndanda FC pointi 31 mechi 29.
  Na katika ASFC timu zilizofanikiwa kutinga Robo Fainali ni Alliance FC ya Mwanza, Namungo FC ya Ruangwa, Lindi, Ndanda FC ya Mtwara, Kagera Sugar ya Bukoba, Azam FC, Simba SC, Yanga SC za Dar es Salaam na Sahare All Stars ya Tanga, timu pekee ya Daraja la Kwanza.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA SC KUANZA MAZOEZI YA PAMOJA JUMATANO KUJIANDAA KUMALIZIA LIGI KUU NA ASFC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top