• HABARI MPYA

    Sunday, May 24, 2020

    JANGA LA CORONA LIMETUPA ELIMU GANI KWENYE MCHEZO WA SOKA

    Na Ibrah Mkemia, DAR ES SALAAM
    "DUNIA ni Uwanja wa mapambano na kama utakuwa uko timamu basi inakuwa rahisi kwa wewe kushinda mapambao hayo" Binadamu kwa sasa duniani wanashuhudia kitu ambacho kitakuwa historia kubwa hapo baadae kwa vizazi vingi vijavyo. 
    Kwamba kulikuwa na ugonjwa hatari uliotikisa dunia karne ya ishirini na moja (21) nao ni ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaotokana na virusi vya Corona. Kwa kweli dunia ipo kwenye mapambano magumu dhidi ya ugonjwa huu hatari ambao unachukua uhai wa watu kila kukicha. 
    Shughuli nyingi zimesimama ikiwemo sekta ya elimu, michezo na nyinginezo  ambazo kwa kiasi kikubwa imeathiri uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na hata taifa kwa ujumla.

    Ila leo jicho la mwananzengo linaangazia zaidi kwa wanamichezo hususani kandanda, soka kwa wale ambao wamekuwa wakilifuatilia kwa karibu popote pale  walipo ulimwenguni wakiwepo mashabiki, wadau au wanachama, watakuwa wamegundua mengi sana katika soka letu la Tanzania.
    Kuna mengi ambayo tunatakiwa kuyatazama kwa karibu ili kuliweka soka letu kwenye mstari ulionyooka na kuendana na mataifa ambayo yameendelea kimpira. Kupitia shirikisho la soka nchini Tanzania, TFF na pia kwenye vilabu vyetu na hata wale watu wa karibu wanaohusika na mpira wetu hapa nchini wakiwemo wadau wa soka.
    Tukianza kwa Tff ambao ndio wenye dhamana ya kushughulikia mpira wa miguu ndani ya nchi yetu. Na hawa wamekuwa wamekuwa wakiteua kamati mbalimbali ambazo zinasaidia kazi ndogo ndogo ndani shirikisho. Ndani ya izo kamati ipo kamati inayotambulika kama kamati ya saa sabini na mbili(72).
    Hii kamati iliundwa mahususi kwa ajili ya kupitia makosa yanayofanywa na wachezaji, viongozi, walimu, na yeyote ambae anahusika moja kwa moja katika mchezo wa mpira. Na huchukua hatua ya kutoa adhabu kwa mtu au timu itakayofanya makosa husika. Kwa upande mwengine kamati hii imekuwa na manufaa kwani imekuwa ikitoza faini ya kiasi cha pesa kwa walengwa au wanaokutwa na makosa. Na imekuwa ikiongeza mapato kwa shirikisho kwa kufanya hivyo.
    Ila kuna mengi zaidi ya faini ambazo zinaingia kwenye shirikisho. Tusikanyage ganda la ndizi tu bali tutafute hata tutatatuaje mambo au majanga yanapotokea kama hivi sasa. Pindi mnapo fanya vikao vya bodi ya ligi pamoja na vilabu ili kupanga ligi ya msimu husika itaendeshwaje basi kuwe na mipango endelevu au kuwe na maono ya mbele ambayo hata janga likija kwa bahati mbaya liwe linapatiwa uvumbuzi kwa haraka zaidi na kusiwe na mijadala kama hivi sasa.
    Tuamie kwa vilabu sasa ambapo huku ndo kuna matatizo mengi sana, na kila siku wadau wanapiga kelele kuhusu kuendelea kimafanikio kwenye klabu zetu hapa nchini. Vilabu vingi nchini vimekuwa vikitikiswa na ukata wa kifedha, Hii inasababishwa na kutokuwa na uongozi bora ndani ya klabu zao. 
    Baadhi ya klabu nyingi hapa Tanzania  wameshindwa kutambua thamani ya nembo zao za timu (logo). Timu nyingi zimekuwa zikiahangaika kutengeneza chanzo cha mapato ndani ya klabu. Lakini wanasahau kuwa nembo ndani ya klabu ina uwezo wa kuita wadhamini na matajiri wakubwa kuja kuwekeza ndani ya klabu. 
    Bado najiuliza maswali mengi sana kichwani hivi hii ligi ikirejea, sijui kama kuna baadhi ya timu zitaweza hata kusafiri kutoka mkoa mmoja kwenda mkoa mwengine. Wakati huu wa mapumziko mafupi tumekuwa tukiwasikia baadhi ya viongozi wakilia ukata ndani ya klabu zao. Maswali yanakuja kwani hivi vilabu vyetu ni vya wachumia tumbo, Au ndo kama waswahili wanavyosema "Kijungu jiko" kwa maana mpaka mechi zichezwe ndo wachezaji wapate posho na nauli? Au ndo tupate pesa ya kulipa wachezaji mishahara duu! Hii ni aibu.
    Tumeanzisha vilabu ili tuwe omba omba? Au ndo tumeshindwa kabisa kutumia nembo za timu zetu kuweza kuwaita wadhamini. Yaani tumekuwa vipofu wa aina gani kushindwa hata kuliona hili dogo tu mpaka tuanze kupitisha mabakuli kuchangisha kweli. 
    Wadhamini, matajiri wengi wanatamani nembo za timu zetu ili waweze kufanya biashara lakini sasa sisi wamiliki wa nembo wala hatutambui hilo, Tupo tu tumezibana makwapani na hatujui la kuzifanyia. Ni muda sahihi sasa wa timu kuamka na kuanza kutengeneza thamani na ukubwa wa nembo zao ili wafanya biashara waingie na hatimaye timu kuacha kulia ukata kila kukicha.
    Ni wakati sasa wa shirikisho kuweza kutoa wataalamu kwa upande wa masoko ili waweze kuziudumia klabu zetu na pia kuweza kunyanyua ligi yetu ili iwe yenye mvuto na ushindani. Kwani ukata ndani ya hivi vilabu huondoa radha ya ligi kwa timu kuwa dhaifu kuliko wenzie. Kongole kwa Tff kufanikiwa kumpata mdhamini wa ligi sio jambo dogo ila kwa hili linaloendelea tukubali kuchomeka fito ili tujenge nyumba mpya na imara zaidi kwani waswahili walisema "kipya kinyemi ingawa ni kidonda" 
    TFF pamoja na vilabu vyote naimani mtakuwa mmenisikia kama si hivyo basi mtakuwa mmesoma walau ata mistari miwili tu. Wadau wanahitaji soka la nchi yetu lipande kila tunapoamka kutoka usingizini na sio kushuka. 
    "Corona ushatufunza tayari tunakuomba ondoka ili tuyafanyie kazi".
    (Imeandikwa na Ibrah mkemia. kalomoibrahim@gmail.com  +255 715 147 449 na +255 692 945 323 @mkemia_tza)
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: JANGA LA CORONA LIMETUPA ELIMU GANI KWENYE MCHEZO WA SOKA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top