• HABARI MPYA

  Sunday, May 03, 2020

  RAIS DK JOHN POMBE MAGUFULI ASEMA ANAFIKIRIA KURUHUSU LIGI KUU YA TANZANIA BARA IENDELEE

  Na Mwandishi Wetu, Chato
  RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Pombe Joseph Magufuli amesema kwamba anafikiria kuruhusu Ligi Kuu ya Tanzania Bara iendelee kwa sababu hajasikia mwanamichezo hata mmoja kuathiriwa na virusi vya corona.
  Akihutuba wananchi kupitia Televisheni leo Chato, Rais Magufuli amesema kwamba kwa sababu wanamichezo hawajaathiriwa na corona kuwazuia ni kutaka waugue.
  “Siku zinazokuja mbeleni ninafikiria hata kuruhusu ligi iendelee, ili watu wawe wanacheza angalau wanaangalia kwenye TV na kadhalika, tuweke utaratibu mzuri, kwa sababu ninaelewa hata walioathirika na corona sijaona mwanamichezo mmoja yeyote ambaye amedhurika sana kwenye hili,”. “Na hii inadhihiridha wazi kwamba kwa wale wanaofanya mazoezi corona inawakwepa sasa kama tunawazuia hata kucheza mpira maana yake tunawaambia waugue corona,”.
  “Najaribu kusubiri wataalamu wangu wanishauri vizuri, kwamba hata ligi tuendelee kuchezwa, inawezekana tunaweza tukaishi na huu ugonjwa kama wanavyoishi watu wenye ukimwi, wenye suruwa, wenye TB na maisha yakaendelea,”amesema leo Rais Magufuli.


  Rais Magufuli ambaye leo pia alimuapisha Mbunge wa Iramba Magharibi Mheshimiwa Dk Mwigulu Lameck Nchemba kuwa Waziri wa Katiba na Sheria akichukua nafasi ya Dk. Augustine Philip Mahiga aliyefariki duna Mei 1, mwaka huu Dodoma na kuzikwa Iringa jana, amewataka Watanzania kuendelea kuchapa kazi licha ya tishio la virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa COVID19.
  Ikumbukwe Machi 17, mwaka huu TFF ilisimamisha ligi zake zote ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kufuatia mlipuko wa virusi vya ugonjwa wa corona duniani kote.  
  Pia TFF ilivunja kambi ya timu ya taifa, Taifa Stars iliyokuwa inajiandaa na fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) zilizopangwa kuanza Aprili 4 hadi 25, mwaka huu nchini Cameroon ambazo pia zimeahirishwa kwa sababu ya COVID 19.
  Kwa ujumla CAF ilisimamisha mechi zote za kufuzu za mashindano ya Afrika kwa ushauri wa Shirika la Afya Dunani (WHO) kufuatia mlipuko wa virusi vya corona hadi hapo itakapaoamuliwa vinginevyo.
  Ligi Kuu ilisimama huku Simba SC ikiwa inaongoza kwa pointi zake 71, ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 54 baada ya timu zote kucheza mechi 28, wakati vigogo, Yanga SC ni wa tatu kwa pointi zao 51 za mechi 27 na Namungo wa nne wakiwa na pointi 50 za mechi 28.
  Hali ni mbaya kwa Singida United inayoshika mkia kwa pointi zake 15 za mechi 29, nyuma ya Mbao FC pointi 22 mechi 28, Alliance FC pointi 29, mechi 29, Mbeya City pointi 30 mechi 29 na Ndanda FC pointi 31 mechi 29.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: RAIS DK JOHN POMBE MAGUFULI ASEMA ANAFIKIRIA KURUHUSU LIGI KUU YA TANZANIA BARA IENDELEE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top