• HABARI MPYA

  Alhamisi, Mei 21, 2020

  RAIS MAGUFULI LIGI KUU TANZANIA BARA NA MICHEZO YOTE NCHINI KUENDELEA KUANZIA JUNI MOSI

  Na Mwandishi Wetu, Dodoma
  RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Pombe Joseph Magufuli ameruhuau Ligi Kuu ya Tanzania Bara kuendelea kuanzia Juni 1 baada ya kujiridhisha maambukizi ya virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa COVID19 yamepungua.
  Mheshimiwa Rais Dk Magufuli ameyasema hayo leo wakati akiwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua hivi karibuni, zoezi ambalo lilifanyika Ikulu, Chamwino mkoani Dodoma na kurushwa na Redio, Televisheni.
  “Na katika mtiririko tuliouona juu juu, sina uhakika kama kuna mwanamichezo yeyote aliyefariki hapa Tanzania kwa corona, kwa hiyo kuwa na michezo pia kunasaidia kupambana na corona. Na michezo ipo mingi, kila mmoja na mchezo wake, lakini michezo ni kitu ambacho kinasaidia kupamabana,”amesema Rais Magufuli.
  Mheshimiwa Rais Dk Magufuli amesema kwamba ameamua michezo nayo, ikiwemo Ligi Daraja la Kwanza, la Pili na kadhalika iendelee tena kuanzia Juni 1, mwaka huu.
  Ikumbukwe Machi 17, mwaka huu TFF ilisimamisha ligi zake zote ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kufuatia mlipuko wa virusi vya ugonjwa wa corona duniani kote.  
  Ligi Kuu ilisimama huku Simba SC ikiwa inaongoza kwa pointi zake 71, ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 54 baada ya timu zote kucheza mechi 28, wakati vigogo, Yanga SC ni wa tatu kwa pointi zao 51 za mechi 27 na Namungo wa nne wakiwa na pointi 50 za mechi 28.
  Hali ni mbaya kwa Singida United inayoshika mkia kwa pointi zake 15 za mechi 29, nyuma ya Mbao FC pointi 22 mechi 28, Alliance FC pointi 29, mechi 29, Mbeya City pointi 30 mechi 29 na Ndanda FC pointi 31 mechi 29.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: RAIS MAGUFULI LIGI KUU TANZANIA BARA NA MICHEZO YOTE NCHINI KUENDELEA KUANZIA JUNI MOSI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top