• HABARI MPYA

  Ijumaa, Mei 08, 2020

  KWA MUZIKI WA DANSI NA TAARAB TEMBO NI MDOGO KAMA UNGO

  Na Said Mdoe, DAR ES SALAAM
  KUNA jambo moja gumu sana kulimeza kwa sisi wadau wa muziki wa Dansi na Taarab, lakini ni ukweli ambao inabidi tuukubali hata kama unaumiza.
  Kwa sasa kwenye soko la muziki hapa nchini, muziki wa Kizazi Kipya (Bongo Fleva), ndio mkubwa zaidi, hakuna cha Dansi wala Taarab, historia imepinduliwa chini juu.
  Wakati muziki wa Dansi na Taarab unafanya vizuri bar, vijana wa Kizazi Kipya wao wanatawala kwenye vituo vya radio na televisheni, katika mitandao ya kijamii, kwenye vyombo vya usafiri, katika kumbi za kisasa, kwenye matamasha makubwa sambamba kupeperusha bendera ya nchi katika soko la kimataifa.

  Kama ni kwenye pori la wanyama, basi muziki wa Bongo Fleva ni mkubwa kama tembo, unaonekana hata kwa mbali. Ukubwa wake hauna kificho.
  Lakini ukweli huu umekuwa mgumu kukubalika kwa wanamuziki na wadau wengi wa Dansi na Taarab, wanaiona Bongo Fleva ni ya kibabaishaji, yenye tungo nyepesi zinachokaa kirahisi.
  Wanamuziki wa Dansi na Taarab wamesahau kabisa kuwa walilishika ipasavyo soko la muziki, lakini ni dharau zao kwa Bongo Fleva ndizo zilizowashusha chini na sasa wanapigwa bao hata na muziki wa Singeli.
  Walemavu wawili wa macho katika kijiji fulani walibahatika kukuta tembo amekufa, basi wakatumia fursa ile ‘kutalii’  kwenye mwili wa mnyama yule mkubwa kupindukia.
  Ndugu zangu wale wakamzunguka tembo yule na kujaribu kuupapasa mwili wake ili kubaini ukubwa wake na walipomaliza kila mmoja akawa na jibu lake.
  Wa kwanza akasema tembo ni mkubwa kama gari, huyu ni yule aliye bahatika kuuzunguka mwili wote wa tembo, lakini yule wa pili ambaye aliishia kushika sikio tu, akasema  kumbe tembo ni mdogo kama ungo.
  Ubishi uliozuka hapo ulikuwa mkubwa sana, hata wapitia  njia walipojaribu kuwasaidia kwa kuwaambia kuwa aliyesema tembo mkubwa kama gari hakuwa mbali na ukweli, bado yule aliyeshika sikio alisisitiza kuwa mnyama yule ni mdogo kama ungo.
  Naam. Hata katika muziki, wako watu kibao wenye fikra kama hizo kuwa tembo ni mdogo kama ungo. Hata utumie njia gani watakubishia kwa nguvu zote.
  Sanaa ni kama mchezo wa ‘draft’, anayecheza hauoni kwa makini kama anvyouona mtazamaji. Hii inaashiria kuwa kama wewe ni msanii  basi ni muhimu kuchukua maoni ya watu wa nje maana wao wana jicho kali kuliko wewe uliye ndani ya gemu.
  Katika makundi yenye watu wabishi na wasiokubali ushauri kirahisi basi wanamuziki na wamiliki wa bendi (hasa za Dansi na Taarab), wanaongoza. Huku ndiko kwenye wataalamu wengi ambao neno 'kukosolewa' ni msamiati mgumu kwao.
  Ni katika Dansi na Taarab  ndipo unapoweza kukutana  na tangazo (poster), la bendi likiwa limepambwa na wanamuziki waliohama kundi zaidi ya mwaka mmoja ulioupita au hata waliofariki.
  Ukihoji unaambiwa mtengenezaji wa tangazo amekosea kwa kuwa  hajui wasanii lakini cha ajabu wahusika  wa bendi ndiyo wanaokuwa wa kwanza kusambaza  (kupost) mitandaoni matangazo hayo yenye makosa ya aibu.
  Ni katika Dansi na Taarab ndiko utakutana na mtu anayeanzisha bendi isiyo na wimbo hata mmoja na inayoishi kwa nyimbo za kunakili kwenye kumbi za vichochoroni. Sijui mmliki huyu ana tofauti gani na mlemavu wa macho aliyesema tembo ni mdogo kama ungo.
  Wakati wanamuziki wa Kizazi Kipya hawaoni choyo kusifia ujuzi wa wasanii wa Dansi, mambo huwa ni kinyume pale unapotaka kujua watu wa Dansi wanajifunza nini kwa wasanii wa Bongo Fleva. Jibu utakalopewa  ni jepesi tu... "Wale si wanamuziki ni wababaishaji, mwanamuziki wa kweli lazima ajue kupiga muziki wa ‘live’."
  Inachukuliwa dosari moja tu na kufanywa kama fimbo, huku mambo mengine kibao mazuri na yenye mafanikio kwa wasanii wa Kizazi Kipya yakifumbiwa macho. Wasanii wengi wa dansi wanaamini Bongo Fleva ni ndogo kama ungo.
  Ni muhimu wasanii wa Dansi na Taarab wakaelewa kuwa njia pekee ya kutanua wigo wa mafanikio katika muziki ni kubadilishana uzoefu na kumegeana ujuzi.
  Mimi bado ni muumini mkubwa wa Dansi na Taarab, naupenda na kuulewa sana, lakini ili kujikwamua basi tunapaswa kuheshimu Kizazi Kipya, tunapaswa kuachana na dhana za kuamini kuwa tembo ni mdogo kama ungo.
  Ni kweli tungo nyingi za Bongo Fleva ni nyepesi, hazidumu, lakini zimepenya kwenye jamii hadi utosini, zinapendwa hivyo hivyo zilivyo.
  Ni kweli kuwa kwenye Dansi na Taarab ndipo utakapokutana na tungo zilizojaa elimu, ala zilizopangwa zikapangika, ufundi wa kupindukia wa uimbaji, lakini sokoni Bongo Fleva iko mbali mno.
  Kutesa kwa zamu, Dansi na Taarab zijipange upya na zijue kuwa vita ni kubwa, imeingia jamii mpya ya mashabiki ambayo haina muda wa kupekua historia, inaangailia kilicho sasa sokoni.
  Dansi na Taarab zipambane  kwenye vita hii kwa kutumia silaha za kisasa, zisitegemee ukubwa na umashuhuri wao wa zamani. Zichukue yale yaliyo mazuri kwa vijana wa Kizazi Kipya na kuyafanyia kazi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KWA MUZIKI WA DANSI NA TAARAB TEMBO NI MDOGO KAMA UNGO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top