• HABARI MPYA

  Jumamosi, Mei 09, 2020

  KOCHA WA AZAM FC, MROMANIA ARISTICA CIOABA AFURAHISHWA NA FIFA KUJA NA WAZO KAMA LAKE

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KOCHA Mkuu wa Azam FC, Aristica Cioaba, amefurahishwa na kauli ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) ambayo imeungana na wazo lake la kupendekeza wachezaji wa akiba kuongezwa hadi kufikia watano.
  Wiki mbili zilizopita, Cioaba alizungumza na tovuti ya Azam FC na kupendekeza Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) liongeze idadi ya wachezaji wa akiba kutoka watatu hadi watano Ligi Kuu ya Tanzania Bara itakaporejea.
  Ligi hiyo kwa sasa imesimamishwa kutokana na janga la ugonjwa wa Corona (COVID-19) linaloendelea kuitesa dunia kwa sasa, ambapo ni mwezi mmoja na nusu hivi sasa tokea isimame, ambapo Ciaoba alisema kuwa ili kuwalinda wachezaji na majeraha pale ligi itakaporejea lazima nafasi za wachezaji wa akiba wanaoingia, ziongezwa hadi kufikia tano.

  FIFA nao walikuja na wazo hilo, mwanzoni mwa wiki hii, wakitoa pendekezo kwa Bodi ya Kimataifa ya Kandanda (IFAB) kuongezwa kwa idadi ya wachezaji wa kubadilisha kwenye mechi moja kutoka watatu hadi watano ili kuwapa nafuu makocha na wachezaji baada ya kutocheza muda mrefu kutokana na janga la Corona.
  Akizungumzia hatua hiyo ya FIFA kuungana naye, Cioaba alisema alikuwa na wazo zuri kwa TFF, ambalo wakubwa hao wa soka duniani nao wamekuja nalo.
  “Hili ni wazo muhimu sana kwa sababu ni jambo la kawaida katika kuwalinda wachezaji. Nimefurahia nilikuwa na wazo zuri, ambalo FIFA nao wamekuja nalo,” alisema Cioaba, akizungumza akitokea nchini kwao Romania.
  Wakati huu wachezaji wakiwa majumbani mwao, wakijilinda na maambukizi ya ugonjwa wa virusi vya Corona, Cioaba amekuwa akitoa programu maalumu za kila wiki kwa wachezaji wake kuzifanya ili kujiweka sawa.
  “Nawasiliana kwa karibu sana na Meneja wa timu (Luckson Kakolaki) na wachezaji wote kujaribu kuona wanavyoweza kufanikisha programu ya mazoezi kulingana na mazingira ya majumbani mwao,” alisema.
  Aidha alisema anafurahishwa sana na wachezaji ambao wanafanya mazoezi kwa ukamilifu kulingana na programu anayowapa katika kipindi hiki kigumu.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KOCHA WA AZAM FC, MROMANIA ARISTICA CIOABA AFURAHISHWA NA FIFA KUJA NA WAZO KAMA LAKE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top